YUMKINI hali si shwari tena nchini, baada ya jana chaguzi mbalimbali za kuziba nafasi za udiwani kutawaliwa na matukio ya vurugu na umwagaji damu.
Katika maeneo mbalimbali zimeripotiwa vurugu hizo ambazo ziliwahusisha mashabiki na makada wa CCM na CHADEMA.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (CHADEMA), alishambuliwa na vijana wa CCM na kulazimika kulazwa katika hospitali ya Selian mkoani Arusha.
Nasari alijeruhiwa katika vurugu zilizotokea katika kituo cha kupigia kura cha Zaburi, Kata ya Makuyuni, Wilaya ya Monduli mkoani Arusha ambayo hadi tunakwenda mitamboni CCM ilikuwa ikiongoza.
Akizungumza kutoka eneo la tukio, Mratibu wa wanawake wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Sesilia Ndossi alisema majira ya saa tano asubuhi walikwenda kituoni hapo na walipofika walimkuta raia mmoja mwenye asili ya Kisomali.
Alisema raia huyo aliwaita watu na kuwaambia ‘pigia CCM’, kauli ambayo ilisababisha Nassari amuulize kwanini anapiga kampeni kituoni na baada ya swali hilo, mtu huyo na wenzake walimvamia na kumpiga.
Wakati hayo yakijiri Arusha, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Mirumbe, anayekaimu nafasi hiyo pia Wilaya ya Serengeti ametuhumiwa kuwateka vijana kadhaa wafuasi wa CHADEMA akitumia magari STK 8430, T 286 BFB, T 245 BFE, yanayomilikiwa na CCM pamoja na gari T 352 AHD, T 573 BEW akisaidiwa na askari magereza na kuwapeleka kwenye jengo moja la chama tawala.
Taarifa zaidi zinasema kuwa mkuu wa wilaya huyo alitaka kuwatumia polisi, lakini Mkuu wa
Bonyeza Read More Kuendelea
Polisi wa wilaya hiyo alimkatalia, hali iliyomlazimu kwenda kuwachukua askari magereza kwa ajili ya kutekeleza operesheni hiyo iliyodumu usiku kucha.
Chanzo kimoja kutoka polisi wilayani humo, kilisema mkuu huyo alifanya tukio hilo na alipoona amebanwa na viongozi wa CHADEMA aliamua kuwapeleka vijana hao polisi.
Mbeya
Katika Kata ya Iyela, gari la CCM lenye namba T 704 BEU, likiwa na watu wawili wanaotambulika kwa majina ya Moris na Nosy, waliwateka vijana wa CHADEMA ambapo mmoja wao Meshack Bernad alichomwa kisu.
Kata ya Mbalamaziwa Mufindi kaskazini
Watu sita ambao ni wafuasi wa CHADEMA walipigwa kwa marungu na visu na kuumizwa huku vitisho mbalimbali vikitolewa kwa wale wote walioonekana kuwaunga mkono CHADEMA.
Kata ya Minepa, Morogoro
Pikipiki ya CHADEMA imechomwa moto na vijana wa CCM (green guard) na Katibu wa chama wilaya ndugu, Lucas Daniel amepigwa na kuumizwa, huku mwenyekiti wa jimbo hilo, Kibam Ally Mohamedi akijeruhiwa na katibu mwenezi Severine Matanila kukatwa vidole
Kata ya Mianzini, Dar es Salaam
Tukio lililotokea huko ni kutekwa kwa wanachama na kiongozi wa CHADEMA ambapo alifungwa vitambaa vyeusi machoni, kisha kupigwa na kuumizwa vibaya.
Mmoja kati ya vijana waliotekwa ni Katibu wa Vijana CHADEMA, Tawi la Machinjioni anayeitwa Julius Vedastua.
Kata ya Genge, Tanga
Vijana wa CCM waliwakamata wafuasi na vijana wa CHADEMA na kuwapiga hali iliyowasababishia majeraha mbalimbali.
Sengerema
Mji wa Sengerema, mkoani Mwanza jana ulionekana kuwa uwanja wa vita, baada ya watu wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuwafyatulia risasi za moto viongozi na makada wa CHADEMA.
