Wednesday, July 31, 2013

Nakusalimu tena Jaji Warioba

MHESHIMIWA Jaji Mstaafu, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu, Joseph Sinde Warioba, salaam. Hii ni mara ya pili nakuandikia tena waraka ukiwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Nilifanya hivyo huko nyuma kupitia gazeti tofauti na hili. Katika waraka ule nilikukumbusha kwamba wewe ni mmoja kati ya viongozi wastaafu wa taifa hili wanaoheshimika sana ndani na nje ya nchi. Kariba yako inaendana na viongozi wengine kama Salim Ahmed Salim, Ibrahim Kaduma, na wengineo. Nyinyi mnaheshimika kwa kuwa enzi za uongozi wenu mlitekeleza kwa vitendo kaulimbiu ya “cheo ni dhamana” mkifuata kwa ukamilifu malezi ya kiongozi wenu na kipenzi cha Watanzania hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mheshimiwa Jaji mstaafu, nilipokuandikia makala ile nilikuasa usije ukaitia doa heshima uliyonayo kwa Watanzania. Nilikueleza kwamba chama ulichokulia na kilichokulea, yaani Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimebadilika na hata wewe unalijua.
Nimekuwa nikifuatilia kwa karibu sana kila unapopata nafasi ya kuongea, iwe kwenye vyombo vya habari, makongamano na mikutano mbalimbali. Kauli zako zinaonyesha wazi unaitambua CCM ya sasa iliyopoteza mwelekeo na ndiyo maana ulipozungumza kwenye kongamano lililoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere chini ya Mwenyekiti wake Salim Ahmed Salim, CCM hii ya sasa ilikushambulia sana kupitia kwa katibu mkuu aliyekuwepo, Yusuph Makamba.


