A: UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, dira
ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ni kuhakikisha kuwa raslimali za
mifugo na uvuvi zinaendelezwa na kutunzwa katika mazingira endelevu kwa ajili
ya ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi. Aidha dira inalenga kuhamasisha ufugaji wa
kisasa na uvuvi endelevu ili kujenga uchumi endelevu kwa jamii nzima ya
wafugaji na wavuvi na taifa kwa jumla.
Mheshimiwa Spika, Licha
ya ukweli kwamba wafugaji na wavuvi wana mchango mkubwa katika uchumi wetu,
Serikali hii ya CCM imeshindwa kuwapatia maeneo maalum kwa ajili ya malisho kwa
maendeleo ya mifugo yao. Wafugaji wamekuwa wakihamishwa na au wakifukuzwa
kutoka eneo moja la nchi hadi eneo lingine kama vile hawana haki ya kufanya
shughuli za kiuchumi kama ufugaji katika nchi yao. Ni aibu kwa Serikali kushindwa kuwapatia wafugaji mahitaji
muhimu ambayo yangepelekea ufugaji wao kuwa wa kisasa, kibiashara na endelevu
kama ilivyobainisha katika dira ya Wizara hii.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA, haioni sababu ya Serikali
kuwapatia wafugaji maeneo ya kufugia kwa
kuwa wafugaji wangeweza kuingia ubia na mashamba
makubwa ya mifugo ambayo yalikuwa yanamilikiwa na Ranchi za Taifa, lakini kutokana
na ubinafsi na ufisadi uliofichwa kwenye kivuli cha cha sera ya ubinafsishaji, Serikali ya CCM imesimamia zoezi la viongozi wa serikali na Chama cha Mapinduzi
wakigawiana ranchi hizo na kuwaacha wafugaji wakifukuzwa ovyo na kupewa jina la
wachungaji.
Mheshimiwa Spika,
kwa upande wa wavuvi hali ni hiyo hiyo, kwani mapato mengi ya Serikali yanayokusanywa kutoka katika sekta ya uvuvi
yanatokana na wavuvi wadogo ambao mara zote wao ndio waathirika wa mfumo
kandamizi wa Serikali. Zana za uvuvi
zinapokamatwa, wao ndio wanapata hasara, lakini wauzaji wa zana hizo za
uvuvi wala hawaulizwi na wala hakuna
hatua zinazochukuliwa dhidi yao.
Mheshimiwa
Spika, changamoto kubwa inayozikabili sekta hizi za ufugaji na uvuvi ni kwamba
sekta zote mbili hazina bima dhidi ya majanga ambayo yanaweza kutokea. Katika mazingira kama haya, dhana ya kuwa sekta
za kisasa, kibiashara na endelevu inakuwa ngumu sana.
Mheshimiwa Spika, katika
hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa mwaka wa fedha
2012/2013 liainisha mapungufu makubwa katika ya kiutendaji na kiuwajibikaji kwa
wizara hii na kuitaka Serikali kufanya mambo yafuatayo:
1.
Kuwajibika kwa uzembe wa kuitelekeza meli ya
uvuvi ya Tawariq iliyokamatwa ikifanya uvuvi haramu katika ukanda wa bahari ya
hindi hadi meli hiyo kuharibika kabisa na kuanza kuzama bila faida yoyote?
2.
Kuchukua hatua dhidi ya mwekazaji wa Kagera
Sugar kwa kushindwa kuendeleza shamba la ukubwa wa hekta 45,000 (sawa na ekari
112,500) kinyume na mkataba.
3.
Kueleza sababu za kuwapa mashamba makubwa
wawekezaji wa kigeni na kuwanyanyapaa wafugaji wa asili kinyume cha sheria.
4.
Kutatua migogoro ya ardhi baina ya wakulima na
wafugaji ambayo mara kadhaa imesababisha uvunjifu wa amani na umwagaji damu
miongoni mwa wananchi.
5.
