Chadema
kimethibitisha umwamba wake katika siasa za Jimbo la Arusha Mjini, baada ya
kutetea kwa kishindo kata zake nne kwenye uchaguzi mdogo wa udiwani uliofanyika
jana.
Katika
uchaguzi huo uliokuwa unasubiriwa kwa hamu na ambao ulichukuliwa kama kipimo
cha siasa za Arusha ambazo zimekuwa na mvutano mkubwa, Chadema kiliongoza
katikia vituo vyote 136 vya kupigia kura Kata za Elerai, Kaloleni, Kimandolu na
Themi.
Kata
hizo zilikuwa wazi tangu mwaka 2011 baada ya Chadema kuwatimua wanachama wake
waliokuwa madiwani Estomih Mallah(Kimandolu), John Bayo (Elerai), Reuben Ngowi
(Themi) na Charles Mpanda (Kaloleni).
Matokeo
Katika
matokeo yaliyotangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi Kata ya Elerai, Obedi
Meng’oriki mshindi alikuwa Jeremiah Mpinga wa Chadema aliyepata kura 2,047
dhidi ya 1,471 za Emmanuel Laizer wa CCM. Katika Kata hiyo kulikuwa na wagombea
wengine ambao ni John Bayo (CUF; kura 302), Seif Shimba (CCK; kura 3) na
Boisafi Shirima (TLP;1).
Katika
Kata ya Themi, Kinabo Edmund wa Chadema aliibuka na ushindi baada ya kupata
kura kupata kura 674. Msimamizi wa Uchaguzi Kata hiyo, Ezeka Mboya alisema
Kinabo alifuatiwa na Victor Mkolwe aliyepata kura 326 na Lobora Ndarpoi wa CUF
alipata kura 307.
Kata ya
Kaloleni, Msimamizi wa Uchaguzi, Anna Ledisa alimtangaza Kessi Lewi wa Chadema
kuwa mshindi kwa kura 1,470 dhidi ya Emmanuel Mliari wa CCM aliyepata kura 330
na Abbas Mkindi wa CUF aliyepata kura 275 na Ngilishi Pauli wa Demokrasia
Makini aliyeambulia kura mbili.
Kata ya
Kimandolu, Msimamizi wa Uchaguzi, Suleiman Kilingo alimtangaza Mchungaji Rayson
Ngowi wa Chadema kuwa mshindi kwa kura 2,761 na kumshinda Edna Saul wa CCM aliyepata
kura 1,163. Kwa matokeo hayo, Chadema sasa kimefikisha madiwani 12 wakati CCM
kimebakiwa na kumi na moja na TLP kina wawili.
Ushindi
huo wa Chadema una athari kwa nafasi ya Meya wa Jiji la Arusha, Gaudence Lyimo
kwani CCM kina wajumbe 14 tu kwenye Baraza la Madiwani, TLP wawili wakati
Chadema sasa kimefikisha 15. Wabunge wa majimbo na wale wa viti maalumu pia ni
madiwani.
Aidha,
Chadema kina nafasi ya kuongeza kiti kingine cha udiwani kwani Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC), kinatarajiwa kuitisha uchaguzi mdogo Kata ya Sombetini.
Mkurugenzi
wa NEC, Julius Malaba alimwambia mwandishi wetu kuwa tume yake inatarajia
kuitisha uchaguzi mdogo hivi karibuni baada ya kata hiyo kutangazwa wazi na
Ofisi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi.
Malaba
alisema uchaguzi huo utaitishwa baada ya aliyekuwa Diwani wake, Alphonce Mawazo
kujitoa CCM na kujiunga na Chadema hali inayokifanya chama tawala kuwa katika
wakati mgumu kukitetea kiti hicho.
Wachache wajitokeza
Uchaguzi
ulikuwa na idadi ndogo ya wapigakura kulinganisha na chaguzi zilizopita.
Elerai
inayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wapigakura 23,885 waliojitokeza ni 3,824
tu ikifuatiwa na Kimandolu yenye wapigakura 17,209 lakini waliopiga kura ni
3,967.
Kata ya
Kaloleni ina wapigakura 12,674 hata hivyo, waliopiga kura ni 2,292. Themi yenye
wapigakura wachache kuliko zote ikiwa na watu 6,387 lakini waliojitokeza kupiga
kura ni 1,319 tu.
