HATUA ya kwanza ya mchakato wa katiba mpya ya Tanzania imemalizika kwa kutolewa rasimu ya awali ya katiba.
Mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba, kutokana na maoni ya wananchi, ni kuwa na shirikisho, ijapokuwa katika maelezo hayo upo utatanishi wa hilo litaloitwa shirikisho.
Utata huu unatokana na huo mfumo mpya, badala ya kubadilika na kuwa na jina la Shirikisho bado tunaona uitwe wa Muungano wakati ipo tofauti kati ya Muungano na Shirikisho.
Kinachoshangaza ni kusikia viongozi wa CCM bado wanataka kung’ang’nia mfumo wa serikali mbili na wengine hata kuzungumzia moja. Kwa maana hiyo watu wanaozungumzia haya hawataki kuheshimu maoni ya wengi.
Tumekuwa tukiambiwa, ijapokuwa wengine tumekuwa na shaka na kauli hiyo, kuwa CCM imekuwa ikiongoza nchi kwa ridhaa ya wengi. Tuchukulie kama viongozi wa CCM wanavyotuambia kuwa wao wanayo ridhaa ya wengi ya kuongoza nchi na wanaiheshimu.
Sasa kama ndiyo hivyo, kwanini basi wasiridhie maoni ya wengi yaliyotolewa kwa Tume ya Katiba wakati wa kukusanya maoni?
Au uundaji wa Tume ya Katiba ulikuwa na lengo la kuwahadaa Watanzania na ulimwengu, kama tulivyoona namna ambavyo ripoti za tume mbalimbali nchini zilivyopokelewa na serikali na CCM?
Katika ukusanyaji wa maoni tumeona sauti ya watu wa Visiwani, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakitaka mfumo wa shirikisho la serikali tatu.
Maoni kama hayo pia yametolewa na Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Sasa kwanini CCM haitaki kuheshimu na kukubali maoni ya wengi?
Lakini lililo baya zaidi na kwa kweli inasikitisha ni kusikia baadhi ya viongozi wa nchi kufikia hadi kusema ati wanaotaka serikali tatu wanataka kuvunja Muungano.
Sijui wapi wamepata ujabari wa kusema haya au ndiyo wanataka kutueleza kwamba wachache ndio wenye haki ya kufuatwa na wengi kudharauliwa?
Baya zaidi ni jeuri inayoonyeshwa na baadhi ya viongozi wa chama tawala ya kuwa wanaotaka shirikisho ni wasaliti. Je, wao wanaotaka mfumo wa serikali mbili (au ili kuelekea moja) si wasaliti?
Wapi imeandikwa katika vitabu vitukufu vya Kuran na Biblia kwamba serikali mbili badala ya tatu ndiyo sahihi.
Watu hawa, kwa bahati mbaya wamekuwa na ubavu wa hata kusema wasiotaka serikali mbili wahame nchi na waende kwengine (sijui wapi).
Je, watu hawa wakiambiwa wao wahame nchi na watokomee kwengineko watafurahi? Au ndiyo itakuwa sababu ya kuwafungulia wengine mashitaka ya kutukana viongozi?
Ni vizuri kwa viongozi wetu katika serikali na vyama vya siasa kuchagua maneno wanayoyatamka. Kama hawataki kusulubiwa na wao wasiwasulubu watu wengine. Mawazo ya kila mtu yaheshimiwe.
Kama serikali tatu ni nyingi basi hata hizi mbili ni nyingi ukilinganisha na moja, na ikiwezekana hata hiyo moja baadaye igeuzwe kuwa nusu.
Ni vyema CCM na viongozi wake wakaanza kujenga utamaduni wa kuheshimu mawazo ya wengi yaliyofikishwa katika tume. Anayekataa wingi ni mchawi na hapa tuelewe kwamba Tanzania sio nchi ya wachawi.
Sasa wakati watu wanajdili kilichokuwemo ndani ya rasimu pamezuka hoja mpya Zanzibar na ambayo ninaona inafaa kuzingatiwa.
