Sunday, June 30, 2013

Sumaye: Vijana msikubali kununuliwa kwenye Uchaguzi

Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye amewatahadharisha vijana kuwa wanaelekea kwenye uchaguzi mkuu wasikubali kupewa rushwa ya kanga, fulana na fedha na mtu yeyote anayetaka kuingia madarakani.
Akizungumza jana alipokuwa kwenye bonanza la michezo la kikundi cha Ukwamani Jogging kilichopo Kawe, alisema vijana wawe makini katika kuchagua mtu mwenye uwezo wa kuongoza ambaye atajali masilahi ya wananchi wake siyo kwa masilahi yake binafsi.
“Najiuliza kama ninajiamini nataka kugombea Kawe au Arusha au Sumbawanga kama ninafaa na wananchi wananiamini mimi ninafaa na wananchi wananihitaji kwa nini niwachochee kwa kanga au fedha ukiona hivyo huyo hawafai kuwaongoza,” alisema na kuongeza:
“Ukiona mtu anatoa kitu ili achaguliwe hafai kuwa kiongozi kwani uongozi ni mzigo,” alisema Sumaye.
Aliwashangaa watu wazima wanaochukua fedha na kuweka mfukoni kisha wanapita mitaani huku wakisema fulani anafaa kwa kuwa anatoa rushwa na fulani hafai kwa kuwa hatoi kitu chochote.
Sumaye alisema anayetoa fedha ili apewe kura huyo hafai kuwa kiongozi kwa sababu atakuwa anawatumikia watu wake waliompa fedha sio mwananchi ambaye alijitolea kumchagua kiongozi hiyo kwa kumpigia kula halali ili aweze kusaidia kumtatulia kero mbalimbali zinazomkabili.
Alisema kama kuna watu wanaumizwa kwa kuambiwa wanapokea au kutoa rushwa huku akiwa anaendelea na kufanya hivyo aache ili asiendelee kuumizwa na hilo.
Sumaye alisema nchi haiwezi kuwa na maendeleo kama viongozi wataendelea kudidimiza nchi kwa rushwa,ufisadi na kuingiza dawa za kulevya nchini.
Alisema viongozi wanaoleta dawa za kulevya kama ni nzuri wangezitumia lakini hawazitumii matokeo yake wanaoathirika ni vijana ambao wanategemewa kulijenga taifa hili.
“Hatuwezi kudidimiza jamii kwa kuwaletea dawa za kulevya ili watoto wa wenzao waharibikiwe kwa nini wasiwape au kutumia hao viongozi ili waathirike wao wenyewe?” alisema Sumaye.

No comments:

Post a Comment