Sunday, May 12, 2013

Makombora ya Lissu yalivyomtoa jasho Nchimbi


MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Chiku Abwao (CHADEMA), aliianza wiki hii kwa kumlipua Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, akidai ndiye analiharibu Jeshi la Polisi nchini na kulitumia kufanya kazi za kisiasa.
Abwao ambaye alikuwa akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani iliyowasilishwa bungeni na Waziri mwenye dhamana, Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema kuwa Lukuvi anatumia jeshi hilo kubambika watu kesi jimboni kwake Isimani.
Alisema kuwa Lukuvi amekuwa kero kubwa jimboni kwake Isimani kwa kulitumia Jeshi la Polisi kutisha wapinzani wake kisiasa kwa kuwa wanamuunga mkono mwana mama huyo.
“Tatizo la Lukuvi ni baada ya mimi kutangaza kugombea ubunge katika Jimbo lake la Isimani. Amekuwa akinitukana kwenye mikutano na kwenye redio kuwa mimi naweza kufanya biashara ya kufungua baa tu,” alisema.
Lukuvi naye alijibu mapigo akisema Abwao anafanya siasa za kuganga njaa na kwamba kwa miaka kumi aliyokuwa bungeni kila mtu anajua hilo.
“Iringa ina wabunge wengi ila kila mmoja ana uwezo wake, hivyo tukiongea hapa wananchi wanajua, hivyo nawaomba Wana Isimani msiwe na hofu,” alisema.
Lukuvi alimtambia pia Abwao akisema kuwa Isimani ameikuta na ataiacha, kwani wenyewe wapo na kwamba itaendelea kubaki mikononi mwa CCM.
Sitta amwokoa Nchimbi
Siku iliyofuata wakati wa kuhitimisha hoja hiyo, Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta, alilazimika kuingilia kati kumnusuru Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, kutokana na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), kumchachafya waziri huyo.
Hatua hiyo ilikuwa wakati Bunge limekaa kama kamati kupitia vifungu vya wizara hiyo, ambapo Lissu alitaka Waziri Nchimbi afafanue serikali kupitia wizara yake imetekelezaje mapendekezo ya kamati yake iliyoongozwa na Jaji Ihema pamoja na ile ya Haki za Binadamu na Utawala Bora zilizoshauri Jeshi la Polisi kusukwa upya ili lifanye kazi bila kufuata matakwa ya wanasiasa wa chama tawala.
Hata hivyo, kama alivyokuwa amejibu mapema wakati akihitimisha hoja za wabunge, Nchimbi alisema ni kweli kwamba Jeshi la Polisi halipaswi kufanya kazi kwa maelekezo ya wanasiasa na kwamba ndiyo sababu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, anaendelea kuwa kazini.
Nchimbi aliongeza kuwa ripoti hizo wamezisoma lakini wanajipa muda kuzifanyia kazi kwani endapo watakurupuka pasipo kuangalia mazingira mwisho wake unaweza kuwa mbaya.
“Unajua ukikutana na mtu aliyetoka kuombwa rushwa na trafiki halafu ukamuulizia utendaji wa jeshi hilo, atakwambia hakuna watu wabaya kama hao. Lakini ukikutana na dereva aliyepata ajali akakatika mguu halafu akaokolewa na trafiki, ukimuuliza utendaji wa jeshi hili, atasema hakuna watu wazuri kama hao,” alisema.
Majibu hayo yalimwinua tena Lissu na kutoa hoja ya kuondoa shilingi akisema Waziri Nchimbi ametoa maelezo ya mzaha wakati tume aliyoiunda yeye na ile ya haki za binadamu iliyoundwa na rais ni kwanini wameshindwa kuzifanyia kazi.
Kabla ya Waziri Nchimbi kujibu, Waziri Sitta ambaye alikuwa akikaimu nafasi ya waziri mkuu aliinuka na kutoa maelezo kuhusu sakata hilo.
Sitta alisema wanasiasa wanapaswa kuwatendea haki wananchi akifafanua kuwa; “Hapa kuna tuhuma nzito dhidi ya Jeshi la Polisi, kuna tuhuma nzito dhidi ya serikali ya CCM na zinatolewa na wenzetu wabunge tunaowaheshimu kutoka upande wa upinzani.
“Nataka kushauri mheshimiwa mwenyekiti, kanuni ya 103 si mahala pake kuzungumza jambo zito namna hii, kwa sababu inahitaji hoja ikae vizuri, iwe na ushahidi, majibu yawepo.
“Sasa haya ukiyachanganya ni furushi kubwa kwa wananchi wetu, ningemshauri mheshimiwa Lissu atumie kanuni nadhani ya 53 apewe nafasi kwenye mkutano ujao alete hoja binafsi kwa mujibu wa kanuni, tuwe na muda wa kutosha kupeana hoja tuijadili vizuri tutoe majibu yanayostahili,” alisema Sitta na kufanikiwa kumpoza Lissu.
CHADEMA yamshukia Tendwa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imesema kuwa imeona mapendekezo yaliyoandaliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa, ambayo lengo lake ni kupiga marufuku mikutano ya vyama vya siasa wakati ambao si wa kampeni za uchaguzi.
Kauli hiyo ilitolewa na Msemaji Mkuu wa kambi hiyo kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Josephat Nyerere, wakati akisoma maoni ya upinzani bungeni jana, akisema kuwa kwa mapendekezo haya, haki ya vyama vya siasa kufanya shughuli za kisiasa itakuwa imeuawa na serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kumtumia msajili wa vyama.
Nyerere ambaye pia ni Mbunge wa Musoma Mjini alisema kuwa mapendekezo hayo ya Tendwa ambayo lengo lake ni kufanya marekebisho kwenye sheria ya vyama vya siasa, ambayo yakikubaliwa yatasababisha kupiga marufuku mikutano ya siasa yanatokana na shinikizo la CCM na kwamba yana lengo la kuidhibiti CHADEMA.
“Kwa miaka mingi CCM na viongozi wake wamekuwa wakivikejeli vyama vya upinzani kwa kuviita vyama vya msimu. Kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita, CHADEMA kimethibitisha kuwa si chama cha msimu kwa kufanya mikutano na maandamano kwa wingi kuliko chama kingine cha siasa. Matokeo yake sasa CCM na serikali yake wanakula njama ya kuzuia vyama vya upinzani kufanya mikutano ya siasa,” alisema.