Licha
ya idadi hiyo ndogo, baadhi ya wapigakura waliojitokeza walishindwa kutimiza
dhamira yao baada ya kugundulika dosari kadhaa kwenye vitambulisho vyao na
Daftari la Kudumu la Wapigakura.
“NEC
wamevuruga uchaguzi huu makusudi kwa kuchezea Daftari la Wapigakura kwa nia ya
kukibeba CCM. Haiwezekani waliopiga kura Uchaguzi Mkuu mwaka 2010 leo hii
waambiwe majina yao hayamo kwenye daftari,” alilalamika mgombea udiwani Kata ya
Kaloleni, Abbas Mkindi ‘Darweshi’.
Mkindi
aliyewania kiti hicho kupitia CUF alitoa mfano wa mtoto wake, Omar Othman
mwenye kitambulisho cha mpigakura namba 32479962 alichokitumia mwaka 2010
kuzuiwa kupiga kura baada ya jina lake kukosekana kwenye Daftari hilo. Wapiga
kura wengine, Godchan Msella mwenye kadi namba 32479396 na Richard Minja
mwenye namba 32479311 alizuiwa kupiga kura baada ya kubainika kuwa namba
iliyopo kwenye Daftari ni tofauti na ya kadi yake.
Kutokana
na kuwapo kwa mkanganyiko huo, Makamu Mwenyekiti wa NEC, Hamid Mohamoud Hamid
alilazimika kuwaita wataalamu wa mfumo wa kompyuta (IT), katika Kituo cha
Kupiga Kura cha Kaloleni kusaidia, kazi ambayo ilifanywa na timu iliyoongozwa
na Seif Mtero.
Malaba
alikiri uwezekano wa kutokea tofauti za tarakimu kwenye vitambulisho vya
wapigakura na Daftari la Kudumu la Wapigakura huku akishauri wasimamizi na
mawakala wa vyama kutumia busara kuruhusu wananchi wenye vitambulisho na
maelezo sahihi kupiga kura.
“Tofauti
ya tarakimu kwenye kadi ya mpigakura na Daftari la Mpiga Kura ni kosa la NEC,
hivyo siyo sahihi kuwahukumu wapiga kura kwa kuwanyima haki yao ya kuchagua
viongozi wawapendao,” alisema Malaba.
Amani yatawala
Ukiacha
dosari na idadi ndogo ya wapiga kura, uchaguzi huo ulifanyika kwa amani na
utulivu mkubwa tofauti na hofu iliyokuwapo awali kwamba huenda vurugu
zingeibuka kutokana na mvutano uliopo kati ya vyama vya CCM na Chadema.
Hata
hivyo, kulikuwa na kamatakamata na baadhi ya waliotiwa mbaroni ni wale
waliokutwa na vitambulisho feki vya kupiga kura.
Katika
eneo la Shule za Msingi Kimandolu na Elerai, watu wawili walikamatwa kwa
kukutwa na shahada feki za kura. Kimandolu msichana aliyejitambulisha kwa jina
la Mariamu alikamatwa baada ya kwenda na kadi inayodaiwa kuwa feki.
Mpiga
kura huyo alikamatwa na msimamizi wa uchaguzi ambaye ni Mtendaji wa Kata hiyo,
Selemani Kikingo na kukabidhiwa kwa polisi.
Katika
Kata ya Elerai, Zainabu Mohamed pia alikamatwa kwa tuhuma za kuwa na shahada
yenye utata na baadaye kukabidhiwa polisi.
Katika
maeneo hayo, pia vijana ambao waliokataa kuondoka karibu na vituo baada ya
kupiga kura walikamatwa.
Msimamizi
wa uchaguzi kwa upande wa CCM katika Kata ya Kimandolu, Abraham Joseph
alisema idadi kubwa ya waliojitokeza ilikuwa ni ya vijana.
“Kituo
hiki kina wapiga kura takribani 12,000 lakini kwa hali ilivyo sidhani kama
wanaweza kufika hata wapigakura 4,000,” alisema Joseph.
Katika
Kata ya Themi hali ilikuwa shwari. Makada wa CCM, wakiongozwa na Katibu wa
Mkoa, Mary Chatanda walikuwa wakizunguka katika vituo vyote vya kata hiyo.
Mbunge
wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema na Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la
Vijana (Bavicha), John Heche na Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua
Nassari nao walikuwa wakizunguka katika vituo.
No comments:
Post a Comment