MSEMAJI Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Sheria na Katiba, Tundu Lissu, na Spika wa Bunge, Anna Makinda, jana walivutaka kikanuni baada ya mbunge huyo kukishambulia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akiwasilisha maoni ya kambi hiyo bungeni kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali ya mwaka 2013, Lissu alisema CCM kwa kutumia vifungu hivyo vya sheria, imejenga utamaduni mbaya wa kuwarubuni wapiga kura wake kufungua mashauri ya uchaguzi mahakamani dhidi ya wagombea wa vyama vya upinzani walioshinda katika uchaguzi.
Kauli hiyo ilimwinua Spika akimtaka Lissu asijadili masuala ya vyama kwa vile wanapochangia muswada wa sheria wanajikita kwenye maboresho.
“Lissu kanuni unazijua vizuri lakini unapoamua kwa makusudi kuzivunja unafanya kweli…hapa hatuweki siasa, sasa hiyo ya CCM imetoka wapi?” alihoji Spika.
Hata hivyo Lissu aliporuhusiwa kuendelea kuzungumza alimwambia Spika, “Najadili vifungu vya sheria zote mbili, nina ushahidi kwamba CCM inarubuni wapiga kura kwa kufanya matumizi mabaya ya vifungu hivi.”
Baada ya kuendelea kuitaja CCM kupitia kwa makatibu wakuu wake, Yusuf Makamba, na huyu wa sasa Abdulrahman Kinana, walivyoandika barua za kuwaelekeza wanachama wao wafungue kesi dhidi ya wapinzani, Makinda alizima kipaza sauti chake na hivyo akawa hasikiki.
Kwa takriban dakika nne Lissu aliendelea kusoma hotuba hiyo bila kutumia kipaza sauti, hatua iliyowafanya wabunge waanze kupige kelele wakidai hawamsikii huku Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, akisimama kuomba mwongozo bila mafanikio.
Baadaye Spika aliwasha kipaza sauti, hivyo Lissu aliendelea kusikika hadi mwisho akisema kuwa namna pekee ya kuwianisha vifungu hivyo ni kukopa masharti yote ya kifungu cha 115 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi na kuyaweka katika kifungu cha 114 cha Sheria ya Uchaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mapema akiwasilisha muswada huo, Jaji Werema alisema pamoja na jedwali la marekebisho unapendekeza kufanya marekebisho katika sheria tatu kwa lengo la kuondoa upungufu uliobainika wakati wa matumizi ya sheria hizo.
“Kuongeza masharti mapya katika sheria hizo na kufanya masahihisho ya kiuandishi na lugha ili kuondoa ukinzani wa tafsiri ya baadhi ya vifungu vya sheria hizo na kuleta utekelezaji madhubuti wa sheria husika,” alisema.
Sheria zilizolengwa na muswada huo ni Sheria ya Uchaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa (Sura ya 292. TL 2010) ambapo inapendekezwa kufanya marekebisho katika kifungu cha 114 kwa kuongeza kifungu kidogo kipya cha (4).
Kifungu hicho kitatoa mamlaka kwa mahakama zinazosikiliza kesi za uchaguzi wa madiwani kuendelea kusikiliza na kutoa hukumu katika mashauri ambayo hayakumalizika ndani ya kipindi cha miezi 18 kama zitaridhika kwamba kutomaliza kesi hizo kutawanyima haki wahusika katika kesi hizo au kuleta matumizi mabaya ya mamlaka ya mahakama.
Katika Sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria (Sura 171 T.L 2002) katika ibara ya 6 ya muswada yanapendekezwa marekebisho katika kifungu cha 5(1) ili kuweka ukomo wa makamishna wa tume kuwa tisa badala ya sita.
Kuhusu marekebisho yanayopendekezwa katika Sheria ya Utumishi wa Umma (Sura ya 298 T.L 2002), Jaji Werema alisema yanahusu kufuta maneno “Director of Local Government Authority na kuweka maneno “Local Government Authoriy kwenye kifungu cha 6(1).
“Kuongeza jukumu la watendaji wakuu wa taasisi za umma, yaani kila Katibu Mkuu, Katibu Tawala wa Mkoa na Halmashauri za Serikali za Mitaa kuwa kama inavyopendekezwa kwenye ibara ya 10 ya muswada yaani kusimamia na kuhakikisha ustawi wa taaluma kwa watumishi wa taasisi hizo,” alisema.
Pia kuweka kifungu kipya cha 29A kama inavyoonyeshwa kwenye ibara ya 13 ya jedwali la marekebisho.
Kwamba marekebisho haya yanalenga kumpatia katibu wa tume ridhaa ya kugatua mamlaka yake ya kusimamia mchakato wa ajira katika utumishi wa umma kwenda kwa mtendaji mkuu wa taasisi ya umma au halmashauri na kuweka masharti.
Wabunge waliochangia muswada huo, Pinda Chama (CCM), Lekule Laizer (CCM), Beatrice Shelukindo (CCM), Jenusta Mhagama (CCM), Mbarouk Rajabu (CUF) na Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) walisifu halmashauri kurejeshewa mamlaka ya kuajiri watendaji wa kada za chini wakisema itapunguza kero ya uhaba wa watumishi.
No comments:
Post a Comment