Bonyeza Read More Kuendelea



CCM yadaiwa kusababisha vurugu za udini
Wakati serikali ikitoa kauli bungeni kulaani tukio la kulipuliwa kwa Kanisa Katoliki mjini Arusha na kudai hatua za uchunguzi zinaendelea, baadhi ya wabunge wa CHADEMA, wamesema vitendo vya vurugu za kidini vinavyoendelea nchini ni matunda ya serikali hiyo ya CCM.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA) alisema kile kilichotokea Arusha pamoja na matukio ya kuvamiwa kwa viongozi wa kidini visiwani Zanzibar ni ukimya wa serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ikiwa ni pamoja na kuchochea matendo hayo.
“Nchi hii imeshuhudia baadhi ya watu wakifanya mihadhara ya kidini na kuhamasisha uchochezi, magazeti yanaandika kuchochea udini, zipo radio zinatangaza mchana kweupe kukashifu dini nyingine, lakini serikli hii iko kimya.
“IGP Omar Mahita, alitangaza mchana kweupe kuwa Chama cha Wananchi (CUF) ni cha kigaidi, akaonesha na visu kwenye vyombo vya habari, lakini serikali hadi leo haijasema kitu juu ya hilo,” alisema.
Lissu aliongeza kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, CCM iliweka kwenye ilani yake kuwa itawapatia Waislamu Mahakama ya Kadhi na ilipoona haiwezi kufanya hivyo ikawasingizia maaskofu kuwa ndio hawataki mahakama hiyo iwepo.
“Serikali hii ndiyo ilisema CHADEMA ni chama cha Wachaga, chama cha Wakristo, chama cha Wakatoliki. Leo wanajigeuza na kuanza kujifanya wanachukia vitendo hivi.
“Mheshimiwa Spika lazima tuambiwe kwanza CUF imeacha lini kuwa chama cha kigaidi na Uislamu wenye itikadi kali, CHADEMA kimeacha lini kuwa chama cha Wachaga, Wakristo na Wakatoliki,” alihoji Lissu.
Naye Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde, alisema kuwa silaha kubwa iliyobaki kulinusu taifa hili kwa sasa ni kusema ukweli kwani bila kufanya hivyo miaka sita ijayo hali itakuwa mbaya.
Alisema kuwa lazima Watanzania wakubali kuwa nchi imegubikwa na matukio ya udini na ukabila ingawa serikali ama kwa kufanya makusudi au rais na Waziri Nchimbi kudanganywa wamekuwa wakishindwa kuchukua hatua.
Silinde alisema kuwa kama ilivyoandikwa kwenye maandiko matakatifu kuwa itafika wakati wenye macho hawataona na wenye masikio kutosikia, na kuifananisha hali hiyo na CCM sasa.
“Serikali ya CCM haioni tena, haisikii wala haiwezi kunusa tena, hili ndilo anguko la serikali hii,” alisema.
Wataka polisi ivunjwe
Kuhusu utendaji wa Jeshi la Polisi, Silinde alisema limeoza, hivyo kupendekeza livunjwe na majukumu yake kuundiwa kitengo ndani ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, maarufu kama Sugu naye aliungana na wenzake akisema kuwa serikali imekosa mikakati ya kutuliza vurugu hizo na badala yake inakuja na maneno ya kisiasa yasiyo na ufumbuzi wa tatizo.
Sugu alishauri kuwa Jeshi la Polisi livunjwe kwa kushindwa kazi na kisha liundwe upya kwa kuwapa kazi vijana wasomi ambao wana uwezo mkubwa badala ya kung’ang’ania kuwaongeza wastaafu mikataba.
