KATIKA Milo na Ustawi wa Mtu, zipo aina tatu za kutosheka, Kushiba, Kuvimbiwa na Kukinai. Na ndani ya Kutosheka, kuna Kulewa Shibe, Kuvimbiwa na Kukinai, ambako kwa Ujumla wake unaoitwa Uharibifu.
Kwa Mila na Desturi au Utamaduni, ukila chakula ukashiba, si vema kumwaga maana wapo wahitaji ambao unachomwaga wangeweza kula. Lakini pia si vizuri ukazidisha kula kwa uroho hadi ukavimbiwa ukadhurika, na si busara mtu ukajishindilia chakula hadi akakinai, ni tamaa na ipo adhari yake kwa jamii.
Viongozi walio wengi walioko madarakani ikiwemo nchi yetu, wanaona Uongozi ni Ukoo wao badala kufahamu kuwa hiyo ni dhamana waliyopewa na wananchi, na kwa dhamana hiyo wanaweza kuwaondoa. Baadhi wamekuwa wakishiba, lakini wengine wanavimbiwa na kulewa na hawataki kukinai.
Viongozi wa namna hii, wana mawazo mgando, wanadhani hakuna wengine wenye uwezo wa kuongoza, na sana sana wakikubali kuongozwa, basi watataka watoto wao ndio wawe warithi wa madaraka yao, wakidani huo ni urithi wa ukoo wao, kama ilivyo mtu akifa katika familia au waganga wanavyorithishana mikoba ya uchawi.
Biblia Takatifu Mithali 30:14 inasema, “Kuna kizazi cha watu ambao meno yao ni panga; Na vigego vyao ni kama visu. Ili kuwala maskini waondolewe katika nchi, Na wahitaji katika wanadamu” Hivyo wapo viongozi wangependa waendelee kutawala hata kama watu wote wangekufa, mradi wao.waongoze.
Huku ni kushiba madaraka kulikopitiliza, ambako kunajali wenye nacho tuu lakini wasionacho yaani walalahoi, hawathaminiwi, labda kama umekubali na kuridhia uwe Mtuwa wa Familia zao na kibarua wa kuwatekelezea na kulinda Maslahi yao.
Watu wa namna hii, hawatofautiani na msbinti wa Mruba, ambao hata akishiba anaendelea kula, akivimbiwa na kudhurika anaendelea kula, na hata akikinai bado huwa anaendelea kula, na hao huwa hawaachii hadi walewe Madaraka, kama ndege mmoja ambaye hulewa ulanzi hadi afie kwenye mti wake.
Nanukuu; “Mruba anao binti wawili, Waliao, Nipe! Nipe! Kuna vitu vitatu visivyoshiba kamwe, Naam, vinne visivyosema, Basi! Kuzimu; na Tumbo lisilozaa; Nchiisiyoshiba maji; na Moto usiosema, Basi! Inasema Biblia Mithali 30:15-16.
Kwa ukweli wa Mungu kupitia kwa Mihali, nchini tunao baadhi ya Viongozi wasiosema Basi! ni kama Kuzimu kusikosema basi, kunapokea tu wafu; Tumbo ambalo huwa halisemi basi au yatosha, na ni Nchi isiyoshiba Maji, na Moto usiotosheka kuchoma au kuunguza,
Viongozi wa namna hii, ni wale ambao Mkurugenzi au Kiongozi akifuja Rasilimali za Umma, anakumbatiwa, na hata akitoboa Mbereko anahamishiwa mahali pengine, Taifa likitenga fedha kulipia madeni ya wazabuni, hata Mkaguzi Mkuu )CAG) akikagua na kusema hazijalipwa, wao hung’angania zimelipwa.
Watu wa namna hiyo, wakifika bungeni; badala ya kutetea hoja za wananchi wanaoteseka na hali ngumu ya maisha, wao wanaouliza Magwanda ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) yamekujaje, lakini hawaulizi Nguo za Kijana tulizipataje na kwa nini tunazivaa na haziulizwi.
Ni rai yangu viongozi waelewe, Watanzania sasa wamepevuka, Wanasoma Magazeti, Wanasikiliza vyombo vya Habari, wanatazama Bunge, na kuona kila Baya na Zuri linalofanywa na waliowapa Dhamana wanavyochezea Muda, Kulala Usingizi, kutoa Matusi na mabishano yasiyo na tija.
Nawashauri Watawala, watakapofanya maamuzi Magumu 2015, msianze kujikomba kwa kuwanunulia Pombe, Ubwabwa, Kanga na kuchelewesha Matokeo, majibu yanapojulikana.
Imeandikwa na Bryceson Mathias
No comments:
Post a Comment