Saturday, May 18, 2013

Mnyika:Sera ya mafuta na gesi iandaliwe kwanza

Serikali imeshauriwa kuandaa  sera ya mafuta na gesi kabla ya kuandaa  sera ya sekta ndogo ya gesi ili kuilinda rasilimali hiyo iweze kuwanufaisha Watanzania.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, alieleza kuwa  taifa kuwa na sera ya gesi asilia kabla ya kuwa na ile  sekta kubwa ya mafuta na gesi ni sawa na kuweka mkokoteni mbele ya punda na kutegemea punda huyo atauvuta.

“…mchakato wa upatikanaji wa sera hiyo uwe shirikishi zaidi ya ulivyo sasa, wananchi wahusishwe kama wadau muhimu, lakini zaidi wakazi wanaozunguka maeneo ya rasilimali hiyo inapochimbwa wapewe kipaumbele,” alieleza Mnyika. 

Mnyika ambaye ni mbunge wa Ubungo (Chadema) aliitaka serikali kusogeza mbele mzunguko wa nne wa utoaji wa leseni za utafiti na ugunduzi wa gesi asili mpaka ikamilishe mchakato wa maandalizi ya sera na sheria ya gesi asilia .

Pia aliishauri kuhakikisha kuwa  ufumbuzi unapatikana katika migogoro na matatizo yanayoendelea kuhusu gesi asilia huko Mtwara na maeneo mengine  na kutaka  mchakato wa katiba mpya uweka msingi thabiti wa utafutaji, uvunaji na uendelezaji wa rasilimali nchini.

Alitaka pia iweke   hadharani ripoti ya uchunguzi inayodaiwa kufanywa siri ambayo imebainisha ubovu wa mikataba iliyopo sasa ili hatua ziweze kuchukuliwa.

“Usiri huo wenye mwelekeo wa kuficha ufisadi unaoendelea katika sekta ya gesi asilia unaendelea hata baada ya kuiandikia serikali barua nikitumia Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge kuomba kuona nakala za ripoti na mikataba ukiwamo wa ujenzi wa bomba la gesi kuanzia mwanzoni mwa 2013, hata hivyo mpaka sasa sijapewa majibu,” alilalamika Mnyika.

Hivi karibuni Wizara ya Nishati na Madini kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli  Tanzania (TPDC) imetoa taarifa ya kuzinduliwa kwa mzunguko wa nne  wa utoaji leseni wa utafiti na ugunduzi wa gesi asilia nchini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, leseni zitakazotolewa  zitahusisha utafiti katika ziwa Tanganyika  na ndani ya kina kirefu cha maji ya bahari ya hindi.

No comments:

Post a Comment