Tukio hilo lilitokea jana majira ya saa nne asubuhi, katika uwanja wa mpira wa Shule ya Msingi Sengerema wakati CCM na CHADEMA walipokutana kufuatilia hali ya mambo katika vituo vya kupigia kura kata ya Nyampulukano.
Katika tukio hilo, milio ya risasi zaidi ya nne ilisikika kutokea upande wa pili wa CCM, ambapo magari matatu yalilizunguka gari moja lililokuwa likitumiwa na baadhi ya viongozi wa CHADEMA Kanda ya Magharibi katika mizunguko yao.
Ndani ya gari hilo la CHADEMA, alikuwemo kiongozi wa Kikosi cha Movement for Change (M4C), Kanda ya Ziwa Magharibi, Alfonce Mawazo, Hussina Amri na makada kadhaa.
Baada ya gari la CHADEMA kuzingirwa na magari matatu ya CCM na baadaye risasi za moto kufyatuliwa hewani, wananchi waliokuwa maeneo hayo walilazimika kuingilia kati kwa kupambana na wafuasi hao wa chama tawala kwa kuwarushia mawe, na baadaye magari hayo yakatoweka kwa mwendo kasi kutoka eneo hilo.
Vurugu hizo za uchaguzi zilianza kutokea usiku wa kuamkia jana, ambapo inadaiwa wafuasi wa CHADEMA walitekwa na magari mawili yaliyokuwa na watu wanaodhaniwa kuwa wafuasi wa CCM, na kwamba yalikuwa yakiongozwa na gari moja linalodaiwa kuwa la Jeshi la Polisi wilayani hapa.
Tukio hilo linadaiwa kutokea majira ya saa tatu usiku, maeneo ya Ibondo kata hiyo ya Nyampulukano, ambapo ilielezwa kwamba wafuasi wa CHADEMA walikuwa wakifuatilia taarifa za kuwepo wafuasi wa CCM kupita mtaa kwa mtaa, nyumba kwa nyumba wakidaiwa kugawa rushwa ya fedha, chumvi na kanga.
Wakizungumzia matukio hayo ya utekaji, kiongozi wa M4C Kanda ya Magharibi, Mawazo na mbunge wa Nyamagana jijini Mwanza, Ezekiel Wenje walilaani kitendo cha CCM kutumia nguvu kwa lengo la kutaka ushindi.
Katika tukio la Kijiji cha Ibondo mfuasi mmoja wa CHADEMA aliyetajwa kwa jina la Renatus anadaiwa kuumizwa.
“Wakati tulipofika uwanja wa shule ya msingi Sengerema, ghafla yalikuja magari matatu ya wafuasi wa CCM kisha yakatuzunguka nyuma, mbele na ubavuni.
“Katika purukushani hizo wafuasi wa CCM walifyatua risasi zaidi ya nne hewani, na baada ya kuona hivyo wananchi waliokuwa maeneo hayo wakaanza kuwapiga mawe ndipo wafuasi hao wa CCM walipotimua mbio,” alisema Mawazo.
Alisema mbali na tukio hilo, mfuasi mmoja wa CHADEMA aliyemtaja kwa jina la Marco alitekwa akiwa kwenye harakati za kufuatilia makada wa CCM waliokuwa wakidaiwa kugawa hongo, na kwamba baada ya kutekwa aliingizwa kwenye gari la CCM na hajulikani alipo hadi sasa.
Naye Wenje alisema: “CCM wanafanya hivyo kwa kuelewa kabisa kwamba hawatashinda. Kwa hiyo wanalazimika kutumia nguvu kubwa kutafuta ushindi wa nguvu...wananchi walishawakataa hata wafanyeje hawatoki.”
Arusha
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeahirisha uchaguzi wa madiwani katika kata nne za Arusha hadi Juni 30.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali zilizotolewa jana zilimkariri Mwenyekiti wa NEC, Jaji Damian Lubuva kuwa tume yake inaruhusiwa kufanya hivyo pale inapoona wananchi hawatakuwa na amani kupiga kura.
Jaji Lubuva alisema kutokana na mlipuko wa bomu uliotokea juzi, uchaguzi wa jana haungeweza kufanyika katika mazingira mazuri.
No comments:
Post a Comment