UZINDUZI wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani, Kata ya Iyela, Jiji la Mbeya uliofanywa na CHADEMA juzi umevunja rekodi na kuelezwa kuwa chama hicho kina mvuto na kuendesha kampeni zake kama Rais wa Marekani, Barrack Obama.
Wakati kampeni hizo zikiwa zimeanza tayari habari za uhakika ambazo Tanzania Daima Jumapili limezipata zinadai kuwa CCM wameandaa mpango mchafu wa kughushi shahada za kupigia kura zinazotengenezwa eneo la Kabwe jijini humo na mwananchi mmoja (jina tunalo).
Mmoja wa mashuhuda katika kuandaa mpango wa utengenezaji wa shahada bandia ambaye ameamua kujivua uanachama wa CCM na kujiunga na CHADEMA, alisema ameshindwa kuvumilia kile alichokiona baada ya kukabidhiwa shahada 300 za bandia.
Mwanachama huyo wa CCM, ambaye jina lake limehifadhiwa, alisema kazi ya kukusanya shahada halali na kuzibadilisha inafanywa kwenye nyumba moja maeneo ya Kabwe ambako mashine maalumu imekuwa ikitumika kubandua picha na kubandika nyingine.
“Ndiyo maana CCM wana uhakika wa kushinda, nimeona niseme wanabadilisha picha isipokuwa namba ni zilezile ambazo zipo kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, mkifuatilia mtagundua picha hazifanani na mpiga kura halali aliyejiandikisha,” alisema.
CHADEMA waliendelea na uzinduzi wa kampeni zao kwa kumnadi mgombea wao, Charles Mkela, aliyeibuka mshindi kati ya wagombea wengine sita wa chama hicho waliokuwa wakiwania kuiwakilisha kata hiyo dhidi ya vyama vingine vya siasa.
Mwenyekiti wa CHADEMA wa Wilaya ya Mbeya Mjini na kiongozi wa kampeni, John Mwambigija, alisema kuwa chama hicho kimegundua njama zote za kuvuruga uchaguzi huo na kuufanya usiwe halali baada ya kulalamikia mapema utengenezaji wa shahada bandia.
“Hawa tutabanana nao kwenye daftari la kudumu la wapiga kura tulilopewa na Tume ya Uchaguzi, wamenunua shahada kutoka kwa watu, wanabadilisha picha, tunawaomba wale walioshiriki kughushi waje siku ya kupiga kura,” alisema Mwambigija.
No comments:
Post a Comment