Kujenga viwanda vya kusindika nyama katika
mikoa ya wafugaji ili kuongeza thamani ya bidhaa ya nyama na hivyo kukuza
uchumi.
6.
Kuweka wazi kiasi cha fedha kinachopatika kama
mrahaba kutokana na uvuvi katika bahari kuu, pamoja na fedha za leseni kwa meli
zinazofanya uvuvi katika ukanda wa bahari kuu.
Bonyeza Read More Kuendelea
- SEKTA
YA MIFUGO
Mheshimiwa Spika, Sekta
ya Mifugo ina nafasi kubwa katika kujenga uchumi imara wa Taifa, kuongeza
kipato kwa Watanzania wanaotegemea mifugo, na kutoa fursa za ajira sanjari na
kuhifadhi rasilimali za Taifa. Sera ya mifugo inaeleza nia ya Serikali na wadau
wengine katika kukabiliana na changamoto zinazokabili Sekta ya Mifugo. Lengo
kubwa ni kujenga mazingira mazuri yatakayotoa fursa za kuongeza kipato na ajira
kwa wafugaji wadogo, kufuga kibiashara na kuongeza ajira. Ili kufikia haya
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutekeleza, malengo makuu matatu ya
kisera kama ifuatavyo:-
- Kuendeleza
Sekta ya Mifugo itakayokuwa na mwelekeo wa kibiashara, yenye ufanisi na
itakayohimili ushindani wa kimataifa;
- Kuibua mifumo
bora ya uzalishaji itakayoongeza tija miongoni mwa wafugaji wadogo na wa
asili.
- Kuhifadhi
rasilimali za mifugo na kuunda sera na taasisi zitakazosimamia maendeleo
na matumizi endelevu ya rasilimali hizo n.k.
Mheshimiwa Spika, Sera
hiyo ya mifugo imeweka wazi azma ya Serikali ya kuboresha sekta hii ya mifugo,
lakini kutokuwepo na mkakati madhubuti wa kufanikisha yale yote yanayohitajika
kufanyika na sera hii ya Mifugo ya mwaka 2006, kunaendeleza matatizo katika
sekta hii mpaka sasa.
Mheshimiwa Spika, Sekta
ya Mifugo hapa nchini ina nafasi kubwa katika ujenzi wa uchumi wa Taifa. Kwanza
kwa kuthamanisha kiwango cha nyama kinachotumika kila siku hapa nchini ikiwa kiwango hicho kingekuwa kinaagizwa toka nje ya
nchi. Pili ni kuongeza kipato kwa Watanzania wanaotegemea mifugo, na kutoa
fursa za ajira sanjari na kuhifadhi rasilimali za Taifa.
Mheshimiwa Spika, Mashamba
makubwa ya mifugo yana uwezo wa kuongeza viwango vya uzalishaji na uuzaji wa
mifugo na mazao yake nje ya nchi, ajira na kuboresha maisha ya wafanyakazi
wake. Mkakati umetumika wa kugawa mashamba makubwa ya Kampuni ya Ranchi za
Taifa KARATA (NARCO) na yale yaliyokuwa chini ya Kampuni ya Ng’ombe wa Maziwa
(DAFCO) kuwa mashamba yenye ukubwa wa kati kwa ajili ya ufugaji wa kibiashara
unaolenga kutekeleza dhana hii. Mkakati huu umeongeza upeo wa umilikaji
mashamba na pia kuwawezesha Watanzania kuingia katika ufugaji wa kibiashara.
Maeneo ya ranchi za KARATA (NARCO) yaliyobaki yataendelea kutumika kama ranchi
za mfano na maeneo yasiyo na magonjwa ya mifugo kwa ajili ya soko la nje ya
nchi[1].
