1.0. UTANGULIZI
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Sura ya 83 (kifungu cha 18
(3)) imetoa wajibu kwa tume wa kuunda Mabaraza ya Katiba kwa ajili ya kupitia
na kutoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume.
Kifungu cha 17 (8) kinaeleza kuwa, isipokuwa kama mazingira
yatahitaji vinginevyo, Tume itabuni utaratibu unaofanana ambao utatumika kila
upande wa Muungano.
Kifungu cha 18 (6) kinaeleza aina nyingine ya Mabaraza ya
Katiba kwa kueleza kuwa Tume inaweza kuruhusu Asasi, Taasisi au Makundi ya Watu
kuwasilisha maoni yao kuhusu Rasimu ya Katiba.
Ikumbukwe
kwamba Kamati Maalum ya CHADEMA ilikutana
na Tume ya Mabadiliko ya Katiba tarehe 7 Januari 2013 kuwasilisha maoni ya
CHADEMA kuhusu katiba mpya kama ilivyoalikwa lakini pia kutumia fursa hiyo
kuwasilisha mapendekezo ya CHADEMA kuhusu marekebisho na maboresho
yanayohitajika kuhusu mchakato wa mabadiliko ya katiba ili kupata katiba bora.
Tarehe 31 Januari 2013 Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilitoa
taarifa kwamba imeamua kuwa Mabaraza ya Katiba yatakuwa katika makundi mawili
yafuatayo: Mabaraza ambayo Tume itayasimamia na kukusanya Maoni (Mabaraza ya Katiba ya Wilaya – Ngazi ya
Mamlaka ya Serikali za Mitaa) na Mabaraza ambayo Tume haitayasimamia.
Mabaraza hayo yatajisimamia yenyewe na kukusanya maoni yatakayowasilishwa
kwenye Tume kwa mujibu wa maelekezo. (Mabaraza
ya Katiba ya Asasi, Taasisi na Makundi ya Watu).
CHADEMA
baada ya kupitia muongozo huo na kwa kuzingatia kuwa tayari tume ilishafanya
uamuzi kuwa mabaraza ya katiba yatakuwa ya wilaya, tarehe 14 Februari 2013
kiliwasilisha maoni na mapendekezo yake kuhusu uteuzi wa wajumbe ambayo kwa sehemu kubwa hayakuzingatiwa na
Tume ya Mabadiliko ya Katiba na hivyo kusababisha matatizo makubwa katika
mchakato mzima wa uteuzi wa mabaraza ya katiba ya wilaya.
Kufuatia
hali hiyo katika Maoni ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu
hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu, tulitangaza kwamba CHADEMA itajitoa ushiriki wake
katika mchakato wa Katiba Mpya endapo mambo yafuatayo hayatapatiwa ufumbuzi
hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2013:
“Mosi; Kufutwa kwa uchaguzi wa
wajumbe wa mabaraza ya wilaya ya Katiba uliofanywa na Kamati za Maendeleo za
Kata, na badala yake wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya wachaguliwe moja
kwa moja na wananchi wa Kata husika bila kuchujwa na WDC;
Pili: Serikali ilete mbele ya Bunge
hili tukufu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
yatayofanyia maeneo yafuatayo marekebisho.”
Bonyeza Read More Kuendelea
Bonyeza Read More Kuendelea
2.0
MAONI NA MAPENDEKEZO KUHUSU MWONGOZO WA MABARAZA YA ASASI, TAASISI NA MAKUNDI
YENYE MALENGO YANAYOFANANA:
Bila kujali upungufu uliokuwepo
katika uteuzi wa mabaraza ya katiba ya wilaya, Tume ya Mabadiliko ya Katiba
imetoa rasimu ya Mwongozo kuhusu Mabaraza ya Katiba ya Asasi, Taasisi na
Makundi yenye malengo yanayofanana; hivyo, CHADEMA kinatoa maoni kuhusu rasimu
hiyo kama ifuatavyo:
- Uendeshaji
(2.2) ; makundi yaliyotajwa ni yale
yanayoanzia chini mpaka taifa na taifa: wakati ambapo kuna makundi ya ngazi
ya chini pekee mathalani taasisi za jumuiya (CBOs), au taasisi
iliyosajiliwa kwenye ngazi ya wilaya au hata mitandao ambayo
haijasajiliwa, hivyo wigo upanuliwe kuruhusu makundi yote.
