MBUNGE wa Musoma Mjini, Vicent Nyerere (CHADEMA) ameitaka serikali ieleze ni kwanini inawazuia wakulima kuuza chakula nje wakati haina uwezo wa kuwatafutia masoko ya uhakika.
Nyerere alitaka maelezo hayo alipokuwa akiuliza swali la nyongeza kwa kuitaka serikali ieleze ina mikakati gani ya kuwaruhusu wakulima kuuza chakula ama mazao yao nje ya nchi ili waweze kujitafutia soko la uhakika tofauti na hali ilivyo sasa.
Awali katika swali la msingi la mbunge huyo, alitaka kujua ukarabati wa ghala la chakula katika mji wa Musoma maeneo ya Nyakato (Baruti) kama umekamilika.
Aidha, alitaka kujua ni lini ghala hilo litaanza kutumika kuhifadhi chakula ili kupunguza umbali uliopo katika kufuata chakula Shinyanga na maeneo yaliyo mbali.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Mhandisi Injinia Christopher Chiza alisema kwa sasa wakulima wengi wameruhusiwa kupeleka chakula nje, lakini wanapaswa kufuata taratibu.
“Hapa tatizo siyo kupeleka chakula nje ya nchi, lakini kuna magonjwa ambayo yanashambulia mahindi na ugonjwa huo karibu nautolea taarifa hapa bungeni, kwa maana hiyo ninachotaka kusema ni kuwa bora kusafirisha unga badala ya kusafirisha nafaka,” alisema Chiza.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Christina Lissu (CHADEMA) aliihoji serikali ina mipango gani ya kuendeleza kanda ambazo zilitangazwa kuwa ni za Kilimo Kwanza, lakini hazina maghala ya kuhifadhia chakula.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima alisema kuwa ni kweli kuwa zipo kanda mbalimbali ambazo ziliteuliwa kuwa ni za Kilimo Kwanza, lakini zinaweza kukosa maghala ya kuifadhia kutokana na sababu mbalimbali za hali ya hewa.
No comments:
Post a Comment