Monday, July 15, 2013

Polisi wakamia CHADEMA, waihofia CCM

WAKATI Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP Said Mwema leo anakutana na waandishi wa habari kuzungumzia suala la vyama vya siasa kuwa na vikundi vya ulinzi, jeshi hilo limeendelea kuwa kimya kuhusiana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumiliki kikundi cha vijana cha Green Guard.
Badala yake polisi wameendelea kukikamia na kutoa vitisho zaidi kwa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kufuatia msimamo wake wa kuendelea na hatua yake ya kuimarisha chama chao kwa ajili ya mafunzo ya ukakamavu kusaidia kujilinda.
Tangu kutolewa kwa tamko la CHADEMA kutaka kuendesha mafunzo kwa vijana wake wa Red Brigade kama wafanyavyo CCM kwa Green Guard, polisi wameendelea kusisitiza kuwachukulia hatua kali za kisheria viongozi wa juu wa chama hicho kutokana na kile walichosema kuunda kikosi cha kijeshi kinyume na sheria.
Juzi msemaji wa polisi, Advera Senso aliweka wazi kuwa wiki hii watachukua hatua kali za kisheria dhidi ya viongozi wa CHADEMA na kuwaonya vijana kote nchini, kukataa kutumiwa na wanasiasa waliodaiwa kutaka kuhatarisha amani ya nchi.
Mbali na polisi, mamlaka nyingine zilizokemea uamuzi wa CHADEMA ni pamoja na Rais Jakaya Kikwete, ambaye alisema kinachotaka kufanywa na chama hicho kimelenga kuhatarisha amani.
Mwenyekiti wa chama cha NCCR Mageuzi, James Mbatia naye juzi alikaririwa akiishambulia CHADEMA kwa uamuzi huo aliouita ni wa hatari.
Hata hivyo, kwa makusudi ama kwa lengo la kukana ukweli, Jeshi la Polisi limekuwa likikwepa mara zote kugusia kuhusiana na CCM kumiliki kikosi cha Green Guard, ambacho baada ya kubanwa na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela alikiri wiki iliyopita kuwa kipo na kinafanya kazi ya kulinda usalama wa viongozi na wanachama katika shughuli zao.
Kadhalika, jeshi hilo limeonekana kupuuza na kutotaka kuzifanyia kazi taarifa za matukio mabaya ya kupiga, kuteka na kujeruhi yaliyofanywa na Green Guard dhidi ya viongozi na wanachama wa CHADEMA.
Hadi sasa sio IGP Mwema, ama afisa yeyote wa ngazi ya juu wa polisi aliyetamka waziwazi kuikemea CCM kama wanavyofanya kwa CHADEMA.
CHADEMA kimeripoti katika Jeshi la Polisi, matukio ya kikatili waliyofanyiwa na vijana hao wa CCM katika mikoa ya Tabora, Dar es Salaam, Mwanza na Iringa, yakiwemo mauaji ya kada wake wa Arumeru mkoani Arusha.
Msimamo wa CHADEMA
Kwa upande wake, CHADEMA imezidi kumtaka IGP Mwema kuweka wazi sababu za msingi zinazomfanya hadi sasa apate kigugumizi na kushindwa kutamka ikiwa ni halali kwa CCM kumiliki kikosi cha vijana kwa ajili ya ulinzi wao, lakini iwe nongwa na dhambi kubwa kwa vyama vingine vya siasa.
Taarifa ya CHADEMA kwa vyombo vya habari jana imelishutumu Jeshi la Polisi kwa kushindwa kuichukulia hatua CCM ambao kwa miaka mingi imehodhi kikosi hicho cha vijana ambacho wamedai kimehusika na matukio mengi ya kikatili.
“Jeshi la Polisi wameshindwa kutoa kauli kwa CCM kumiliki kikundi cha ulinzi, ambacho kimekuwa kikifanya mazoezi ya kijeshi kama kule Igunga, kikituhumiwa kushambulia, kupiga, kuteka na kutesa wapinzani wa CCM.
“Kwa mfano, wabunge Kiwia (Hainess) na Machemli (Salvatory) walishambuliwa Kirumba, Peter Msigwa, akashambuliwa Iringa, Mbwana Masoud akapigwa Igunga, na marehemu Msafiri Mbwambo ambaye waliomuua walitoroka mbele ya polisi wenye silaha mahakamani,” imesema taarifa ya CHADEMA.
Aidha, chama hicho kimesema kuwa hadi sasa hakuna ripoti ya kutekwa na kuteswa kwa Dk. Stephen Ulimboka, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Absalom Kibanda, ukweli wa waliolipua bomu Kanisa Katoliki la Olasiti na katika mkutano wa CHADEMA, Soweto mjini Arusha.
CHADEMA wamezidi kuongeza kuwa Green Guard wameshutumiwa pia kuwashambulia waandishi wa habari nchini, na kuwataja waliofikwa na vipigo hivyo kuwa ni Frederick Katulanda wa Mwananchi, mwaka 2010 katika uchaguzi mkuu huko Kwimba, Munir Zakaria wa Channel Ten huko Bububu Zanzibar na Musa Mkama wa Dira katika uchaguzi mdogo wa Igunga.

No comments:

Post a Comment