Mheshimiwa
Spika, ilani ya CCM ya mwaka 2005-2010 aya ya 32 inasema kwamba, “Pamoja na kwamba Tanzania ina mifugo mingi sana; mchango wa
mifugo kwenye uchumi wa Taifa ni mdogo. Kwa lengo la kuendeleza Sekta ya Mifugo
ili ichangie zaidi ukuaji wa uchumi wa Taifa na kuwaongezea kipato wafugaji,
Serikali za CCM zitaendeleza kwa msisitizo zaidi lengo la kuzingatia zaidi
ubora kuliko wingi pekee katika ufugaji. Ili kufikia lengo hilo, hatua zifuatazo
zitachukuliwa katika kipindi cha 2005-2010:-
(a)
Kujenga mazingira ya kuvutia uwekezaji katika viwanda vya
kuongezea thamani mazao ya mifugo kama vile ukataji nyama, usindikaji wa
maziwa, utengenezaji wa bidhaa za ngozi n.k.”
Mheshimiwa Spika, na
katika Ilani ya CCM ya mwaka 2010-2015 aya ya 38 inasema kwamba; “Katika kipindi cha Ilani hii ya miaka
2010-2015, Chama Cha Mapinduzi kitazielekeza Serikali kuiendeleza sekta ya
mifugo kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kasi zaidi ili kuiwezesha kutoa mchango
mkubwa kwenye pato la Taifa kwa kuchukua hatua zifuatazo:-
(a) Serikali iandae programu kabambe ya
kuendeleza sekta ya mifugo na ufugaji. Programu hiyo ijumuishe pamoja na mambo
mengine masuala ya uendelezaji wa maeneo ya malisho, kuchimba na kujenga
malambo, mabwawa, majosho na huduma za ugani ili hatimaye wafugaji waondokane
na ufugaji wa kuhamahama.
(b) Benki ya Kilimo itakayoanzishwa iwe pia
Benki ya Mifugo ili iweze pia kutoa mikopo kwa wasomi wenye nia ya kufuga na
kuwawezesha kuingia kwa wingi katika ufugaji wa kisasa.
(c) Kuelimisha wafugaji uwiano kati ya idadi
ya mifugo na eneo.”
Mheshimiwa Spika, katika
kuonyesha kuwa CCM yale wanayoandika sio wanayosimamia katika kuinua sekta ya ufugaji hasa wa asilia ambao
unachangia zaidi ya asilimia 85 ya ufugaji wote, Kambi Rasmi ya Upinzani,
inauliza kwa mkakati huo wa CCM dhidi ya wafugaji na Ufugaji ni kwa vipi
ufugaji unaweza kuwa endelevu na wa kisasa wakati wafugaji wanaporwa maeneo ya
kulishia mifugo yao, hawapewi maeneo ya malisho, hawapati huduma za ugani,
hawapati mikopo na hawana soko la uhakika wa bidhaa zinazotokana na mifugo.
Kambi Rasmi ya Upinzani, inauliza kwa makati huo wa CCM dhidi ya wafugaji na
ufugaji ni kwa vipi ufugaji unaweza kuwa endelevu na wa kisasa wakati wafugaji
wanaporwa maeneo ya kulishia mifugo yao?. Hawapewi maeneo ya malisho, hawapati
huduma za ugani, hawapati mikopo, hawana soko la uhakika. Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali kutoa kauli juu ya ni wapi wafugaji wa asili
watafugia mifugo yao ili kuwa endelevu nay a kisasa?
jumla ya wafugaji wakulima wa vijiji vinne vya Makuyuni, Loikisale, Naiti na Mswakini katika Wilaya ya Monduli wanatishiwa
kuhamishwa kutokana na mkakati mahususi ulioasisiwa na Mheshimiwa Waziri
Kagasheki wa kutangaza maeneo hayo kuwa ni Wildlife Management Area (WMA).
Uhakika ni kwamba WMA hiyo ni hewa haipo na ukweli ni kwamba eneo hilo kinapewa
kikundi kinachoitwa ELEWANA AFRIKA.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwaeleza Wafugaji hao, ni wapi
wanakwenda na mifugo yao? Aidha, kwa kuwa utaratibu wa kuanzisha WMA huwa
inaanzishwa kwa kupata ridhaa za wanavijiji ambao kwa hiari yao wanatoa maeneo
ya vijiji vyao kuwa WMA na ndipo kazi ya Waziri husika inafuata ya kutoa idhini
ya uanzishwaji wa hiyo WMA. Kwa kuwa huo
ndio utaratibu wa kuanzisha WMA, Je, ni kwanini vijiji hivyo havikupewa fursa
hiyo?
