Wednesday, August 14, 2013

CCM kwachafuka

 RUSHWA, MIZENGWE VYATAWALA KUMBEBA MEYA
HATIMAYE Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kagera kimewafukuza uanachama madiwani wake wanane, waliokuwa wamesaini hati ya tuhuma za ufisadi, ili kumng’oa Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani.
Hata hivyo, uamuzi huo unadaiwa kulinda ufisadi anaotuhumiwa kufanywa na Amani katika utekelezaji wa miradi mitatu ya upimaji viwanja, ujenzi wa soko la kisasa na kituo cha mabasi.
Madiwani hao wanane pamoja na wenzao saba wa CHADEMA na CUF walisaini hati ya kutokuwa na imani na meya huyo na kuiwasilisha kwa Mkurugenzi wa Manispaa, wakimtaka aitishe kikao ili wapige kura ya kumng’oa tangu mwishoni mwa mwaka jana.
Waliofukuzwa na kata zao kwenye mabano ni Richard Gaspar (Miembeni), Murungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Alexander Ngalinda ambaye pia ni naibu meya (Buhembe), Yusuf Ngaiza ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa wilaya (Kashai), Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendagulo) na Dauda Kalumuna (Ijuganyondo).
Wapinzani waliokuwa wameungana nao ni Dismas Rutagwelela (Rwamisenyi), Israel Mlaki (Kibeta), Winfrida Mukono (viti maalumu), Conchester Rwamlaza ambaye pia ni mbunge wa viti maalumu CHADEMA pamoja na Ibrahim Mabruk (Bilele), Felician Bigambo (Bakoba) na Rabia Badru (viti maalumu - CUF).
Hata hivyo, hatua hiyo imepingwa vikali na baadhi ya viongozi wa CCM ambao wanaamini kwamba kufukuzwa kwa madiwani hao ndilo kaburi la chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao.
“Sijawahi kuona ujinga wa namna hii. Huwezi kufukuza madiwani wanane kwa wakati mmoja halafu chama kikabaki imara,” alisema mmoja wa viongozi waandamizi wa CCM alipohojiwa na Tanzania Daima Jumatano.




