Sunday, June 23, 2013

Serikali sasa isikilize hoja hizi za wabunge kuhusu bajeti ya 2013/14

Jumatatu ijayo wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watapitisha bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2013/14 iliyowasilishwa bungeni wiki iliyopita.

Bajeti hiyo iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa ya Sh. trilioni 18, itapitishwa baada ya wabunge kadhaa kuitolea maoni kupitia mjadala uliochukua  takribani wiki moja.

Kuna kasoro kadhaa ambazo wabunge waliochangia bajeti hiyo tangu Jumatatu ukiwaondoa wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoundwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walizieleza kwa undani.

Moja ya mambo yaliyokosolewa sana na wabunge wengi ni mapendekezo ya bajeti hiyo ya kuweka tozo kwenye huduma za simu wakisema kuwa hali hiyo itawaumiza zaidi wananchi wa kawaida.

Walisema serikali isiongeze kodi kwa wananchi bali itafute njia nyingine mbadala kwamba wafanyakazi wamepunguziwa kwa kiasi kidogo kodi ya mishahara (PAYE), lakini bajeti inawaongezea kodi hiyo katika matumizi ya huduma za simu, mafuta ya dizeli, vinywaji baridi, pombe na sigara.

Eneo lingine lililokosolewa ni utaratibu wa serikali kununua magari ya kifahari na vitu vingine kama kompyuta kupitia watu wa kati badala ya kununua moja kwa moja kutoka kwa watengenezaji.

Walisema kuwa utaratibu wa kufanya manunuzi hayo kupitia kwa mtu wa kati yanaongeza gharama kwa serikali na kwamba kama ingenunua moja kwa moja kutoka kwa watengenezaji fedha nyingi za walipa kodi zingeweza kuokolewa na kutumika katika huduma muhimu za jamii.

Matumizi makubwa ya fedha za serikali pia yalilalamikiwa na wabunge kwamba bado serikali inaendelea kutumia fedha nyingi katika mambo yasiyo ya lazima wala tija kama safari, posho, semina, ununuzi wa mafuta na vilainisho.

Kwamba kwa miaka mingi serikali imekuwa ikielekeza fedha nyingi kwa matumizi hayo na kwamba fedha hizo zinatumiwa na baadhi ya watumishi wa serikali pamoja na watu wengine kwa masuala ya anasa.

Mmoja wa wabunge alisema hakuna sababu ya kutoza tozo, kodi wala ushuru kwa sababu matumizi ya serikali yamekuwa makubwa bila sababu za msingi.

Misamaha ya kodi inayotolewa na serikali vile vile ilipingwa vikali na wabunge wakisema kuwa kwa muda mrefu imekuwa ikilalamikiwa na watu wengi, lakini serikali imekaa kimya bila kuchukua hatua.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ililalamikiwa kwa  kutopanua wigo wa vyanzo vya mapato na kushindwa kukusanya kodi kikamilifu hususani kwa makampuni makubwa ya wawekezaji badala yake serikali inang’ang’ania kuongeza kodi katika bidhaa za sigara, vinjwaji baridi na pombe.

Walionya kuwa, kushindwa kuainisha vyanzo vipya vya mapato kumesababisha baadhi ya wananchi kuacha kuzitumia bidhaa ambazo serikali inaziongezea kodi kila mwaka.

Tozo katika mafuta pia imelalamikiwa na wabunge kwamba itasababisha kupanda kwa nauli pamoja na bidhaa nyingine.

Kuna maoni pia kwamba bajeti ya mwaka 2013/14 haionyeshi matumaini ya kukabiliana na changamoto kadhaa kama maradhi, uharibifu wa mazingira, mfumuko wa bei, ajira kwa vijana na uhakika na usalama wa chakula. 

Kwa kuwa mambo haya yamezungumziwa na wabunge wengi, ni wajibu wa serikali kuyachukua na kuyapitia kwa makini ili kuona kama kuna haja ya kuchukua hatua.

Wabunge kama wawakilishi wa wananchi wametoa ushauri huo kwa serikali kutokana na kufahamu mazingira halisi wanayoishi wananchi wao pamoja na changamoto zinazowakabili.

Baadhi ya hoja za wabunge zimebeba ukweli kwa mfano, tozo katika mafuta ni dhahiri itaongeza ugumu wa maisha kwa sababu bei ya mafuta itapanda na kusababisha huduma na bidhaa pia kupanda.

Kwa mfano, nauli zitapanda tena ikiwa ni muda mfupi baada ya kupandishwa Aprili mwaka huu na kusababisha hali ngumu zaidi kwa wananchi.

Kuweka tozo katika simu pamoja na kwamba kunaiongezea serikali mapato, lakini hatua hiyo itaikwaza serikali katika jitihada zake za kutaka kuboresha huduma za mawasiliano vijijini ambako idadi kubwa ya Watanzania wanaishi.

Bila shaka serikali itakuwa tayari kusikiliza kilio hiki na itafanya marekebisho wakati Waziri Mgimwa atakapokuwa anafunga mjadala wa hotuba yake.


Mhariri NIPASHE

No comments:

Post a Comment