Sunday, June 16, 2013

Ni CHADEMA yataka kura za huruma au ni CCM yataka kuwadanganya wenye fikra pevu?

Nasikitika sana kwa yote yaliyotokea Arusha. Mungu awapumzishe kwa amani ndugu zetu waliotangulia, awaponye haraka majeruhi, atufariji sote kwa maana sote tu wafiwa na kubwa atuoneshe njia ya kuweza kuwashika watuhumiwa.

Tangu jambo hili baya la kigaidi litokee kila mtu amekuwa akisema lake, nami naomba niseme langu, hilo langu lionekane kama maoni yangu tu na si njia muafaka kuwapata washukiwa. Mimi nalitazama lile tukio katika nukta nne, kwa nukta hizo waweza kuniona kuwa sina msimamo mmoja na makhususi au sieleweki ni nini hasa nakiamini. Niseme kuwa nimelitazama tukio lile kwa kuzingatia zaidi namna ya watanzania walivyolipokea.

MOSI: CHADEMA YATAKA KURA ZA HURUMA?
Hiti tukio hili la Arusha linamjenga nani kisiasa kati ya CCM na CHADEMA? Kwakuwa tukio hili limetokea katika mkutano wa CHADEMA, hivyo basi ni rahisi kwa tukio lile kuijenga CHADEMA. Hivi kwa uhasama uliopo kati ya CHADEMA na CCM, CCM inaweza kufanya vile bila kuogopa kudhaniwa kuwa inahusika? Hivi CCM haijui kuwa kwa tukio lolote baya litakalokipata CHADEMA itahisiwa yenyewe CCM kuhusika? Kama CCM inayajua haya, iweje ikafanya upuuzi ambao kwa vyovyote vile utatoa mtaji kwa CHADEMA? Niseme tu kwamba, tukio lile litaanza kutumika na viongozi na makada wa CHADEMA katika hotuba mbalimbali. Nafikiri tumeshaanza kuona kwenye mitandao jinsi watu CHADEMA wanavyolitumia katika siasa.

Kwakuwa tukio linaijenga CHADEMA kisiasa, je tukihisi kuwa mfanyaji wa tukio alijua kuwa litaijenga CHADEMA kisiasa tutakosea? Kama hatukosei, tukisema kuwa CHADEMA imejilipua ili izoe huo mtaji wa kisiasa tutakosea? Haya maswali kwa vyovyote vile atajiuliza mtu mwerevu. Wengi wao wameshajiuliza na wameshapata sababu ya kuihusisha CHADEMA na ushenzi ule. Sasa wanaamini kuwa CHADEMA imefanya vile ili ipate kura za huruma, wewe waonaje? CHADEMA ndio imefanya hivyo? Jibu lako weka kapuni huenda litakusadia katika kufanya maamuzi katika siku ya uchaguzi wa mwaka 2015, naam, hivyo ndivyo wanasiasa wa Tanzania wanavyotaka, wanafanya ushenzi ili wapate kuathiri maamuzi ya umma kupitia ushenzi wao, nitawachukia sana wanasiasa kama kweli hili tukio lina mkono wao.

Bonyeza Read More Kuendelea

PILI: CCM YATAKA KUWADANGANYA WENYE FIKRA PEVU?

Katika hiyo mosi ya hapo juu, wenye fikra pevu watajiuliza maswali yatakayo waaminisha kuwa CHADEMA imejilipua. Kwa werevu ni rahisi kuamini kuwa CHADEMA imehusika kwani ni vigumu kwao wao(werevu) kuamini kuwa CCM imefanya hivyo ili hali hao (CCM) wanajua pasinali kuwa hili suala litaijenga CHADEMA. 

Kama hivyo ndivyo, hivi tukisema kuwa CCM imefanya hivi ili CHADEMA ionekane inawekeza mtaji wa kisiasa kupitia damu za watanzania tutakosea? Hivi tukisema kuwa mfanyaji wa tukio lile alijua kuwa werevu wataishukia CHADEMA badala ya CCM tutakosea? Kama ndivyo tukisema kuwa ni CCM imefanya vile ili kuwadanganya werevu hata waione CHADEMA ni chama cha kigaidi pia tutakosea? Hivi kwa hili tukio CCM hawapati faida mbili? Ya kwanza si ya kuwatisha watu wasiende kupiga kura? Ya pili si kuiba kuku na kisha manyoya kutupa kwa jaa la nyumba la jirani?
Hivi kwa STATUS za Juliana Shonza na Mtela Mwampamba zinazoishutumu CHADEMA kuwa inataka kura za huruma si kishiria tosha kuwa CCM imefanya vile ili watu wenye tafakuri kubwa wadhani kuwa CHADEMA imehusika? Kwa hivyo CCM imehusika? Wewe wadhani CCM imehusika? Usijbu, utaratibu ni uleule, jibu lako weka kapuni huenda litakusadia katika kufanya maamuzi siku ya uchaguzi wa mwaka 2015, naam, hivyo ndivyo wanasiasa wa Tanzania wanavyotaka, wanafanya ushenzi ili wapate kuathiri maamuzi ya umma kupitia ushenzi wao, nitawachukia sana wanasiasa kama kweli hili lina mkono wao.