- Utaratibu
wa kutambua makundi (3.0); kipengele
cha kutaka kuwasilishwe ‘taarifa ya kusudio’ kiondolewe, kinaongeza urasimu hasa kwa
kuzingatia kwamba taarifa hizo zinawasilishwa tume makao makuu. Tume
ikishatoa muongozo maana yake ni kwamba tayari imefungua mlango kwa
makundi kujadili rasimu, hivyo ngazi pekee itayobaki iwe ni 4.0 ya
kuwasilisha maoni. Hatua hii itachelewesha makundi ya kijamii kutumia haki
na uhuru wako wa kikatiba wa kujumuika na kuwasilisha maoni.
- Utaratibu
wa kuwasilisha (4.0), maneno “Tarehe
zitazoelekezwa na tume ya mabadiliko ya katiba” katika sentensi ya kwanza,
kwa sababu inaweza kuleta tafsiri ya kwamba tume itayapangia tarehe za
kukutana mabaraza hayo ya makundi ya kijamii ambayo kimsingi ni
kuyaingilia. Tume ipange tu tarehe ya mwanzo wa kupokea maoni na mwisho wa
kupokea maoni kwa awamu ya mabaraza. Tarehe ya kuanza uendeshaji
imeshatajwa kwenye 2.2 “wakati wowote kuanzia tarehe itayotangazwa na
tume”, tarehe ya mwisho wa kuwasilisha maoni imewekewa utaratibu kwenye
4.0 “ maoni yatawasilishwa kwa tarehe zitazoelekezwa na Tume”; hivyo
sentensi hiyo ya kwanza haina haja ya kuwepo.
- Uzito wa
maoni (6.0), maelezo ya kwamba
‘maoni yatakuwa na uzito ulio sawa’, yanapaswa kufafanuliwa; kwa mantiki
ya sentensi hii ni kwamba makundi yenye malengo yanayofanana hata yawe
mengi kiasi gani yatakuwa na uzito sawa na mabaraza yatayosimamiwa na tume
ambayo tayari yameshalalamikiwa kwamba yana hodhi ya chama kimoja na
hayana uwakilishi wa moja kwa moja wa wananchi. Hivyo, tafsiri itolewe
ambayo itahakikisha kwamba maoni ya wengi na matakwa ya umma yatatamalaki.
- Tume
kualikwa kusikiliza; Pamoja na kwa
mujibu wa kipengele 2.2 mabaraza ya makundi yenye malengo yanayofanana
‘yatajisimamia na kujiendesha yenyewe’, pawepo na kipengele kwamba iwapo
asasi, taasisi au kundi husika linaweza kuomba tume itume maafisa wake
kuangalia/kusikiliza moja kwa moja ziada/zaidi ya utaratibu uliotajwa
kwenye 4.0
3.0 MAONI NA MAPENDEKEZO JUU YA MASUALA MENGINE
KUHUSU UENDESHAJI WA MABARAZA NA UTOAJI MAONI JUU YA RASIMU:
Aidha,
pamoja na maoni kuhusu muongozo; CHADEMA kinatoa maoni ya ziada kwa Tume
kuzingatia yafuatayo:
- Muongozo
wa kwanza uliotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba ulihusu “Muundo, utaratibu wa kuwapata wajumbe wa
mabaraza ya katiba ya wilaya (Mamlaka za Serikali za Mitaa) na uendeshaji
wake”. Hata hivyo, muongozo uliotolewa ulijikita katika muundo wa mabaraza
na mchakato wa uteuzi wa wajumbe wa mabaraza hayo, lakini haujatoa maelezo
na maelekezo ya kutosha kuhusu namna mikutano ya mabaraza ya katiba ya
wilaya itavyoendeshwa na utaratibu mzima utakaotumika kujadili rasimu ya
katiba mpya katika mabaraza hayo. Aidha, CHADEMA kinapendekeza kwa mara
nyingine kwamba tume itoe muongozo mwingine mahususi kuhusu uendeshaji wa
mabaraza ya katiba ikiwemo utaratibu utakaotumika wakati wa kujadili
rasimu katika mabaraza; aidha kabla ya muongozo huo kuanza kutumika
wananchi wapewe nafasi ya kutoa maoni na mapendekezo kama ilivyokuwa kwa
muongozo huu kuhusu uteuzi wa wajumbe.