Mheshimiwa Spika, Mgogoro wa ardhi katika eneo la
Loliondo ni taswira nyingine ya jinsi ambavyo Serikali ya CCM imekiuka haki za
wafugaji wa Kimaasai kwa manufaa ya wawekezaji wa kigeni katika sekta ya
uwindaji wa kitalii.
Mheshimiwa Spika,
mgogoro wa Loliondo bado haujapatiwa ufumbuzi na sasa umeanzishwa mgogoro
mwingine Wilaya ya Monduli. Hii ni kwa makusudi kuhakikisha wafugaji wa asili
wanakwisha kabisa?
Mheshimiwa Spika,
hapo kabla ya uhuru Serikali ilitenga
eneo la zaidi ya hekta 18,000 sawa na ekari 45,000 wilayani Maswa
lililojulikana kama SHISHIYU Holding
ground kwa ajili ya kunenepesha mifugo kabla ya kusafirishwa kwenye kiwanda
cha Nyama cha Tanganyika Packers, ambacho kimekufa, cha ajabu ni kwamba katika
eneo hilo bado hadi sasa wafanyakazi wa Idara ya mifugo wapo pale lakini mifugo
hainenepeshwi. Je, hii si hujuma kwa sekta ya mifugo na wafugaji hasa wa wilaya
ya Maswa?
Mheshimiwa Spika,
si hilo tu bali pale Ipala wilaya ya Nzega Mkoa wa Tabora kuna kituo cha treni
kilichokuwa kikitumika kupakia ng’ombe kwenda Dar es Salaam. Eneo hilo lilikuwa
limetengwa rasmi kwa ajili ya mifugo na kuna miundombinu ya kupakia mifugo
kwenye treni, jambo la ajabu ni kwamba serikali imeligeuza eneo lile kuwa
hifadhi ya misitu. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwa wafugaji
wanaoishi eneo hilo waachiwe eneo litumike kwa malisho na miundombinu iliyopo.
Mheshimiwa Spika,
aidha, kitendo kinachofanywa na Wakuu Wilaya na Wakurugenzi wa Halimashauri kuwahamisha
wafugaji kwa nguvu katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa kuwalipisha
mamilioni ya fedha wafugaji hao (Mfano mfugaji mmoja wa mikumi alitozwa faini
ya shilingi milioni 42.78 kwa kukamatwa ng’ombe wake, mfugaji wa chunya million
19 n.k) nao ni ushahidi wa dhahiri kwamba Serikali hii ya CCM haina dhamira ya
dhati katika kuhakikisha wafugaji na ufugaji unakuwa na tija katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika,
wafugaji wa asili ya kisukuma,kimasai,wairaq na wabarbaig katika wilaya za
Kilombero, Ulanga, Kilosa, Mbarali, Chunya, Kilindi, Handeni,Mpanda, Rufiji n.k
wamepata matatizo makubwa sana na
wengine wameuawa na vyombo vya dola, kosa lao kubwa ni kuwa na mifugo mingi
iliyosababisha wahame toka mikoa ya kanda ya ziwa kwa sababu za malisho. Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge, je kosa la ndugu zetu hao
ni kuwa na utajiri wa mifugo mingi au nini hadi wanadharauliwa na kunyanyaswa
na kufanywa kuwa watanzania wa daraja la nne katika nchi yao?
Mheshimiwa Spika,
kutokana na ukweli kwamba Wizara
imeshindwa kuwatetea na kuwalinda wafugaji wa asili, hivyo basi, Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali iwaeleze wafugaji ni wizara gani itakayosikiliza na
kutatua matatizo yao?
