Sunday, May 5, 2013

Zitto: Kashfa za Meremeta zisijirudie JWTZ


MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA), amekemea vikali baadhi ya kashfa za Meremeta na Suma JKT ambazo zimekuwa zikilikumba Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuchafua sifa ya jeshi hilo.
Zitto alitoa kauli hiyo jana bungeni mjini hapa alipokuwa akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2013/2914 iliyowasilishwa na Waziri Shamshi Vuai Nahodha.
Pia alilitaka jeshi hilo kuwajali askari wake kwa kuwalipa vizuri mshahara na mafao yao ili wawatumikie wananchi wao kwa ufanisi, waondokane na tamaa ya kuweza kurubuniwa na waasi ambao wanaweza kujitokeza kutoka nchi jirani.
“Kashfa hizo zinazoiandama JWTZ hazina budi kutatuliwa ili kuepuka yanayotokea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambapo baadhi ya wanajeshi wameasi,” alisema.
Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, alimtaka Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, kuhakikisha kashfa kama zile za Meremeta na Shirika la Uchumi la JKT (Suma) kuhusu matrekta hazijirudii.
”Ndugu yangu Mwamunyange natumaini unanisikiliza hapa, naomba tu katika uongozi wako jeshi letu liwe safi kuliko kitu chochote na makosa yaliyokuwa yakitokea siku za nyuma yasijirudie tena," alisisitiza.
Sambamba na hilo, Zitto alisisitiza kutorudiwa kwa  makosa yaliyotokea mwaka 1994 ya serikali kusitisha mafunzo ya JKT, hatua iliyosababisha kutokuwepo na maadili kwa baadhi ya askari wanaojiunga na jeshi kwa vile hawajapitia mafunzo hayo.
“Napendekeza mafunzo ya JKT yawe kwa watumishi wote bila kujali vyeo au umri kwani wabunge  mbalimbali akiwemo mimi na wengine tuliacha viti vyetu na kwenda kujiunga na mafunzo hayo ili kupeleka ujumbe kwa vijana kuwa hayachagui mtu,” alisema.
Pia aliitaka serikali kuboresha mafunzo hayo kwa kuwaandaa vijana kuwa wataalamu wa ufundi mbalimbali ukiwamo useremala na umeme badala ya kuishia kujifunza kupiga kwata.
Alisema wanaomaliza lazima watoke na stadi za maisha na jeshi lishirikiane na vyombo vya elimu kama Mamlaka ya Elimu ya Mafunzo Stadi (Veta) ili kuweza kupata vijana wakiwa wataalamu wa ufundi wawapo jeshini.

No comments:

Post a Comment