Monday, August 5, 2013

BAVICHA yaivaa Serikali sakata la ajira

BARAZA Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAVICHA), limesema sakata la ajira kwa vijana nchini, ni matokeo ya mfumo mbaya wa elimu ambao hautoi fursa kwa vijana kupata ajira. Baraza hilo limeeleza kuwa elimu inayotolewa ni duni kiasi kwamba haifanyi vijana wengi kuingia katika soko la ushindani katika ajira.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu wa Bavicha, Deogratus Munishi alisema Serikali imeshindwa kuwaandaa wanafunzi wakati wakiwa vyuoni namna ya kulinda rasilimali na badala yake inatumia makongamano kutoa elimu hiyo.

Alisema talizo la ajira ni kubwa na litaongezeka kwa sababu ya mfumo na kiwango duni cha elimu kinachotolewa ambacho kinasababisha zaidi ya vijana 800, 000 kila mwaka kuhitimu masomo yao ya kidato cha nne na vyuo, huku wakiwa hawana uwezo wa kuajiriwa popote na hata kujiajiri wenyewe.

“Serikali ya CCM imekosa maarifa ya kutambua kuwa elimu bora inayokidhi mahitaji ya taifa, ndio njia mojawapo na mwafaka kutatua tatizo la ajira nchini, kwani fursa za ajira zimejaa duniani kote na wanaozifaidi ni wale wenye maarifa na ujuzi ambao msingi wake ni elimu bora waliyopata.

“Kuonyesha kwamba Serikali ya CCM imefilisikia fikra na maono ya kulinasua taifa kutoka kwenye janga hili, sekta ya elimu si kipaumbele kwenye bajeti yake ya mwaka 2013/2014 na hata bajeti zilizopita.

“Kama taifa ni lazima kuwekeza kwenye elimu kwa ufanisi na si kwa ubabaishaji na usanii kama huu unaofanywa na Serikali ya CCM, huku wakishindwa kufanywa mapinduzi ya elimu na wamendelea kuwaweka rehani vijana wa taifa hili.

“Viwanda ndio sekta inayoweza kuajiri watu wa aina yoyote, wenye ujuzi na wasio na ujuzi, wenye elimu na wasio na elimu, lakini Serikali imefubaa kimawazo kulitambua hili.

“Kuimarisha sekta ya viwanda maana yake ni kuinua sekta ya kilimo ambayo ni eneo muhimu la kutatua tatizo la ajira nchini, kwa kujenga uchumi wa viwanda maana yake utahitaji mali ghafi ambazo zinazalishwa hapa nchini. 

“Kujenga viwanda vya kubangua korosho, maana yake unawahamasisha wananchi wa mikoa ya Kusini walime kwa wingi korosho maana unawahakikishia soko la korosho zao,” alisema.

Ili kumaliza tatizo la ajira kwa vijana, ni lazima taifa liwe na viongozi wenye maono mapya ili kujenga misingi bora na kuongeza kwamba ni fedhea kuwa na serikali ya watu waongo wenye kutoa ahadi zisizotekelezeka.

Munishi alisema Serikali imebaki kukimbizana kwa mabomu na vijana mitaani ambao wameona njia ya kujiajiri wenyewe ni kufanya umachinga ambao wameonekana ni nuksi mijini.

No comments:

Post a Comment