Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa, Benki Kuu, vyama vya siasa na Uhamiaji ni miongoni mwa mambo yapendekezwa kuondolewa katika Rasimu ya Katiba mpya.
Mapendekezo hayo yamo katika kijitabu cha Baraza la Katiba Zanzibar (Bakaza) kilichobainisha maeneo muhimu ya kufanyiwa mjadala wakati wa mikutano ya mabaraza ya katiba ya wilaya.
Mwenyekiti wa Bakaza, Profesa Abdul Sheriff, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa mapendekezo hayo yatakuwa miongoni mwa mambo ya kuelimishwa wajumbe wa mabaraza ya wilaya upande wa Zanzibar.
Alisema hakuna sababu yoyote ya maana ya Jeshi la Polisi na Usalama wa Taifa kuendelea kubaki kama mambo ya Muungano katika mfumo wa serikali tatu uliopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa ja Jaji Joseph Warioba.
Sheriff alisema Ibara ya 217 katika rasimu hiyo ni vema ikafutwa na kuruhusu kila mshirika wa Muungano kuwa na Benki Kuu yake itakayoweka na kusimamia sera za fedha pamoja na kuangalia mwenendo wa uchumi wa mshirika, ikiwamo kudhibiti mzunguko wa fedha wa ndani ya Jamhuri ya Muungano.
“Ni vyema Zanzibar ikawa na mfumo wa sarafu yake na Benki Kuu yake ili iweze kudhibiti na kuendesha uchumi wake bila ya kuathirika na Muungano kama ilivyo kwa Hong Kong na Macau ndani ya Jamhuri ya Watu wa China,” alisema Profesa Sheriff.
Mapendekezo ya Bakaza yameweka sharti kuwa kama suala la Mambo ya Nje litaendelea kubaki chini ya Muungano, basi ni muhimu nafasi za watendaji na mabalozi zitolewe kwa usawa kati ya washirika wa Muungano.
.
Alipendekeza katika Ibara ya 2 ya rasimu hiyo kuingizwe haki ya nchi mshirika wa Muungano kujitoa kwa kutumia utaratibu wa kura ya maoni baada ya wananchi wa mshirika husika kuridhia kupitia kura ya maoni.
Bakaza wameunga mkono wazo la Mwanasheria Mkuu mstaafu, Jaji Mark Bomani ya haja ya kwanza kuitishwa kura ya maoni kwa ajili ya kuwauliza watu wa pande zote mbili kama wanautaka Muungano au la.
Bakaza inatarajia kuanza kutoa elimu kwa wananchi kuhusu yaliyomo kwenye rasimu hiyo katika kipindi ambacho mabaraza ya wilaya pamoja na ya kitaasisi yanajiandaa kukutana kwa ajili ya kuichambua rasimu na kuitolea maoni.
No comments:
Post a Comment