Wednesday, July 17, 2013

CHADEMA wanasa siri za CCM

WAPENYA NGOME YA MWIGULU
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimefanikiwa kunasa siri za mipango ya hujuma zilizokuwa zimeandaliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata nne za Jiji la Arusha, Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Habari kutoka vyanzo mbalimbali vya kuaminika, zimebainisha kuwa CHADEMA katika uchaguzi huo kilifanikiwa kushinda kata hizo baada ya kuvunja ngome ya CCM iliyokuwa ikiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba.
Kwa mujibu wa habari hizo, mipango karibu yote iliyokuwa ikifanywa na CCM, ikiwemo halali na haramu, ilivuja na kufika mikononi mwa wapinzani wao ndani ya muda mfupi hata kabla ya utekelezaji.
Imedaiwa kwamba baadhi ya watu waliokuwa katika kambi ya CCM, waliamua kwa siri kufichua mipango hiyo na kuifikisha kwa mahasimu wao kutokana na kile kilichodaiwa kuchoshwa kushiriki katika mambo ya kidhalimu.
Habari zinasema maofisa kadhaa wa CCM ambao wamekuwa wakiratibu na kusimamia mipango karibu yote miovu dhidi ya wapinzani, waliamua kwenda kinyume na makubaliano hayo, na kwa njia ya siri wakafanikiwa kutoa mpango mzima hadharani.
Mmoja wa maofisa wa CHADEMA ambaye awali alikana taarifa hizo, kabla ya kukiri baada ya kubanwa, amedai zilifikishwa kwao na watu wenye mapenzi mema na nchi.
“Hata nasi awali tulishangaa, lakini tulilazimika kuziamini baada ya kuzifanyia kazi na kubaini kwamba zilikuwa za kweli.
“Kwa mfano taarifa za kuwepo kwa mipango ya kutumbukiza kura bandia, kununua shahada za kupigia kura ilivuja mapema nasi tukaamua kuweka mitego kila mahali tulipoambiwa, kiasi cha kuwafanya washindwe kutimiza lengo lao,” alisema ofisa huyo.
Habari zimezidi kufichua kuwa, kambi hiyo ya CCM ilianza kuyeyuka mapema mchana wa Jumapili, siku ambayo ilikuwa ya uchaguzi, baada ya kuhisi kuwa mambo yao yamekwama kutokana na viongozi na vijana wao kuonekana katika maeneo yote muhimu yaliyokuwa yamepangwa na chama hicho tawala kuendesha hujuma zake.
Chanzo kimoja cha habari cha kuaminika kimeliambia Tanzania Daima kuwa ‘usaliti’ huo wa baadhi ya watendaji wa chama hicho tawala umetokana na kutopendezwa na mtindo wa utendaji kazi za kisiasa unavyoendeshwa na Mwigulu na baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho tawala.
“Wameanza kuchoshwa na siasa za majitaka ambazo zimezidi kulichafua taifa na kuangamiza maisha ya watu.
“Ni kweli tunataka ushindi, lakini wengi hawataki utokane na kuumiza watu ambao wana haki ya kuunga mkono na kufuata chama wanachotaka,” kimesema chanzo hicho, ambacho kimeomba jina lake lisitajwe kutokana na sababu za kiusalama.
Mbali na sababu hizo, taarifa zimebainisha kuwa sababu nyingine zilizowafikisha baadhi ya watendaji wa CCM kusaliti, ni kasi ya CHADEMA kuungwa mkono na wananchi, pamoja na vitisho, na vitendo vingi vya ukatili ambavyo viongozi na wanachama wa chama hicho pinzani wamekumbana navyo.
Hadi sasa, viongozi wakuu wote wa CHADEMA wameonja adha ya polisi kwa kukamatwa, wengine kupigwa na hata kufikishwa mahakamani kwa tuhuma mbalimbali.
“Tunao wanachama waaminifu ambao wamo ndani ya CCM na wamekuwa sehemu muhimu ya intelijensia ya chama chetu,” alitoboa mmoja wa maofisa wa CHADEMA.
Katika uchaguzi huo mdogo wa udiwani katika kata nne za Jimbo la Arusha ambao ulifanyika Jumapili CHADEMA iliweza kushinda kata zote.
Awali uchaguzi huo uliahirishwa mwezi uliopita kutokana na mlipuko wa bomu katika mkutano wa kampeni za CHADEMA uliosababisha vifo vya watu wanne na wengine zaidi ya 70 kujeruhiwa.

1 comment:

  1. fanyeni kazi wala msiogope lolote sisi tupo nyuma yenu tuna monitor mwenendo mzima wa hao "green guard" na tena tuendelee kutii sheria za nchi bila shuruti na pasipo WOGA WOWOTE....Mungu ibariki Tanzania.

    ReplyDelete