MBUNGE wa Viti Maalumu, Mariam Msabaha (CHADEMA) amewataka wanawake wa ndani ya chama hicho kuchukua fursa ya kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.
Msabaha alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na viongozi Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA) katika semina ya kujipanga kwa ajili ya kukitumikia chama chao.
Msabaha ambaye ni Makamu Mwenyekiti BAWACHA upande wa Tanzania Zanzibar, aliwataka wanawake wasikubali kubweteka na kufurahia uongozi wa kupewa.
Alisema ni vema wanawake wakajipanga kikamilifu ili waingie katika kinyang’anyiro cha chaguzi mbalimbali kwa kujiamini zaidi.
“Katika uchaguzi wa mwaka 2014 na 2015, wanawake jitokezeni kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ikiwa ni pamoja na majimbo na nafasi za madiwani ili tupate nafasi, tusisubiri kupewa nafasi za upendeleo,” alisema Msabaha.
Aliwataka wanawake kuwahamasisha wenzao wajiunge na CHADEMA ikiwa pamoja na kujitokeza kupiga kura katika chaguzi.
Alisema wakijitokeza kwenye chaguzi hizo watawachagua viongozi wa CHADEMA na watarahisisha ukombozi.
Msabaha alibainisha kuwa wanalenga kuwa ifikapo mwaka 2015 Bunge liwe na wanawake wengi wa CHADEMA wanatokana na majimbo badala ya kuwa na viti maalumu.
“Sisi wanawake wa CHADEMA hatukubaliani na kuwepo kwa viti maalumu bungeni, tunataka katiba ijayo iweke utaratibu mzuri wa kuwapata wabunge wanawake, lakini siyo kwa mfumo wa viti maalumu.
“Kikubwa zaidi ni wanawake kujitosa majimboni kwa lengo la kugombea ubunge wa jimbo,” alisema Msabaha.
No comments:
Post a Comment