Tuesday, June 18, 2013

Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge Iwahoji Wakuu wa Usalama.

NI Muda Muafaka sasa, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge ichukue Jukumu lake iweze kuwaita na kuwahoji Wakuu wa Usalama wajieleze mbele ya Kamati kwa nini hali ya Usalama wa Raia na Mali zao nchini imefikia mahali pa kumwaga Damu za watu Ovyo Ovyo!.
 
Hii ni kutokana na Dosari kubwa inayoonekana dhahiri kuanzia Ngazi za Mkuu wa Jeshi hilo nchini (IGP), kushuka ngazi za wakuu wa Polisi wa Mikoa (RPCs), Wakuu wa Vituo (OCSs), Vituo vya Polisi Kata na wa kawaida yanapotokea Mauaji, hakuna uwajibikaji (accountability).
 
Mtaji wa Ushindi wa Jeshi lolote kwenye uwanja wa Medani, hujivunia wananchi wake kama lina na Mahusiano mazuri au mema na watu wake, wanaweza wakapigana vita zaidi ya Vyombo vya Usalama kwa kutoa taarifa za Uharifu mbalimbali ukadhibitiwa.
 
Kamati inatakiwa ihakikishe vyombo vya Usalama wa Raia na Mali zao vinafanya kazi karibu kabisa na wananchi katika kusimamia sheria, kuwalinda wao na mali zao, kuzuia uhalifu, ili kuwapunguzia hofu ya kufanyiwa vitendo vya kihalifu wajisikie huru.
 
Serikali kwa upande wake ihakikishe Jamii inaishi kwa kufuata sheria na taratibu za nchi na ikapambana na wahalifu ikishirikiana na wananchi na vyombo vingine vya Usalama kwa Ujumla wake! Nchi itakuwa katika Amani na watu wataishi kwa Aman hata nguo zitalala nje.
 
Licha ya kushamiri Utekaji, Kuuawa Mwandishi, Kiongozi wa Kidini, Kuumizwa kwa Kiongozi wa Madakitari, Viongozi wa Kisiasa na sasa Wananchi wanafanyiwa Ugaidi hadharani, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge ambayo ni sehemu ya Wawakilishi wake; Imekuwa Bubu.
 
Ububu huo wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge kutowaita na kuwahoji Wakuu wa Usalama na Wenyeviti wa Ulinzi na Usalama wa Wilaya na Mikoa nchini ili wajieleze kufuatia Vitendo vya Mauaji, Uharamia, na Dalili za Ugaidi zinazojiri machoni mwao!
 
Kamati pia ione Wakuu wa Usalama na Wenyeviti wa Mtaa, Kitongoji, Kijiji, Kata, Tarafa, Wilaya na Mikoa ni jambo moja, ila vitendo viovu vinapotokea mikononi mwao bila hatua za msingi kuchukuliwa, kwa kuhojiwa na kujieleza, ni budi kwao kuwajibika Utata unapojitokeza.
 
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge, Ivibane Vyombo vyake kuhusu utete wa Usalama hasa ndani ya nchi, kiasi kumekithiri umwagaji damu na vitendo viovu, ilihali wao bado wamekumbatia nyadhifa na dhamana za kazi wakiwa wameshindwa.
 
Kama Kamati ya Ulinzi na Usalama nayo kwa upande wake itakuwa imeshindwa kuwasemea watanzania ili kuondokana na mauaji ya kutisha yanayojiri sasa, basi si vibaya nayo ikawajibika kuanzia Kiongozi wake, jambo ambalo kwa ueledi hatuamini ishindwe!
 
Aidha ni jambo la aibu kwa Kamati, kuendelea kukaa kimya bila kuchukua hatua zozote dhidi ya watendaji, na kuishauri serikali yaani waajiri wake [wananchi] juu ya hatua ya kile kinachotishia maisha na mali zao, huku wakiachwa na ulevu wa makusudi ya watu fulani.
 
Ikumbukwe, tukiwa vitani Uganda; kufanikiwa kwa Shambulio la Fashist Idd Amini Kyaka;, Wakuu kadhaa wa Kijeshi (nawahifadhi Majina) waliwajibika!
 
Mbali ya kuonesha kufishwa kwa Demokrasia, wananchi wananyimwa haki za kujua Hatima ya Rasimali na Uchumi wao, kama una tija kwa maisha yao au unawasaidia wageni!

No comments:

Post a Comment