CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetamba kuwa hatua ya wabunge wake kugomea hotuba ya Rais Jakaya Kikwete wakati wa uzinduzi wa Bunge mwaka 2010 ndiyo imezaa mchakato wa Katiba mpya.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, wakati akihutubia wananchi wa mji wa Kahama, mkoani Shinyanga ukiwa ni mwendelezo wa mikutano ya chama hicho kujadili rasimu ya Katiba mpya katika mabaraza yao.
Mbowe alisema kuwa kitendo hicho cha wabunge wao kutoka nje wakati Rais Kikwete alipoanza kuhutubia kilikuwa ni kielelezo cha kupeleka ujumbe kwamba Katiba iliyopo imepitwa na wakati.
“Licha ya ulimwengu mzima kutoelewa na kutushutumu kwa kitendo hicho, lengo letu lilikuwa ni kuishinikiza serikali ya CCM ikubali kufanyika kwa mchakato wa kuanzishwa Katiba mpya ambayo ndiyo njia pekee ya kuelekea katika ukombozi wa wananchi wanyonge,” alisema.
Aliongeza kuwa hatua hiyo ilikuwa moja ya sababu za Rais Kikwete kuridhia kuanzishwa kwa mchakato wa Katiba mpya.
“Tulifanya hivyo kwa nia njema kabisa na baadaye tulianza maandamano nchi nzima kwa lengo hilo hilo,” alisema.
Mbowe alifafanua kuwa jambo kubwa lililowasababisha kusuia na hatimaye maandamano, ni matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, ambayo chama hicho kinaamini yalichakachuliwa.
Alisisitiza kuwa uchakachuaji huo ulisababishwa na Katiba mbovu iliyopo sasa.
“Baada ya kususia hotuba hiyo na kisha maandamano, Rais Kikwete alikubali kukutana na viongozi wa vyama kikiwamo CHADEMA, kwa lengo la kujadiliana na kukubaliana muundo wa uanzishwaji wa mchakato huo,” alisema.
Mbowe alivionya vyama vya siasa kutouchukua mjadala wa Katiba katika sura ya kisiasa zaidi, badala yake alivitaka viwe nyenzo ya kuwezesha wananchi kuandikwa kwa Katiba mpya.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, katika ziara hiyo ya mikutano ya mabaraza ya kujadili rasimu ya Katiba mpya, ameongozana na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika.
No comments:
Post a Comment