Viroba vipigwe marufuku
Serikali imeombwa kupiga marufuku pombe aina ya konyagi inayofungwa kwenye mifuko ya plastiki maarufu kama viroba, kwa madai kuwa inaua nguvu kazi ya taifa.
Ushauri huo ulitolewa na Mbunge wa Viti Maalumu, Lidiana Mng’ong’o, wakati akichangia hotoba ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Alisema kuwa pombe hiyo ambayo kwa sasa inauzwa kiholela mikoani imekuwa ikinywewa bila utaratibu na hata wakati mwingine kwa wale wasiopaswa kuinywa.
“Mheshimiwa Naibu Spika, naomba serikali ipige marufuku pombe za viroba. Wanafunzi siku hizi hawaingii tena darasani wanaishia kunywa viroba, vijana mitaani, waendesha bodaboda wanakunywa viroba kuanzia asubuhi,” alisema.
Keisy: Wabunge wanaojichubua wakamatwe
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Keisy, ametoa mpya akitaka wabunge wanaotumia vipodozi kujibadilisha sura zao kuwa weupe wakamatwe kwa kuwa wanaitia hasara serikali kuwatibu muda mrefu wanapopata ugonjwa wa saratani.
Keisy alitoa kauli hiyo wakati Bunge limekaa kama kamati kupitia vifungu vya bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kifungu cha mshahara wa waziri.
“Wanaokamatwa na vipodozi visivyokidhi viwango wanakamatwa na kuchomewa bidhaa zao, lakini wanaokamatwa na bangi wakinunua au kuvuta wote wanakamatwa kama ilivyo kwa wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya wanakamatwa na kufungwa.
“Meza za kina mama zimejaza vipodozi hivyo hafifu wanavyovitumia kujibadili rangi hadi watu wa kijijini wanawakimbia wakidhani ni Wazungu,” alisema Keisy.
Alifafanua kuwa kuna wagonjwa wa kansa ya kujitakia na wakifanyiwa upasuaji wanakaa muda mrefu bila kupona hivyo kuipa hasara serikali.
“Serikali itupe majibu kamili hao wanaojipodoa na kuharibu sura zao… Wachina si Wachina inawachukulia hatua gani tukianzia humu ndani, maana watumiaji na wauzaji wasinyanyaswe wakati na watunga sheria wamo humu,” aliuliza Keisy na kuwaacha wabunge wakiangua vicheko.
“Natoa ushauri wa bure, wanaotaka kuwa weupe watuone sisi wapate mbegu,” alisema .
Hata hivyo, akijibu hoja ya Keisy, Waziri wa Afya, Dk. Hussein Mwinyi, alisema kuwa wao kama wizara kazi yao ni kuhakikisha usalama wa vipodozi hivyo wala si kuwafuatilia watumiaji.
“Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ndiyo wenye kazi ya kuhakikisha ubora wa vipodozi hivyo kwa watumiaji. Na kuhusu kuwakamata watumiaji hiyo ni kuingilia haki ya kijinsia,” alisema Mwinyi.
Watoto 800,000 waishi mitaani
Watoto 849,051 katika halmashauri 95 wametambuliwa kuishi katika mazingira hatarishi.
Takwimu hizo zilitolewa bungeni na Waziri wa Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
Simba alisema kuwa katika idadi hiyo wasichana ni 407,544 na wavulana ni 441, 507, ambapo sasa wanapatiwa huduma za elimu, afya, chakula na msaada wa kisheria na kisaikolojia kupitia wadau mbalimbali.

No comments:

Post a Comment