Mheshimiwa Spika, kama
ambavyo imekuwa ikitokea katika maeneo ya Ranchi zilizokuwa za mkoa wa Kagera,
Rukwa, Morogoro, Tanga, Pwani watu waliopewa 4000 ha au ekari 10,000 za maeneo
ya Ranchi za Taifa kama wawekezaji, watu hao wameshindwa kuziendeleza ranchi
hizo kwa vile wengine hawana hata mifugo ya kuweka katika maeneo hayo. Kukosa
mifugo ya kuendeleza eneo hilo kwa makusudi watu hao huona kuwa mbadala
unaobakia ni kupangisha maeneo hayo kwa wawekezaji kutoka nchi jirani.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaona lingekuwa ni jambo la busara kama ushirika wa wafugaji
au mwekezaji mmoja mmoja kupewa ekari 1000 ikiwa eneo lote la ekari 10,000 lingegawanywa ili kurahisisha
uwekezaji wake na kufanya kuwa endelelevu. Kwa eneo dogo uwezekano wa kupata
mkopo toshelezo kwa uwekezaji toka benki zetu na asasi zingine za fedha ni
rahisi kwani hata investiments risks inakuwa ni ndogo na inakuwa imesambaa kwa
wawekezaji wengi.
Mheshimiwa Spika,
wakati Waziri akijibu swali Na. 26 kuhusu maeneo ya Ranchi za Mkoa wa Kagera, “Je,
kwa nini Serikali isiyarudishe maeneo hayo kwani waliopewa wanayakodisha kwa
wafugaji toka nchi jirani? Je, ni
Watanzania gani kwa majina waliogawiwa maeneo kwenye ranchi hizo? Mheshimiwa
Spika, orodha ya majina ya Wawekezaji Watanzania waliogawiwa maeneo hayo ya
ranchi ipo, nitaomba kukutana na Mheshimiwa Mbunge baada ya hapa ili nimkabidhi
orodha hiyo”.
Mheshimiwa Spika, hadi
sasa hivi majina hayo ya wamiliki, Waziri ameshindwa kuitoa kama alivyoahidi
ndani ya Bunge, hoja ni kama kweli wamiliki ni watanzania ni kwanini
wanashindwa kuweka majina hadharani? Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani
inamtaka Waziri kutoa kwa wabunge majina hayo ya wamiliki na uraia wao
hadharani.
Mheshimiwa Spika, ili
kuiwezesha sekta ya mifugo kutoa mchango stahiki kwa Taifa hili ni lazima
uboreshaji katika sekta ya mifugo wetu ufanyike kwani wanachokosa wafugaji wetu
ni Ardhi na elimu ya ufugaji yenye mafanikio kutokana na kutumia mbinu za
zamani za kuzalisha mifugo. Changamoto kubwa katika sekta hii ni kukosekana kwa
mbinu za kisasa, vifaa na madawa ya uhakika kuhudumia wanyama. Aidha, mifugo
mingi inatunzwa kienyeji na matokeo yake kukosa soko la kimataifa kama zilivyo
nchi nyingine. Kama elimu ya kutosha itatolewa na kuruhusu wawekezaji wa ndani
katika sekta ya mifugo changamoto hizo zitapungua kwa kiasi kikubwa na hivyo
kutoa nafasi ya ongezeko la bidhaa zitokanazo na mifugo.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inasema wawekezaji wa ndani, kwa maana kwamba wafugaji
wa asili wao mtaji wao mkubwa ni mifugo na NARCO wao mtaji wao ni utaalam na
miundombinu iliyopo tayari. Hivyo basi, ni rahisi wa ubia huo kati ya wafugaji
wa asili na NARCO kuleta tija zaidi kuliko mwekezaji toka nje.
