Wednesday, July 24, 2013

Intelijensia ya polisi ni kwa Mbowe tu?

JESHI la Polisi limeendelea kumlazimisha Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe awasilishe kwao ushahidi wa kuhusika kwa jeshi hilo na mlipuko wa bomu uliotokea mwezi uliopita mkoani Arusha.
Siku ya mwisho aliyokuwa amepewa Mbowe kufanya hivyo ni jana saa nane mchana, ingawa kiongozi huyo amesisitiza msimamo wa chama hicho kuwa hatakabidhi ushahidi huo kwa jeshi hilo bali kwa tume huru ya majaji itakayoundwa na Rais Jakaya Kikwete.
Mbowe alisema kamwe hawezi kwenda kinyume cha msimamo wa chama chake, na badala yake amewataka polisi kumpeleka mahakamani kwa kuwa wao ni watuhumiwa katika sakata hilo.
Pamoja na kwamba hatuungi mkono msimamo wa Mbowe moja kwa moja, lakini tungependa kufahamu iliko intelijensia ya jeshi letu ya kutambua wahalifu kama ambavyo wakuu wake wamekuwa wakijitapa kila wakati.
Mara kadhaa tumeshuhudia jeshi hilo likiingilia mikutano ya CHADEMA kwa kuipiga marufuku muda mfupi baada ya kuwa limetoa kibali kwa kisingizio kwamba intelijensia yao imeonyesha kutakuwepo na vurugu.
Kwa uwezo huo wa polisi kubashiri kuwepo vitendo vya vurugu kabla ya mkutano kufanyika, tunachelea kuuliza ni kwanini uwezo na nguvu hizo visifanyike kuwasaka walipuaji wa bomu jijini Arusha na badala yake wanajiegemeza kumtegemea Mbowe?
Tunahoji umakini wa utendaji kazi wa jeshi letu katika kuchunguza matukio tata na mazito yaliyolikumba taifa hivi karibuni badala yake wanajiegemeza kwenye visingizio vya ajabu.
Kama Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alilieleza Bunge kuwa polisi waliokuwa wanalinda usalama kwenye mkutano huo walimuona mlipuaji, lakini walipotaka kumkamata wananchi wakawashambulia, kwanini hawamsaki sasa?
Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba na Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye wamenukuliwa kwa nyakati tofauti wakisema wana ushahidi kuwa CHADEMA walijilipua wenyewe, kwanini wasiwabane hao wawape ushahidi pia?
Kwa mazingira tata kama haya ya matukio yote mazito yakiwemo ya utekaji na uteswaji wa Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda, mashambulizi ya viongozi wa dini visiwani Zanzibar na sasa milipuko ya mabomu Arusha watuhumiwa kutokamatwa, ni dalili za wazi kuwa jeshi letu linayumba.
Sio nia yetu kulifunza kazi Jeshi la Polisi, lakini sababu hizi za kuegemea ushahidi wa Mbowe pekee wakati vyanzo vya uchunguzi kuhusu mlipuko wa Arusha vimejitokeza vingi vikidai vinao ushahidi, ni dhahiri wanalenga kumwandama kiongozi huyo wa kambi ya upinzani bungeni ili kufifisha tukio hilo kiana.
Hatua ya Mbowe kutopeleka ushahidi wake polisi kwa kiasi fulani inachelewesha ukweli wa jambo hilo kujulikana, lakini sababu za yeye kutofanya hivyo kwa jeshi hilo amezieleza, sasa kwanini asifunguliwe mashitaka ili ushahidi huo ufikishwe mahakamani?

No comments:

Post a Comment