Friday, June 14, 2013

Mchawi wa kinachoitwa Umaskini wa Nchi yetu ni Nani?

WATAWALA na hasa Viongozi walio wengi, wamekuwa wakidai nchi yetu ni Maskini jambo ambalo wananchi na wadau wa mambo ya kiuchumi na Sheria wanapinga kwamba si maskini, ila kinachoelezwa ni Gia ya Watawala kujinufaisha na Railimali zilizopo huku wananchi wakidanganywa kupitia uelewa mdogo walionao.
Wachumi na Wanasheria wanaobahatika kuona na wakati mwingine kudadisi Uwazi wa Mikataba Feki ya Wawekezaji Uchwara na Usiri wake ambao hauwekwi wazi kwa wananchi wa Taifa hili kuhusu haki ya Rasilimali na uwekezaji, ndiko kunakowasababishia kupinga kuwa nchi si Maskini, ila kuna Ujanja ujanja unapita.
Wakati tunahangaika na kumtafuta Mchawi wa kinachosababisha Umaskini, ni lazima kwanza tuanagalia Watawala wanapima Uchawi na Umaskini wa Kiroho walionao kutanguliza Maslahi yao Binafsi hasa wanaposhirikiana na Wawekezaji Feki kulihujumu Taifa? Tukijua hilo tunaweza kutoa Malalamiko hata kwa Mungu.
lakini; kama Watawala hawawezi kubaini wakipandisha bei ya Mafuta wamefanya Uchawi wa Umaskini kwa wananchi wao kwa kuwa, kila kitu kitalazimika kupanda, na hivyo kuwatesa watu wake, kwa nini walalamike nchi ni maskini wakati wamesababisha wao?.
Iwapo Watawala hawaoni sababu ya kuwabana Wawekezaji wa Migodi na Mdini ili watozwe Kodi kama Ruzuku ya kuwapunguzia wananchi mzigo wa kupanda kwa bei za bidhaa na Huduma nyingine muhimu kwa raia wake, kwa nini wakurupuke kusema nchi ni maskini wakati wanaacha Rasilimali zichezewe na Wageni?
Kama mtu anaacha Wanyama na Mazao ya Pori yabebwe kama Mbwa kachukua Sufuria la Ubwabwa na wahusika wasichuliwe hatua kali ila kupenyeza nafasi za kulindana, kwa nini waibuke na Uongo wa kwamba nchi ya Tanzania ni Maskini? Tanzania si Maskini ni Tajiri sana! Washindwe na Walegee wanaosema Maskini!
Hakuna kitu kibaya kama Watawala wanapokosa Maadili ya Utawala Bora wakawa Bora watawala Mradi siku zinaenda bila kuwa na mpango endelevu wa kuwasaidia wananchi wao kuondokana na kugandamizwa na Uchumi Holela wa kigeni wenye bidhaa feki.
Thamani (Value) ya Watawala katika nchi ni kujali Kero, Adha, na Mateso ya watu. Lakini ikifika mahali wananchi wakidai haki yao inafichwa mifukoni kwa kulindwa na Maji ya Kuwasha, Mabomu ya Machozi na Virungu, wananchi hawawezi kujiletea maendeleo ila Mateso na Uchumi kudorola.
Kama Mikataba ya Wawekezaji mbalimbali inayoingiwa na Serikali ni Halali, kwa nini iwe ya Siri na Ifichwe? Kwa nini Mikataba hiyo iwe Bubu machoni pa Watanzania ambao huo ndio urithi wa Maendeleo yao? Kitendo hicho kinapoka umiliki wa Wananchi na kuwa Mtu mmoja au Kikundi binafasi.
Mchawi mwingine wa unaodaiwa Umaskini wetu, ni kila siku kuwa na Wazo kuongeza mapato kwenye Pombe, Sigara, Vinywaji Baridi na vitu kamavingine vya Starehe kama hivyo, kana kwamba ni Vipofu hatuoni, maeneo mengine kama Vitalu vya Uwajindaji wa Wanyama, Utalii, Uwekezaji Asasi na Asize.
Kama Watawala hawataona maeneo hayo na mengine yanayofanana na Hayo, wananchi wetu hawatatokea hata siku moja kuona ubora na uzuri wa Rasilimali waliyonayo, yakiwemo Madini, Gesi, Ardhi, Mito, Maziwa na Bahari.
Watawala wasirudierudie kusema Nchi ni Maskini wakati wao ndio Maskini wa kiroho wa kupanga na kutekeleza mbinu za kuipatia nchi Utajiri Lukuki ambao Mungu amelipatia Taifa kama zawadi  wasiwe Ombaomba, kama tunavyoitwa. Ukijiita maskini, huwezi kupandisha bei ya Mafuta maana ni sawa na kuumwagia Moto Maji, hakuna Chakula kitaiva.

na Bryceson Mathias

No comments:

Post a Comment