Mheshimiwa Spika, kutokana
na kuongezeka kwa idadi ya watu, kipato na ukuaji wa miji kwa nchi
zinazoendelea Duniani, Tanzania ikiwa ni mojawapo, mahitaji ya bidhaa za mifugo
nayo yamekuwa yakiongezeka pia. Takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania pekee itaongeza mahitaji mara nne kwa mwaka 2030. Hivyo
ni jukumu la Serikali sasa kulieleza Bunge hili ni kwa vipi Wizara imejipanga
kukabiliana na changamoto ya ongezeko hilo la mahitaji ya nyama kwa muda huo?
Mheshimiwa Spika,
hivi sasa ni 2% tu ya mifugo yote inayozalishwa na kufugwa kibiashara, hivi
sasa Tanzania ina machinjio ya kisasa manne (4) ambayo
hayatoshelezi kwani mahitaji ya nyama safi na salama yanaongezeka kila siku. Aidha, inaonyesha kuwa chini ya 1% ya nyama yote
iliyosindikwa ndiyo inazalishwa hapa nchini na sehemu yote iliyobaki inaagizwa
na kuingizwa nchini kutoka Kenya. Vile vile taarifa hiyo inaonyeshwa kuwa zaidi
ya tani 700 ya nyama safi inaaagizwa toka nje ya nchi kila mwaka wakati
mahitaji ya nyama ndani ya nchi na Kanda yetu ya ushirikiano yanazidi
kuongezeka[2].
Mheshimiwa Spika,
Tanzania ni nchi ya pili nyuma ya Ethiopia kwa kuwa na mifugo wengi katika Bara
la Afrika, sasa kwa hali ya kawaida tu inakuwaje nchi yetu inaagiza nyama
kutoka nje ya nchi?
Mheshimiwa Spika,
Tanzania ina rasilimali kubwa ya maliasili ikiwemo ardhi, malisho na idadi
kubwa ya mifugo. Kati ya jumla ya hekta milioni 94 za rasilimali ya ardhi,
hekta milioni 60 ni nyanda za malisho zinazofaa kwa ufugaji. Kwa sasa kuna
ng’ombe milioni 21.3, mbuzi milioni 15.2 na kondoo milioni 6.4. Mifugo wengine ni pamoja na nguruwe milioni
1.9, kuku wa asili milioni 58[3].
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa taarifa ya utekelezaji wa mpango na bajeti ya mwaka 2012/2013 na
makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2013/2014 kiambatanisho Na.3
kinaonyesha kuwa kwa mikoa 21 wilaya 69 na vijiji vilivypimwa 479 eneo la
malisho ambalo linasadikiwa kuwa limetengwa kwa ajili ya wafugaji kuwa ni hekta
milioni 1.28. Hii ni sawa na asilimia 2.13 ya hekta million 60 za nyanda za
malisho katika nchi hii.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inamtaka Mhe Waziri awaeleze wafugaji kwa ng’ombe
milioni 21.3 na mbuzi na kondoo milioni 21.5 wanatakiwa wachungwe kwenye eneo
la ukubwa gani?
Mheshimiwa Spika,
uzalishaji wa mifugo umegawanyika katika mifumo mikuu miwili ambayo ni ufugaji
huria na ufugaji shadidi. Mfumo wa ufugaji shadidi japo sio mkubwa nchini,
unatiliwa mkazo zaidi katika kuendeleza ufugaji na uwekezaji kwani unachangia
zaidi kwenye uchumi wa soko.
Mheshimiwa Spika, kwa upande mwingine, mfumo wa ufugaji huria
ambao hufanywa na wakulima-wachungaji na wachungaji -wahamaji, ni mfumo
unaotegemea upatikanaji wa malisho na maji kwa msimu na matokeo yake
husababisha wafugaji kuhamahama. Mfumo huu unakabiliwa na matatizo ya utunzaji
duni wa mifugo, matumizi duni ya teknolojia za kisasa, kuhodhi mifugo wengi
zaidi ya uwezo wa ardhi na ukosefu wa mazingira mazuri ya masoko.