Mkakati wa kuwafukuza madiwani hao ulidaiwa kutawaliwa na vitendo vya rushwa na mizengwe ndani ya CCM, vilivyodaiwa kufanywa na baadhi ya viongozi wa chama na serikali Mkoa wa Kagera kwa lengo la kumwokoa meya.
Kwa mujibu wa Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Kagera, Hamimu Mahamud, kura za ndiyo zilikuwa 50 wakati zile za hapana zilikuwa tano.
Hata hivyo, madiwani hao waliovuliwa uanachama walidai kuwa Halmashauri Kuu (NEC) haina mamlaka ya kuwachukulia hatua hizo bali uamuzi huo ulipaswa kupitia NEC wilaya baada ya kujadiliwa na sekretarieti na kamati ya siasa.
Awali katika kuwadhibiti madiwani hao ili wasitimize lengo lao, kutwa nzima ya jana CCM ilifanya vikao viwili vya Kamati ya Siasa na NEC mkoa ili kuwajadili.
Vikao hivyo ni mwendelezo wa vile vitatu vya sekretarieti, kamati ya siasa na NEC vilivyomalizika wiki iliyopita pasipo kufikia muafaka wa hatua za kuwachukulia madiwani hao wanaodaiwa kusaliti chama kwa kuungana na wapinzani.
Wakati CCM wakimlinda meya wao, madiwani hao waliibua tuhuma nyingine nzito kwa vigogo wa chama na serikali mkoa kuwa walitumika kuwarubuni kwa rushwa ili waondoe hoja yao.
Wakizungumza na gazeti hili jana, madiwani hao walisema kuwa kikao cha NEC wiki iliyopita kilimalizika bila kuwachukulia hatua yoyote, lakini wakashangazwa na uamuzi wa katibu wa chama Mkoa wa Kagera.
“Huyu Katibu Revelend Mushi alijipachika jukumu la kutuandikia barua za onyo zinazotutaka tusitende kosa lolote ndani ya kipindi cha miezi sita.
“Lakini tunahoji ni kwanini yeye, Mwenyekiti wake, Costnacia Mliye na Mkuu wa Mkoa, Fabian Massawe wamekuwa mstari wa mbele kumtetea meya. Sisi tunawaonyesha ufisadi wake wao wanamkumbatia,” alisema mmoja wa madiwano hao.
Waliongeza kuwa Rais Kikwete alitambua hoja yao na kuamuru viwanja vigawiwe upya kwa walengwa na ujenzi wa soko la kisasa ufuate utaratibu, lakini wakahoji kwanini chama kinageuza lengo na kutaka kuwafukuza.
“Hivi hii itakuwa CCM ya wapi inayokubali kupoteza madiwani wanane kwa lengo la kumlinda mtu mmoja (meya) asiondolewe? Maana hata Amani akiondolewa leo lazima kiti kitarudi kwetu,” alisema diwani mwingine.
Madiwani hao walikwenda mbali zaidi wakifichua ufisadi uliofanywa na viongozi wa chama ili kufanikisha vikao vya kuwafukuza uanachama.
Walisema kuwa mikutano yote ya chama hufanyika katika ukumbi wa ofisi zao, lakini wakahoji zilikotoka fedha za kulipia vikao vyote hivyo vilivyofanyika katika hoteli ya kitalii ya Walk Guard pamoja na kulipia posho za wajumbe.
Kwa mujibu wa mmoja wa wajumbe waliohudhuria vikao hivyo, gharama ya ukumbi uliotumika kwa siku ni sh 150,000 na kwamba kila mjumbe alilipwa posho ya sh 30,000.
Madiwani hao walidai kuwa fedha hizo ni za kifisadi kwani zilichangishwa kwa nguvu kutoka kwa wafanyabiashara wakubwa na makampuni ya ujenzi waliokuwa wapewe zabuni za ujenzi, wakitishwa kuwa meya aking’oka na wao pia kazi imekwisha.
“Hizi fedha zilikusanywa na mfanyabiashara mmoja (wanamtaja). Kwa siku mbili. Zilikuwa zinatembezwa sh milioni 40 kwetu na viongozi wa CCM ili kutununua tuachane na hoja yetu.
“Sisi tulishasema hatukatai miradi hiyo isipokuwa hatumtaki meya aitekeleze kwa kuwa si muadilifu, aondoke tuchague mtu muadilifu na muwazi. Amani mwenyewe alishinda kwa rushwa sasa amegeukwa,” alisema mmoja wa madiwani hao.
Waliongeza kuwa katika kutafuta huruma ya wananchi, meya Amani amegeuza mgogoro huo kuwa wa udini akidai kwamba madiwani Waislamu ndio wanampinga kwa sababu ni Mkristo.
Hivi karibuni, madiwani hao walimgeuka Rais Kikwete, wakipinga uamuzi wake wa kumtaka meya kumaliza tofauti zake na mbunge wa Bukoba mjini, Balozi Khamis Kagasheki kwa kile walichodai mgogoro huo si ugomvi kati ya wawili hao.
Madiwani hao walipinga kauli hiyo wakisema suluhu ni kupinga ufisadi wa meya, kwani hakuna ugomvi binafsi kati yake na mbunge.
Akihutubia mkutano mjini Bukoba, Rais Kikwete alisema ujenzi wa soko kuu la kisasa katika manispaa hiyo lazima uendelee na kwamba hakuna hoja ya kuendelea na malumbano “yasiyokuwa na msingi”.
Madiwani hao 15 walisema malumbano yaliyopo ni ya msingi kwa kuwa watu watakaobebeshwa deni la kurejesha mikopo inayochukuliwa na meya ni wakazi wa Bukoba, si meya mwenyewe.
Walisema rais ameonekana hafahamu kiini cha mgogoro, kwani kinachopingwa si miradi, bali utaratibu ambao meya ametumia kuanzisha miradi hiyo kifisadi bila kuzingatia maslahi ya wananchi.
Miradi hiyo ni upimaji wa viwanja 5,000 unaodaiwa mkopo wake wa sh bilioni 2.9 kutoka Mfuko wa Dhamana ya Uwekezaji (UTT) haukufuata taratibu, na wananchi hawakushirikishwa ipasavyo.
Tuhuma nyingine ni mradi wa ujenzi wa soko. Meya anadaiwa kusitisha malipo ya ushuru na kutaka kuwaondoa wafanyabiashara bila kufuata utaratibu.
Anatuhumiwa pia kukopa sh milioni 200 kutoka Benki ya Uwekezaji (TIB) bila kibali cha Baraza la Madiwani. Vile vile alitoa taarifa kwenye kikao cha baraza hilo kuwa TIB iliwapa ruzuku ya sh milioni 90, lakini hakueleza misingi yake.
Upo pia mradi wa kuosha magari ambao unadaiwa kutumia kiasi cha sh milioni 297 zinazotiliwa shaka. Ameshindwa pia kutoa mchanganuo wa mapato na matumizi ya mradi ya kiasi cha sh milioni 134, za ujenzi wa kituo cha mabasi.
Kwa mujibu wa kanuni za manispaa hiyo yenye madiwani 24, watatu wa CUF, wanne wa CHADEMA na 17 wa CCM, ili kupitisha uamuzi huo wa kumuondoa meya, ni lazima robo tatu ya madiwani yaani 16, wapige kura ya kuunga mkono hoja hiyo.
Hata hivyo katika orodha hiyo, waliamua kumwondoa Balozi Kagasheki kwa vile ni waziri na sehemu ya serikali.
Hata hivyo, inajulikana kuwa hata Kagasheki anawaunga mkono ingefikia hatua ya kupiga kura ya kutokuwa na imani na meya.

No comments:

Post a Comment