Akizungumza juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Stendi ya Malori, Majengo mjini Songea, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema utaratibu wa chama hicho kujadili maoni hayo utatolewa hivi karibuni.
Alisema wamekuwa na dhamira ya kuona Watanzania wanapata katiba inayotokana na matakwa yao kwa ajili ya kusimamia na kulinda masilahi yao, hivyo chama chake hakitafanya mikutano ya ndani au ya siri.
“Tunavyozungumza hapa tayari Mabaraza ya Katiba yameanza kukutana, lakini kama mnavyojua pia asilimia kubwa yametawaliwa na CCM lakini sisi pia na Watanzania wengine wote wanaoipenda nchi yao, tunayo fursa ya kuunda baraza letu, tutakuwa na mabaraza ya katiba nchi nzima, ambayo tutayafanya kwenye mikutano ya wazi ya hadhara. Hatutajifungia ndani kama wanavyofanya wao,” alisema.
Alisema kuna mambo manne ambayo Mtanzania yeyote makini na anayeipenda nchi yake atalazimika kukubaliana na mapendekezo ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Bahati mbaya sana, mambo yote haya manne ambayo kwa kweli ni muhimu sana yakawemo kwenye Katiba Mpya ya Watanzania, CCM wanayapinga. Tunaomba sana Watanzania mambo haya ni muhimu kwanza kuna suala la maadili na miiko ya viongozi, pili kuna suala la tunu za taifa, tatu haki za binadamu na nne ni Serikali Tatu.
“Haya ni kati ya mambo ya muhimu ambayo tunaona ni vizuri yakatajwa na kuzingatiwa kwenye Katiba Mpya, lakini jamaa mengine hawayataki au mengine eti wanataka yasitajwe kwenye Katiba Mpya, bali yaundiwe sheria.
Upotoshaji wa amani
Mbowe alisema kuna propaganda ambazo ama zinafanywa kwa makusudi au kwa kutokujua, zikipotosha maana nzima ya amani ambayo kila Mtanzania hana budi kuipigania. Akimnukuu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwenye hotuba aliyoitoa mwaka 1986, Ukumbi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dar es Salaam, Mbowe alisema ikiwa jamii haina wala haioni matumaini kwa viongozi wao huku haki zikiminywa, amani haiwezi kudumu.
Amjibu Tendwa
Alimtuhumu Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa akisema kauli zake zinahatarisha demokrasia na amani ya nchi.
Mbowe huku akiwahoji wananchi kama wanakubaliana na uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema ya kuimarisha kitengo cha ulinzi na usalama (Red Brigade) kwa kuwapatia mafunzo ya ukakamavu, alisema mtu yeyote mwenye nia mbaya na nchi yake, hawezi kutangaza hadharani. Alisema Chadema kilifanya hivyo kwa nia njema ndiyo maana kilitangaza mchana kweupe.
No comments:
Post a Comment