Kwa kuyatambua hayo, nilikutahadharisha kwamba CCM hii ya sasa itataka uchukue katiba ya nchi hii ya mwaka 1977 halafu uichape upya na kubadilisha jalada lake lisomeke “Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 2014”.
Nikakutahadharisha kwamba ingekuwa vema kama utashindwa kusimamia maslahi ya nchi basi ujiuzulu nafasi hiyo kuliko kuandika katiba ya nchi ya CCM na si ya Tanzania.
Niliyoyazungumza kwenye waraka wangu wa kwanza ni mengi na nimefurahi kuona umefanya kama nilivyokushauri.
Nilikuomba utumie uwepo wa watu waadilifu, wazalendo na wapenda nchi yao katika tume yako, akina Dk. Salim, Prof. Paramagamba Kabudi, Prof. Mwesiga Baregu, Dk. Sseng’ondo Mvungi, na wengineo, kutuandikia katiba nzuri inayojali maslahi ya wananchi wote.
Nilisema wewe andaa rasimu iliyo bora ili kama Bunge la Katiba lililojaa wana CCM litaichakachua na kuleta kitu wanachotaka, Watanzania waone kwamba tatizo si wewe na tume yako bali CCM na Bunge lake la katiba.
Nimefurahi na nakupongeza sana kwa kuwa rasimu yako inaonekana kabisa umefuata maoni ya wananchi bila kupindisha mambo.
Napenda nikupongeze kwa maeneo machache maana sitaweza kuyaorodhesha yote.
La kwanza ni muundo wa Muungano. Umejali matakwa ya Wazanzibari na Watanganyika walio wengi.
La pili mamlaka ya rais. Ni kama Mungu mtu, ana mamlaka yanayomfanya wakati fulani Mwalimu Nyerere kusema kwamba akiamua kuyatumia barabara anaweza kuwa dikteta kwa mujibu wa katiba.
Kauli hiyo pia nilipata kuisikia kwa Rais Jakaya Kikwete mwaka juzi kwamba akiamua kuitumia katiba ya nchi anaweza kuamuru tu “kamata Dk. Slaa, weka ndani” na ikawa.
Nakupongeza pia kwa kuliangalia suala la Tume ya Uchaguzi na kupendekeza iwe huru na ukaiwekea utaratibu wa kupatikana kwa makamishna wa tume walio huru kweli kweli.
Nakupongeza kwa suala la mawaziri kutokuwa wabunge na kuweka kabisa idadi kikomo ya mawaziri hao. Hili litaizuia serikali kuingilia Bunge kwa sehemu yake. Maana kwa sasa rais ana uwezo wa kuteua mawaziri 100 na hivyo wakati wowote mswaada ama hoja ya serikali inapopelekwa bungeni tayari serikali ina kura 100 kabla ya zile za wabunge wa kawaida wanaoiunga mkono.
Mambo mengine ni kuifanya Tume ya Maadili kuwa na meno, kubadili uteuzi wa wakuu wa majeshi na jaji mkuu, kuondoa nafasi ya waziri mkuu kwenye Serikali ya Muungano, kuweka tunu za taifa, mamlaka ya wananchi kwenye serikali yao, misingi maalumu, mwelekeo wa shughuli za serikali na sera za kitaifa, miiko ya uongozi wa umma, utaratibu mpya wa uteuzi na utendaji wa mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali na mwanasheria mkuu wa serikali, upatikanaji na utendaji wa spika na naibu spika, na kadhalika.
Hata hivyo, isingewezekana kwamba ufanye kazi kubwa hiyo halafu isiwe na kasoro.
Mimi naona kasoro kadhaa kwenye rasimu yako. La kwanza kabisa nakubaliana na Zitto Kabwe kwamba tume yako ilikosea sana kutozungumzia namna Serikali ya Tanganyika itakavyofanya kazi. Kwa kuwa nyinyi ndio mna maoni ya Watanzania wote waliochangia na kudai serikali tatu mlikuwa na haja ya kueleza japo kwa kifupi kwamba katiba za Tanganyika na Zanzibar zikaeje ili kuendana na Katiba ya Muungano ambayo sasa itakuwa ikitambua serikali tatu.
Nahisi kwamba upinzani mkubwa unaopata kwa baadhi ya watu wasiopenda serikali tatu ni kwa sababu hukueleza zitakaaje na zitafanyaje kazi. Sasa niseme kwa kifupi mambo kadhaa katika hili:
Moja, Muungano uwe serikali tatu, lakini kusiwe na marais watatu kama kulivyo na wawili leo. Naungana mkono na Samwel Sitta kwamba wale watakaoongoza serikali za Tanganyika na Zanzibar watafutiwe jina lingine na si kuitwa rais ili taifa liwe na rais mmoja tu.
Nadhani mapendekezo ya Zitto ni sahihi kabisa kwamba kwa kuwa Serikali ya Muungano haitakuwa na cheo kinachoitwa waziri mkuu basi viongozi wa Tanganyika na Zanzibar waitwe Waziri Mkuu wa Serikali ya Tanganyika na Waziri Mkuu wa Serikali ya Zanzibar.
Sijapendezwa pia na suala la wewe kukataa serikali za majimbo kwa sababu eti gharama kubwa.
Serikali za majimbo zitapunguza gharama na zitakuwa ‘effective’ zaidi kwa kuwa zitakuwa na mamlaka kamili. Gharama zitapungua kwa sababu mikoa itaunganishwa.
Jaji, unazifahamu serikali zetu za mikoa za sasa. Nenda pale Arusha, Moshi, Mwanza, Mbeya, rudi hapa Dar kabla ya kwenda kwingineko. Ofisi ya mkuu wa mkoa ni jengo kubwa sehemu nyingine lenye ghorofa kadhaa na watumishi lukuki, lakini wasio na tija.
Tunataka jengo moja tu kama lile la pale Arusha liwe ni ofisi ya gavana wa jimbo na maofisa wake ambao wataitwa maofisa, wakurugenzi, makatibu, ama jina lingine lolote na si mawaziri. Hilo jengo moja tu litaongoza jimbo lenye mikoa kwa mfano mitatu ya Kilimanjaro, Manyara na Arusha yenyewe. Ukifunga ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro pale Moshi na ile ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara pale Babati, hujapunguza gharama? Kama ni suala la wawakilishi kwenye baraza la wawakilishi la jimbo mbona hata leo wapo? Tuna idadi kubwa ya watu wanaoitwa wajumbe wa Baraza la Ushauri la Mkoa kwenye kila mkoa na kwenye kikao chao idadi ni kama ile ya wabunge wa jamhuri. Na kila kikao wanalipwa posho lukuki.
Sasa tunavunja yote kwenye kila mkoa, badala yake tunakuwa na wabunge wa kuwakilisha kila wilaya iliyo kwenye jimbo husika. Gharama iko wapi ukizingatia kwamba kuna watumishi kibao wa mkuu wa mkoa ambao hawatakuwepo?
Ingawa tunataka gavana na wawakilishi hawa wachaguliwe moja kwa moja na wananchi, lakini hiyo haitaongeza gharama maana uchaguzi wao utakwenda sambamba na ule wa rais wa Muungano na mawaziri wakuu wa Tanganyika na Zanzibar na wabunge wote kama tulivyoona Kenya.
Mimi nilitaka sana serikali moja, lakini haiwezekani kwa kuwa Zanzibar wanaogopa kumezwa na ni haki yao. Lakini hatuwezi kuendelea kuwa serikali mbili na hivyo suluhisho ni kuwa na serikali tatu ambayo gharama yake ni sawa tu na kuongeza waziri mkuu mmoja na kuwa na mawaziri wakuu wanaotunzwa na kulindwa kama waziri mkuu tuliyenaye basi.
Nashauri tuwe na muundo wa Tume Huru ya Uchaguzi kutoka juu hadi chini angalau kwenye majimbo. Kuwatumia watumishi wa rais aliyeko madarakani kule kwenye majimbo kusimamia uchaguzi siyo sahihi.
Wasimamizi wa ngazi za kata na vituo vya kupigia kura wanaweza kuwa wanaajiriwa kila uchaguzi na Tume ya Uchaguzi, lakini na wao wasiwe maofisa wa kata na vijiji ama mitaa.
Napinga pia suala la haki nyingi za raia ambazo rasimu inazitoa halafu hapo hapo inaweka maneno “bila kuathiri sheria nyingine za nchi.” Narejea mfano ibara ya 30 inayozungumzia uhuru wa habari halafu hapo hapo ibara ndogo ya (4) ya ibara hiyo hiyo inasema “masharti ya ibara hii yatalazimika kuzingatia masharti ya sheria ya nchi itakayotungwa kwa ajili hiyo…”. Hapa unawapa watawala nafasi ya kutunga sheria itakayokandamiza uhuru wa habari kwa kisingizio cha usalama wa taifa, amani, maadili, haki, na kadhalika.
Mheshimiwa Jaji mstaafu, nimedonoa yaliyo muhimu ambayo yatazingatiwa katika rasimu ya mwisho ya katiba. Ahsante kwa kunisoma.

No comments:

Post a Comment