Friday, June 7, 2013

CHADEMA yajipanga kuikosoa rasimu ya Katiba

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepanga kutoa tamko kuhusu rasimu ya mabadiliko ya Katiba iliyotangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba.
Akizungumza na Tanzania Daima jana Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri wa CHADEMA John Mrema alisema kwa sasa viongozi wa juu na watalaamu wanaisoma na kuichambua.
“Hatuwezi kutoa maoni ya juu juu kuhusu rasimu ya katiba… ni kitu nyeti ambacho kinatakiwa kufanyiwa kazi kwanza ili chama kitakapozungumzwa iwe kwa ajili ya manufaa ya Watanzania wote na si ya mtu mmoja ndiyo maana kazi hii tumeikabidhi kwa wataalam,” alisema Mrema.
Pamoja na mambo mengi wachambuzi hao watapitia mambo yaliyokubaliwa na yaliyoachwa ili kuionyesha tume hiyo kuwa kuna ambayo yana manufaa kwa taifa ingawa wameyaacha.
Katika rasimu hiyo mambo yaliyoachwa ni pamoja na serikali ya majimbo kwa sababu kuwa gharama za kuiendeshea zitaongezeka endapo serikali tatu zitakuwapo pamoja kuweza kufumuka mambo ya udini, malalamiko, dalili za kujitenga, ukabila na ukanda.
Mambo mengine yaliyokataliwa katika serikali ya muungano ni Mahakama ya Kadhi kwa maelezo kwamba nchi washirika zinaweza kulijadili.

No comments:

Post a Comment