Saturday, June 15, 2013

Chadema chaishutumu CCM kwa kudhoofisha upinzani

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimerusha shutuma CCM na kwa serikali kupitia Mwigulu Mchemba, kuwa kimekosa sera na matokeo yake kimeamua kutumia propaganda za mauaji ya raia ili kuufifisha upinzani.
Aidha Chadema kimesema Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Tanzania Bara), Mchemba, amekuwa akimtumia kijana aliyemwagiwa tindikali na CCM kuoombea kura.
Mchemba ambaye ni mbunge wa Iramba Magharibi pamoja na chama chake, walirushiwa tuhuma hizo jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Oganaizesheni na Mafunzo wa chama hicho,  Singo Benson alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
 
Benson alisema CCM kwa sasa kimekuwa kikipanga mauaji na kuusingizia upinzani kuwa ndio unaohusika.
 
Alisema CCM kupitia Mchemba na wakubwa na wadogo wake kazini ( bila kuwataja), wamekuwa wakipita huku na huko katika kampeni za udiwani wakijianika walivyo mufisili wa hoja.
 
“Kutoka kampeni hizi zianze anatembea na kijana Musa kuombea kura na kusema alimwagiwa tindikali na Chadema katika uchaguzi mdogo wa Igunga,Tabora, ” alisema na kuongeza:
 
“Igunga nilikuwepo Musa alikuwa miongoni mwa vijana zaidi ya 600 waliowekwa kwenye makambi ya Ulemo Singida, Nzega na Uyui wakifundishwa mbinu za kijeshi kushughulikia wapinzani,” alisema.
 
Benson alisema waliwahi kuonyesha ushahidi ambao CCM hawawezi kuupinga wala kuukanusha kuhusu ukatili wa kumwagiwa tindikali kijana huyo kuwa ulikuwa sehemu ya utekelezaji wa mbinu walizopewa vijana wao wa ‘green guards’.
 
Alisema upo ushahidi wa kutosha kuwa vijana hao wa CCM chini ya ushirika wa baadhi ya watumishi wa vyombo vya dola, walipewa mafunzo ya kuua, kutumia silaha, tindikali na  asidi.
 
Pia alisema mafunzo mengine waliyopewa ni kuteka kuumiza na kuua kwa kutumia sindano ya sumu au kusambaza virusi vinavyosababisha upungufu wa kinga mwilini.
 
“Mchemba kama anaushahidi Chadema kilihusika kwenye tukio hili la tindikali autoe hadharani na sio kudanganya tumeua watu nane kwenye mikutano yetu ya Igunga, Morogoro, Iringa na Ngago, Singida,” alisema.  
 
Benson alisema Mchemba alienda Mbeya na kutaka vijana 500 wawekwe kwenye kambi ya shule moja ya sekondani kata ya Mwakibete ambapo viongozi wa Chadema waliposikia waliwasiliana na Kamanda wa Polisi mkoani humo Diwani Athuman, na kujibiwa kuwa wanajifunza ukakamavu.
 
Pia alisema usiku wa kuamkia jana watu watano waliokuwa kwenye gari lenye namba za usajili T 820 BJA mali ya CCM mkoa wa Lindi, wamemteka, kumpiga virungu na kumvunja pua Katibu Mwenezi Chadema Andrea Mlaponi.
 
“Katika tukio hilo Dismas Lucas ambaye alikuwa miongoni mwa wale waliokuwepo kwenye gari hilo alikamatwa na viongozi wetu, Chadema wakati ikitoa taarifa za tukio kwa OCD, gari la CCM lilifika hapo na baada ya kuwaona watu wetu liligeuza na kukimbia,” alisema.
 
Pia alikumbushia matukio mbalimbali likiwemo la Arusha ambalo watu walikatwa mashoka, Arumeru mwenyekiti wa kata ya USA River ambaye alitumiwa ujumbe mfupi wa vitisho na Mchemba na baadaye kuchinjwa.
 
Matukio mengine kuuwawa kwa muuza magazeti Morogoro wakati wa mikutano ya chama na tukio la kuuwawa kwa mwandishi Daud Mwangosi, Iringa.
 
“Mwigulu anaishi kwa ajili ya leo, anatafuta cheo.. na CCM inakumbatia watu wajinga imempandisha cheo kama ilivyofanya kwa RPC Iringa ambaye ndiye aliyemwamuru yule askari amuue Mwangosi,” alisema.
 
Pia alikumbushia tukio la Dk. Steven Ulimboka kuwa baada ya kurejea nchini kutoka Afrika ya Kusini kwa matibabu, alisema anamjua aliyemfanyia kitendo hicho lakini polisi (Kova) hakuenda kuchukua ushahidi.
mwisho

No comments:

Post a Comment