Tuesday, July 23, 2013

BAVICHA KUWA MWENYEJI WA MKUTANO WA VIJANA WA VYAMA VYA DEMOKRASIA DUNIANI KUANZIA TAREHE 25-30 JULAI 2013 JIJINI DAR ES SALAAM

Baraza la Vijana wa Chadema (BAVICHA) limepata heshima ya kuandaa na kuwa mwenyeji wa mkutano wa bodi ya Umoja wa Vyama vya Demokrasia Duniani (IYDU). Mkutano huu utafanyika kuanzia tarehe 25 -30 Julai, 2013 Jijini Dar es Salaam

IYDU (International Young Democrat Union) ni chombo kinachoundwa na umoja wa mabaraza/jumuiya za vijana kutoka vyama vya kidemokrasia duniani.

Zaidi ya vijana 30 kutoka mataifa 18 duniani, Ujerumani, Hispania, Marekani, Italia, Ugiriki, Romania, Lebanon, Georgia, Finland, Bulgaria, Australia, Nepal, Ureno, Taiwan, Denmark, Togo, Kenya, Uganda, Namibia, Ivory coast na wenyeji Tanzania, watahudhuria mkutano huu mkubwa wa kimataifa.

Katika historia ya IYDU inayoundwa na mataifa 81, Tanzania inakuwa nchi ya kwanza kuwa mwenyeji wa mkutano huu kwa nchi za Afrika zilizoko Kusini mwa Jangwa la Sahara. Hii ni heshima ya pekee kwa BAVICHA, CHADEMA, Vijana wa Tanzania na taifa zima kwa ujumla.


IYDU imeamua kufanya mkutano huu Tanzania kwakuwa imeiona BAVICHA ni taasisi imara na madhubuti ya vijana barani Afrika.

Aidha, kufanyika kwa mkutano huu nchini Tanzania kunatokana na jitihada za BAVICHA za kuhakikisha mazingira ya kisiasa, kijamii na kiuchumi nchini Tanzania yanajulikana duniani kote na hivyo IYDU ikaamua kuja kujionea jinsi uhalisia wa mambo ulivyo zaidi ya yale waliokuwa wakiyapata kwenye ripoti ambazo baraza limekuwa likiwasilisha kwenye vikao mbali mbali vya umoja huu.

BAVICHA itatumia mkutano huu  kwa malengo yafuatayo:
1.  Kuwapatia washiriki wote wa mkutano huu fursa ya kujua mambo yafuatayo;
·         Demokrasia na Mfumo wa vyama Vingi nchini Tanzania
·         Tasnia ya Habari na nafasi yake katika maendeleo ya demokrasia
·         Uzoefu wa kujenga jamii za kidemokrasia kupitia mabadiliko ya katiba
·         Uwezeshaji na hali ya kiuchumi ya Vijana Afrika kwa mtazamo wa Sera za CHADEMA.
·       Fursa na Changamoto kwa vijana wa Jumuiya ya Africa Mashariki

2. Kuitangaza Tanzania katika sekta muhimu ya utalii kwa kuwa tunaamini bado kama taifa hatujafanikiwa kujitangaza vilivyo kupitia nyaja hii. Utalii ni eneo ambalo likitumika vizuri litaweza kusaidia vijana wetu kujikwamua kiuchumi na kuliongezea taifa pato. Hivyo basi washiriki watapata fursa ya kufanya utalii kwa kutembelea hifadhi ya Mikumi na baada ya mkutano baadhi ya washiriki watakwenda kutalii Zanzibar.

Itakuwa ni rai ya BAVICHA kwa washiriki kuwa IYDU iwe balozi wa Tanzania popote itakapokuwa ikifanya vikao vyake katika kuutangaza utalii wa taifa letu.

Mkutano wa IYDU utafunguliwa na Katibu Mkuu wa CHADEMA Dr. W.P Slaa na utafungwa na Mwenyekiti wa Taifa, Mh. Freeman Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

Tarehe 26.07.2013, kutafanyika mkutano katika hotel ya Coral Beach ambapo mada mbalimbali zitawasilishwa na kujadiliwa ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha washiriki kuifahamu Tanzania kwa undani wake. Wawasilishaji mada kwa siku hiyo ni pamoja na Mh. Mabere Marando(Mwanasiasa mwandamizi, wakili wa kujitegemea), Jaji Thomas Mihayo(Jaji Mstaafu, Mwenyekiti wa Tume ya Maadili ya Baraza la Habari Tanzania), Wakili Francis Stolla(Rais wa Chama cha Mawakili Tanzania), Mhe. John Mnyika (Makamu wa Rais mstaafu wa IYDU) na, Jenerali Ulimwengu(Mwandishi  mwandamizi).

Tarehe 29 Julai, 2013, ujumbe wa IYDU utapata fursa ya kuwa na Mazungumzo na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, na , Jumuiya ya Ulaya nchini na kituo cha Sheria na Haki za Binadamu nchini (LHRC)
Pia tunatarajia ujumbe huu wa IYDU kukutana na Spika wa Bunge la Tanzania na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Imetolewa leo tarehe 21.07.2013 Jijini Dar es salaam na;

Deogratias Munishi
Katibu Mkuu – BAVICHA
+255715 887712


No comments:

Post a Comment