Wednesday, May 15, 2013

Katiba mpya kupingwa mahakamani

Jukwaa la Katiba Tanzania limesema linatarajia kwenda Mahakama Kuu ndani ya siku saba kuanzia jana kuweka zuio la kuendelea kwa mchakato wa Katiba mpya.

Zuio hilo linatokana na mchakato huo kuwa na kasoro nyingi zitakazosababisha kukosekana kwa Katiba mpya na ya kidemokrasia.

Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deus Kibamba, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Alisema timu ya mawakili 10 wakiongozwa na mwanasheria wa masuala ya Haki za Binadamu, Dk. Rugemeleza Nshala, wanaandaa hoja muhimu za kuwasilisha mahakamani.

Hata hivyo, alipotakiwa na NIPASHE kutaja majina ya mawakili wengine, Kibamba alisema kwa sasa hayako hadharani ila yatatajwa siku chache zijazo na kwamba kwa sasa wamejichimbia wakiandaa hoja za msingi.

“Ingawa mchakato wa Katiba unahitajiwa na kila Mtanzania mwenye nia njema na nchi yake, ila unatakiwa uwe bora utakaozaa Katiba bora, kinachoendelea sasa ni bora mchakato ambao unaweza kuzaa bora Katiba,” alisema Kibamba.
Kibamba alisema uamuzi .

wakwenda mahakamani unatokana na Jukwaa hilo kupuuzwa na mihimili ya Bunge na Serikali pamoja na wasaidizi wa Rais kuwakataza kuonana na Rais, Jakaya Kikwete, kwa ajili ya kuwasilisha maoni yao na kuona njia pekee ya kutafuta haki ya Watanzania ni kwenda mahakamani.

“Tunakwenda mahakamani kuomba isimamishe mchakato wa Katiba mpya hadi watakapoona umuhimu wa kuheshimu na kufuata ratiba waliojiwekea, kuheshimu misingi ya uandikaji na iamuru kusimama kwa mchakato huo,” alisema. 

Alisema kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Marekebisho ya Katiba, Aprili 4 hadi Mei 2, mwaka huu ni uandishi wa rasimu ya Katiba, Mei 3 hadi 8 ni uchapishaji wakati Mei 9 hadi Juni 7, mwaka huu ni kutolewa kwa elimu ya rasimu ya Katiba.

Hata hivyo, alisema hadi kufikia jana zilikuwa zimepita siku saba na tume haijazungumza lolote kwa Watanzania.

Aliainisha kasoro zilizopo kwenye mchakato huo kuwa ni kupelekwa kwa kasi inayoathiri misingi mikuu ya mchakato wa ujenzi wa Katiba mpya hususani uelewa na hamasa, ushiriki, umiliki wa wananchi na hivyo mchakato huo unaweza kuzaa Katiba isiyo na sauti na maoni ya Watanzania wote.

Alisema kuandika Katiba mpya ni mchakato wa kisiasa, kwa maana ya kutafuta mwafaka wa kitaifa ambao unapitia njia na hatua za kisheria.

Alisema baada ya wabunge wa vyama vya Chadema na NCCR-Mageuzi kutoka nje ya ukumbi wa Bunge Novemba mwaka 2011, Rais alikutana na vyama vya siasa na mashirika yasiyo ya kiserikali ili kupata mwafaka na kwamba waliwasilisha mapendekezo yao kwa Rais.

Kwa mujibu wa Kibamba, madai ya vyama vya siasa yaliyokuwapo kwenye ajenda za vyama vya siasa yalipotea baada ya mkutano huo na sasa yameanza kujitokeza baada ya kuona haja ya utekelezaji.

Alisema Jukwaa hilo linaitaka serikali kusikiliza madai hayo yakiwamo ya asasi za kijamii, makundi ya wasomi, wafanyakazi na wananchi kwa upana wake na kuyafanyia kazi.


Bonyeza Read More Kuendelea





Alitaja nyingine kuwa ni mabadiliko ya sheria inayoongoza mchakato huo kwa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kutoelezwa vema kwenye sheria, kuanzia upatikanaji wa wajumbe wake kutojulikana moja kwa moja kama utahusisha uchaguzi ngazi ya vijiji, mitaa na kata au shehia kwa upande wa Zanzibar.

Alisema hali hiyo ilisababisha dosari nyingi kwenye uchaguzi wa wajumbe wa wilaya na kuzua malalamiko na Tume ilikiri kupokea malalamiko hayo na kutoa msimamo wake kuwa haihusiki na kutoa mwongozo wowote wa malalamiko hayo. Alisema wajumbe wengi kwenye mabaraza hayo walichaguliwa kwa mizengwe, rushwa na ushabiki wa kiitikadi za vyama, dini na wengi hawana sifa muhimu za kuchambua, kutafsiri na kujadili rasimu ya Katiba mpya.

Jingine ni Bunge Maalum la Katiba na kusema kuwa kinachopaswa kufanyika ni kuwaondoa wabunge wote na kuchagua watu wengine huru, kwa kuwa waliopo Dodoma na Zanzibar hawakuchaguliwa kwenda kutunga Katiba mpya bali sheria za kawaida za nchi ikiwamo marekebisho ya Katiba.

Alisema kati ya wabunge 357 walioko Bungeni sasa, vyama vya upinzani vina wabunge takribani 90 ambao ni asilimia 25 ya Bunge zima, hivyo kuwatumia hao kwenye Bunge la Katiba ni kuendeleza U-CCM. 

Alisema jingine ni kura ya maoni kusimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ambayo inalalamikiwa kuwa siyo huru na ndiyo moja ya sababu za kuanza kwa mchakato wa Katiba mpya, hivyo kuitumia hiyo ni wazi kuwa haikidhi vigezo.

Alisema pia uchaguzi wa mabaraza ya Katiba umevurugwa kwa makusudi na tume hiyo kwa kushirikiana na chama tawala na kwamba idadi ya madiwani nchini ni 4,453 na vyama vya upinzani vina madiwani 450, hivyo ni dhahiri kuwa CCM ilijipenyeza kwenye mchakato huo.

LIPUMBA ALALAMIKIA MCHAKATO
Wakati huo huo; Chama cha Wananchi (CUF) kimelalamika kuwapo kwa upendeleo wa kuwapata wajumbe wawakilishi wa mabaraza ya katiba ngazi ya kata, huku ikitoa tahadhari kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kurekebisha mfumo huo kabla haujaleta matatizo katika upatikanaji wa katiba mpya.  Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, jana wakati wa utoaji wa taarifa juu ya kikao cha Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la chama hicho jijini Dar es Salaam.

Lipumba alisema mfumo unaoendelea sasa wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya katiba ngazi ya Kata hautendi haki kwa kuwa unapendelea chama kimoja.

Alisema kuna eneo wajumbe saba wa  CUF kati ya nane walipita katika uchaguzi wa katiba ngazi ya mtaa, lakini walipofika ngazi ya kata walienguliwa wote na nafasi hiyo kupewa mgombea wa CCM.

Alitoa wito kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuharakisha mchakato huo kwa kuwa kasi yake hairidhishi ukilinganisha na muda wa kukamilika kwa Katiba hiyo mwaka 2014 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. 

No comments:

Post a Comment