WAZIRI wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta, juzi alimuokoa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, dhidi ya makombora ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA).
Busara za Sitta ndizo zilizomfanya Lissu abadilishe nia yake ya kuondoa shilingi kwenye bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani.
Hatua hiyo ilikuja wakati Bunge limekaa kama kamati kupitia vifungu vya wizara hiyo, ambapo Lissu alitaka Waziri Nchimbi afafanue serikali imetekelezaje mapendekezo ya tume yake iliyoongowa na Jaji Ihema pamoja na ile ya Haki za Binadamu zilizoshauri Jeshi la Polisi kusukwa upya ili lifanye kazi bila kufuata matakwa ya wanasiasa wa chama tawala.
Lissu alitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa kikao hicho, Anne Makinda, kuwa anakusudia kuondoa shilingi kwenye mshahara wa Waziri Nchimbi endapo majibu yake yataendelea kuwa mafupi na mepesi.
Hata hivyo, kama alivyokuwa amejibu mapema wakati akihitimisha hoja za wabunge, Nchimbi alisema ni kweli kwamba Jeshi la Polisi halipaswi kufanya kazi kwa maelekezo ya wanasiasa na kwamba ndiyo sababu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, anaendelea kuwa kazini.
Nchimbi aliongeza kuwa ripoti hizo wamezisoma lakini wanajipa muda kuzifanyia kazi, kwani endapo watakurupuka pasipo kuangalia mazingira mwisho wake unaweza kuwa mbaya.
“Unajua ukikutana na mtu aliyetoka kuombwa rushwa na trafiki halafu ukamuulizia utendaji wa jeshi hilo, atakwambia hakuna watu wabaya kama hao. Lakini ukikutana na dereva aliyepata ajali akakatika mguu halafu akaokolewa na trafiki, ukimuuliza kuhusu utendaji wa jeshi hili, atasema hakuna watu wazuri kama hao,” alisema.
Hivyo, Dk. Nchimbi alisema ripoti hizo hawawezi kuzifanyia kazi moja kwa moja bali wanapima kuona wakati zinafanyiwa kazi wajumbe waliegemea kwenye nini.
Majibu hayo yalimwinua tena Lissu na kutoa hoja ya kuondoa shilingi akisema Waziri Nchimbi ametoa maelezo ya mzaha wakati tume aliyoiunda yeye na ile ya Haki za Binadamu iliyoundwa na rais ni kwanini wameshindwa kuzifanyia kazi.
Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge wengi wa upinzani ambao walianza kuichangia wakidai jeshi hilo linafanya kazi kwa maelekezo ya wanasiasa, hata kufikia hatua ya kushindwa kuwachukulia hatua vigogo wa CCM kwa amri za wakuu wa mikoa na wilaya.
Kabla ya Waziri Nchimbi kujibu hoja hizo, Makinda alimuita Waziri Sitta ambaye alikuwa akikaimu nafasi ya waziri mkuu ili aweze kutoa maelezo kuhusu sakata hilo.
Sitta alisema wanasiasa wanapaswa kuwatendea haki wananchi, akifafanua kuwa: “Hapa kuna tuhuma nzito dhidi ya Jeshi la Polisi, kuna tuhuma nzito dhidi ya serikali ya CCM na zinatolewa na wenzetu wabunge tunaowaheshimu kutoka upande wa upinzani.
“Nataka kushauri mheshimiwa mwenyekiti, kanuni ya 103 si mahala pake kuzungumza jambo zito namna hii, kwa sababu inahitaji hoja ikae vizuri, iwe na ushahidi, majibu yawepo.”
“Sasa wakati wa kuondoa shilingi tuzungumze suala la polisi kutumiwa na wanasiasa, na pande zote ziweze kupeana taarifa kulingana na mujibu na pengine upande wa serikali wana jambo la kusema, maana tunakerwa na kauli za viongozi wa vyama vingine wanaotoa eti saa 24 fulani aondoke,” alisema.
Alisema kuwa kuna wanasiasa wanataka kuonesha serikali haifai, ni goigoi, kwamba hakuna serikali inayoendeshwa hivyo.
“Sasa haya ukiyachanganya ni furushi kubwa kwa wananchi wetu, ningemshauri Mheshimiwa Lissu atumie kanuni nadhani ya 53, apewe nafasi kwenye mkutano ujao alete hoja binafsi kwa mujibu wa kanuni, tuwe na muda wa kuijadili vizuri na tutoe majibu yanayostahili,” alisema Sitta.
Hoja hiyo ilikubaliwa na Lissu akisema kuwa Sitta ametoa majibu yanayoeleweka, ambayo si ya kuokoteza kama ya Dk. Nchimbi, maelezo ambayo baadaye yaliruhusu kikao kuendelea na kupitisha vifungu na hatimaye kuipitisha bajeti ya wizara hiyo.
No comments:
Post a Comment