- Kwa
kuwa mpaka awamu ya nne ya ukusanyaji maoni ya wananchi binafsi
ilipokamilika wananchi waliotoa maoni kwa njia ya simu walikuwa 16,261 tu
kati ya idadi ya wateja wa makampuni ya simu za mkononi ambao watajwa kuwa
zaidi ya milioni 20 (mobile phone subscribers); Tume ya Mabadiliko ya
Katiba iweke mfumo wa wananchi binafsi kuweza kutoa maoni kuhusu rasimu ya
katiba kupitia simu za mkononi. CHADEMA kinarudia kutoa mwito kwa tume kushirikiana na makampuni ya simu
kuwezesha ujumbe wa simu ya mkononi kutumwa kwenye kila mtanzania mwenye
simu kumpa dondoo juu ya rasimu ya katiba na kumpa namba anazoweza kutuma
maoni kwa njia ya simu na pia maelekezo ya namna ya kutuma ujumbe wa bure
wa maoni yake. Hii itafanya wananchi wengi kuweza kushiriki kutoa maoni.
Aidha, pawepo na uwazi katika mfumo mzima wa maoni yanayokusanywa kwa njia
ya simu na mitandao mingine ili kusiwe na uwezekano wa ‘kuchakachua’.
4.0 HITIMISHO:
Pamoja
na kuwasilisha maoni na mapendekezo haya izingatiwe kuwa madai ya Kambi ya
Upinzani inayoongozwa na CHADEMA kuhusu kufutwa kwa chaguzi za mabaraza na
kuwasilishwa bungeni kwa muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria ya
mabadiliko ya katiba katika mkutano wa kumi na moja wa Bunge unaoendelea
hayajatimizwa.
Waziri
Mkuu aliahidi (wakati wa kuhitimisha hoja ya Ofisi ya Waziri ) kwamba Serikali
italeta Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kabla ya
mwisho wa Mkutano huu wa Bajeti.
CHADEMA
kinasubiri ahadi hiyo kutekelezwa katika kipindi hiki ambacho kitaenda sambamba
na Tume kutoa Rasimu ya Kwanza ya Katiba Mpya kwa ajili ya kuanza kujadiliwa na
Watanzania.
Endapo
hadi kufikia mwisho wa kipindi hicho Serikali itakuwa haijaleta Muswada wa
marekebisho yanayotakiwa; au endapo Muswada utakaoletwa hautakidhi matakwa ya
kuboresha mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya; basi CHADEMA itawaalika
wanachama, wafuasi na mashabiki wake Tanzania nzima, pamoja na taasisi za
kiraia na za kidini, vyama vya siasa na Watanzania wote wenye nia njema na
taifa hili kuhamasisha umma kuikataa Rasimu ya Katiba Mpya kwenye kura ya maoni
itakayofanyika kwa ajili ya kuihalalisha Katiba hiyo mbovu.
Naomba
kuwasilisha,
John
Mnyika (Mb)
Kny.
Katibu Mkuu
19/05/2012
No comments:
Post a Comment