Nayo ni mgawanyo wa madaraka ndani ya hilo shirikisho linalopendekezwa.
Wapo Wazanzibari waliosema kwa muono wao kilichofanyika ni sawa na watu waliopewa sahani ya wali katika shughuli na kulalamika udogo wa chakula kilichotiwa siniani. Muhimu ni kwa wenye shughuli kuongeza wali katika sinia.
Lakini jingine ambalo nalo halifai kupuuzwa ni kauli za baadhi ya watu juu ya huo mgawo wa madaraka.
Wapo wanaosema neno shirikisho linatokana na ushiriki. Kwa wanavyoelewa wao wanachama wa ushirika wana haki sawa ya madaraka.
Lakini wanachokiona wao katika huo mfumo wa shirikisho unaopendekezwa ni kwa Bara (Tanganyika) kuwa na haki zaidi. Mfano ni idadi ya wajumbe wa pande mbili katika Bunge la Shirikisho kwa Tanganyika (inayotaka kuitwa Tanzania Bara) ni wengi ukilinganisha na wale wa Zanzibar.
Kwa maoni ya watu hawa uwiano sawa wa washirika hawa wawili (nchi mbili huru zilizoungana na sio pande mbili za Tanzania) kuwa na haki sawa.
Dhana iliyochomoza na sasa Visiwani ni kwamba unapokuwa na mmoja kati ya washirika ana sauti kubwa zaidi kuliko mwenzake basi hilo tena sio shirikisho.
Haya ni mambo makubwa na sio madogo. Ninahisi na hili nalo linafaa kuamriwa kwa undani na kwa uadilifu na sio mzaha au propaganda ili panapokuja kuundwa shirikisho pasiwepo mwanya wa kuzuka lawama kama tunavyosikia hivi sasa juu ya mfumo wa Muungano wa serikali mbili.
Ninafikiri njia sahihi ya kulipatia ufumbuzi ni kuwepo kwa kura ya maoni, lakini lilio muhimu zaidi ni nia njema ya kukubali na kuheshimu maoni yatakayotolewa.
Kwa ujumla tatizo linaloonekana katika huu mchakato wa katiba wa baadhi yetu ni kuona hatari ya watawala kutaka kulazimisha fikra zao zikubalike, kuheshimiwa na kuabudiwa.
Mtizamo huu sio sahihi na unaviza utawala wa kidemokrasia, haki na sheria. Ni mtazamo wa zama za kale za watu kutakiwa kuheshimu fikra za moja. Zama hizi zimepitwa na wakati na lazima tubadilike kabla ya wakati haujatulazimisha kubadilika.
Rasimu ya katiba imetolewa. Tutazame njia zipi nzuri za kupita ili tufike huko tunakotaka kwenda kwa salama na amani bila ya kuwepo mtafaruku Bara (Tanganyika) wala Visiwani (Zanzibar).
Tunao wajibu wa kujifunza kwa nchi ambazo ziliungana hapo nyuma na matatizo yaliyojitokeza katika huko kuungana kwao na wengine kuamua; “Na litote tugawane mbao.”
Tujitahidi kuhakikisha jahazi letu halitoti na kugawana mbao au misumari. Kitu muhimu ni kuaminiana, kuheshimiana na kushindana kwa nguvu za hoja na sio vitisho au kutumia ujabari, jeuri na kibri kwa sababu mmoja anashika mpini na mwengine ncha ya kisu.
Tukumbuke kwamba yaliyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba sio maoni ya wajumbe wa tume bali matokeo ya maoni waliyopokea kila pembe ya nchi yetu.
Tuheshimu yaliyowasilishwa na tume na pale tunapohisi pangelifaa kurekebishwa tutoe mapendekezo yetu kwa njia ya kidiplomasia, heshima na adabu.
Kila la kheri Watanzania katika huu mchakato wa katiba. Safari tunaiona ni ngumu, lakini penye nia pana njia. Tuitafute njia sahihi tusije kupoteza mwelekeo
Salim Said Salim
No comments:
Post a Comment