Tuesday, July 16, 2013

Mnyika amkalia kooni JK

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amemtaka Rais Jakaya Kikwete, kujitokeza hadharani na kukiri kuwa Ikulu imeshindwa kusimamia kauli aliyoitoa juu ya ujenzi wa kituo kipya cha mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi (UBT).
Pia Mnyika amemtaka Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk. Didas Masaburi ajitokeze ndani ya wiki moja na aeleze sababu ya kumdanganya Rais Kikwete kuwa kituo kipya cha mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi kingekamilika Januari mwaka huu.
Mnyika alitoa kauli hiyo jana alipofanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha mabasi Ubungo kwa ajili ya kujionea miundombinu ya kituo hicho baada ya kufanyika ubomoaji wa awali na kusitishwa kwa huduma muhimu ndani ya kituo hicho.
“Kama rais alitoa agizo na halikusimamiwa, anapaswa arudi na atuambie kuwa ameshindwa kusimamia kauli yake, lakini pia Meya Masaburi aseme hadharani kuwa walimuongopea rais juu ya upatikanaji wa kituo kabla ya Januari mwaka huu, kwa kuwa sasa ni miezi sita imepita na hakuna taarifa yoyote wala maandalizi ya kuwapo kwa kituo hicho,” alisema Mnyika.
Katika ziara hiyo Mnyika alishuhudia adha wanazopata abiria ikiwamo ukosefu wa vyoo vya uhakika, eneo la kujihifadhi wakati wa mvua pamoja na kukosekana kwa gereji ndani ya kituo hicho.
Aidha, abiria walimueleza mbunge huyo namna wanavvyolipa kiingilio katika mageti ya kuingilia ndani huku kukiwa hakuna huduma yoyote wanayopata wakiwa ndani.
Kwa upande wao wafanyakazi wa kada tofauti ndani ya kituo hicho walielezea kero wanazokabiliana nazo baada ya kituo hicho kuvunjwa.
Kwa upande wa madereva walieleza kuwa licha ya Sumatra kuagiza wamiliki wa mabasi ya abiria kuwapatia mikataba ya ajira madereva wao suala hilo halijafanyika mpaka sasa.

No comments:

Post a Comment