Kwa aliyewahi kutazama tamthilia ya Queen Sendok ataweza kurejea pale Queen alivyofanikiwa kumdanganya mwerevu Misil. Ili Queen aweze kumdanganya Mwerevu Misil ilimpasa amdanganye Bidami ambaye ndiye aliyetumwa kwa Misil. Bidami alitumwa kumdanganya Misil kuwa jua litapatwa na mwezi, Bidami alikwenda kumdanganya Misil. Kwakuwa Misil alikuwa mwerevu aliweza kuugundua urongo wa Bidami. 

Mara baada Misil kugundua Bidami mrongo, alimfunga jela huku akitoa ahadi ya kumuua Bidami hadharani endapo hilo jua halitapatwa katika siku aliyosema litapatwa. Huku Bidami akijua fika kuwa alitumwa kudanganya alianza kukata tamaa kwa kujua kuwa adhabu ya kifo haikwepeki kwani alijua kuwa jua lisingepatwa na yeye alitumwa kudanganya tu. Bila kutegemea kwa Bidami na Misil kufika ile siku jua likapatwa kweli., kumbe Queen alimdanganya Bidami ili kupitia huyo apate kumchuza mwerevu Misil. Hapa kwetu CCM yataka kujitia werevu wa Queen Sendok? Yataka kuwachuza werevu kwa kufanya yote yale katika mkutano wa CHADEMA ili ubaya ibebe CHADEMA?. Kama ndivyo, lile tukio ni Bidami, CCM ni Queen Sendoke na werevu(wapiga kura) ni Misil. Je, tuko tayari kudanganywa kama Misil? Jibu hili pia liweke kapuni.

TATU: UDINI NA TUKIO LA ARUSHA.
Kuna watu wameshaanza kulihusisha tukio hili na mambo ya udini kisa tu mshukiwa wa kurusha bomu inasemekana alivaa bagharishia. Sioni sababu yoyote ya msingi kwa waislamu kuhisi wanasakamwa au kuandamwa. Muuaji hana dini, kabila wala utaifa. Mtu yoyote anaweza kuwa mhalifu ili mradi tu awe na dhamira mbaya ya uhalifu.

Kama mshukiwa alivaa kofia hiyo asisemwe kuwa kavaa kofia kisa kuwahofia waislamu? Au kama kavaa msalaba asisemwe kuwa kavaa msalaba kisa tu kuwahofia wakristo? Halafu, si kila mvaa kofia hiyo ni muislamu, hivi Mrema ni muislamu? Mimi nafikiri hata kama huyo akitajwa kuwa ni musilamu bado si tatizo hata kidogo, ndio sembuse kusema kuwa kavaa kofia? Lingekuwa tatizo endapo wapasha habari wangesema kuwa uislamu ndio umehusika. Nilishawahi kusema dini ponyo na udini ni sumu kwa taifa, mwenye kudhani kuwa mshukiwa katajwa kwasababu ya dini yake na si kwasababu ya kushukiwa kwake huyo mtu ni wa kuogopwa kama ukoma, lile tukio litatuvuruga kabisa endapo tukiruhusu japo kwa bahati mbaya dhana ya udini kutuongoza, kwa pamoja tuuchukie udini na tuupige vita.

NNE: MAADUI WA NJE NA TUKIO LA ARUSHA.
Nisema tu siasa hizi za kukamiana na kuchafuana zitatuingiza katika machafuko ambayo hatukuyatarajia hata kidogo. Ikumbukwe kuwa kulikuwa na tishio la M23, hili kundi huenda linataka nchi yetu iwe katika machafuko kama Kongo Kinshasa. Brigedia Nyekundu na Walinzi wa Kijani huenda wakaanza kuoneshea vidole wakati cha umbeya na mgombanishi yuko kando. Si hivyo tu, CHADEMA inaweza kujiingiza katika mgogoro na serikali hata pazuke machafuko zaidi kumbe kuna vikundi vya kishenzi toka nje vinatuvuruga kwa makusudi.
Lingine na la muhimu pia, nchi yetu sasa imeshathibitika kuwa ina kiwango kikubwa cha gesi ya asili, lakini pia kuna urenium ya kutosha. Jambo hili haliwezi kuwa habari njema kwa makampuni makubwa ya kibepari na nchi kubwa za kibepari. Utajiri wa Kongo Kinshasa unazinufaisha nchi za ulaya, hata yale makundi ya waasi yanafadhiliwa na serikali za kimagharibi huku serikali hizo ikipata madini na malighafi zingine kwa bei chee. Tanzania yangu niipendayo ndani yake kuna kila dalili ya uwepo wa nguruwe mwenye uchu na mihogo yetu. Nguruwe anataka kutugombanisha ili wapate madini haya kwa bei chee, tusikubali ya Kongo Kinshasa kutokea Tanzania. Kwanini mara baada ya gesi kugunduliwa ndio yatokee matukio ya urushwaji wa mabomu na vurugu za kuchinja? Swali hili naomba ulijibu leo, kwani linatujenga kama taifa na si swali la hawa wanafiki(wanasiasa).

Hivi ni rahisi kihivyo kuamini kuwa CCM na serikali imefikia hatua hiyo? Hakuna uwezekano wa kuamini kuwa kuna vikundi toka nje ya nchi yetu vinataka kutulazimisha tuamini kuwa CCM na serikali yetu imefikia hatua hiyo? Naam, hatua ya kuua wanachi wake ambayo kimsingi jukumu lake ni kuwalinda. Wanata tuamini hivyo, ili na sisi tuanzishe machafuko ya kama ya Libya? Kisha baadae waanze kuleta tambo za kuwapatia silaha watanzania watakaoasi? Hivi Marekani yeye ni nani hasa hata ajitie ujabali wa kugawa silaha kwa wale waliokuwa waasi wa Libya na sasa anataka kufanya hivyo Syria. Hivi zile silaha za nyuklia za Iraq zimeshaonekana? Hazijaoneka hadi sasa, tukisema kuwa ilikuwa ni mipango ya Marekani kumng'oa Sadam madarakani ili ipate mafuta kwa bei chee nitakosea? Je, na sisi tuko tayari kuzalisha waasi watakaotaraji msaada wa silaha toka magharibi?
Nukta yangu hii ya "NNE" haiondoi ukweli kuwa katika kutafuta "nguvu" na "ukwasi" binadamu yuko radhi kuinyofoa roho ya mwanadamu mwenzake kama roho hiyo itakuwa kikwazo au ni kafara muhimu katika kufanikisha ndoto zake za kupata "nguvu" au "ukwasi". Kwa hivyo yawezekana CCM kuhusika ili kuwatisha wapiga kura na kuichafua CHADEMA au, pia yawezekana CHADEMA kuhusika ili ipate kura za huruma na kuungwa mkono kisa tu wanaonewa.

HITIMISHO.
Mashuhuda wengi wanailaumu polisi kwa kufyatua risasi bila mpangilio na kusababisha mshukiwa kutoroka. Jambo hili la Polisi kushutumiwa si dogo na si la kubezwa hata kidogo. Sidhani kama ni sahihi kwa jeshi hili kuaminiwa katika uchunguzi wa tukio hili. Jeshi la Polisi lisipewe jukumu la kuchunguza hili suala, napendekeza rais na hii ni kutokana na kuwa dhamana ya usalama wetu iko chini ya mikono yake kikatiba aje namna ya kufanya uchunguzi huru pasina kulishirikisha jeshi hilo.


Watanzania tujiepushe na mihemko ya kidini katika kujadili mambo tata kama haya, tunaweza kudhani kuwa tunajenga kumbe ndio kwanza tunabomoa. Mkristo anaweza kuwa mshukiwa kama lilivyokuwa kwenye tukiwa la bomu la kwanza ambapo Ambrose ni mshukiwa na pia hata muislamu anaweza kuwa mshukiwa. Hakuna uhusiano kati ya dini ya mtu na uhalifu au kushukiwa kwa mtu husika.

Niviambie vyama vya CCM, CUF na CHADEMA kuwa "nguvu" ni mithiri ya mchanga wa pwani uliotulizana kiganjani, ni vema vyama hivi viufumbe huo mchanga kwa taratibu, kwa heshima na tahdhima zote. Jaribio lolote la kutumia mabavu kuufumba na kuumiliki mchanga huo litasababisha mchanga huo kuwatoka kiganjani na kupeperuka hovyo ardhini. Huko ardhi ukikutana na kiganja chenye ustaarabu basi huo mchanga utakifanya kiganja hicho ni rafikiye. 


Asanteni.


Njano5.

No comments:

Post a Comment