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa tafiti uliofanywa na asasi ya kiraia ya Tanzania Pastoralists, Hunters
and Gatherers Organization- (TAPHGO)
kuhusu mfumo wa biashara ya mifugo Tanzania inaonyesha kwamba sekta ya ufugaji
Tanzania inachangia asilimia 18 ya pato la Taifa, uzalishaji wa nyama kwa mwaka unakadiriwa
kuwa ni tani 259,800, kwa mifugo inayofugwa kwa ajili ya nyama pekee huchangia
tani 181,800.
Mheshimiwa Spika,
aidha mchango wa wafugaji ambao pia ni wakulima huchangia asilimia 98 ya
uhitaji wote wa nyama hapa nchini, huku asilimia 2 hutoka kwenye ranchi za
taifa. Wakati mbuzi na kondoo huchangia tani 75,800. Thamani ya nyama
inayozalishwa inakadiriwa kuwa ni
shilingi bilioni 727.44, kati ya hizo shilingi bilioni 537.94 zinachangiwa na
nyama ya ng’ombe na zilizobaki shilingi bilioni 189.5 ni kwa mbuzi na kondoo.
Mheshimiwa Spika, katika
hotuba ya Rais wakati wa kufungua
mkutano wa uwekezaji kwa shabaha ya kuibua maendeleo ya Mkoa wa Mara kwa
kutumia rasilimali na utajiri uliopo mkoani Mara “Lazima tuanze kutekeleza misingi ya ufugaji wa kisasa na tujipange
vizuri kwa uwekezaji kwenye sekta hii. Naomba tutenge maeneo maalum ya ufugaji
wa kisasa. Kwa mfano, tukigawa maeneo ya ukubwa wa hekta 2,000 kila moja na
tukawagawia watu kwa ajili ya kufuga kisasa. Watakaopewa maeneo hayo wahimizwe
na kusaidiwa wayaendeleze kwa malisho na huduma muhimu za maji, majosho pamoja
na za matibabu kwa mifugo. Maeneo hayo yakatumiwa kunenepesha ng’ombe wa nyama
tunawezesha kuwepo kiwanda cha nyama kitakachonunua toka kwao mifugo ya
kuchinja. Kiwanda hicho kitatengeneza soko la uhakika kwa wafugaji”.
Mheshimiwa Spika, kauli
hiyo ya Mhe Rais imekuja muda ambao tayari maeneo mengi mazuri yaliyokuwa
yanamilikiwa na Serikali tayari yamekwishachukuliwa, na kama utaratibu ambao
tumejaribu kuutolea maelezo kwa kuangalia Ranchi za Mkoa wa Kagera jinsi gani
migogoro iliyopo haimaliziki kutokana na ukweli kwamba wahusika wakuu katika
migogoro hiyo ni watendaji wa Serikali.
Mheshimiwa Spika, Changamoto
kubwa inayoikabili tasnia ya mifugo ni namna ya kufikia viwango vya ubora wa
mifugo na mazao yake vitakavyokidhi mahitaji ya soko la kikanda na kimataifa.
Mheshimiwa Spika,
katika kuonyesha kuwa watendaji wanashindwa kutenganisha kati ya machinjio ya
kisasa na viwanda vya kusindika ni pale, Waziri alipokuwa anajibu swali namba
27 kwa mujibu wa Hansard, “Je, hivi sasa kuna viwanda vingapi vya
nyama na vinasindika kiasi gani cha nyama?” Jibu la Waziri lilikuwa “Mheshimiwa
Spika, Tanzania inahitaji viwanda ama machinjio makubwa takribani 16 yenye
uwezo wa kuzalisha nyama tani 133 kwa siku kwa kila kiwanda au kila machinjio”
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inasisitiza tena ni kwa njia zipi utekelezaji wa Ilani
unaweza kufikiwa kama tafsiri ya kiwanda cha kusindika nyama na machinjio
inaonekana kuwa ni kitu kimoja?
Mheshimiwa Spika, kwa
hali ya kawaida ng’ombe wa asili hutoa maziwa 0.5ltr kwa siku wakati yule wa
kisasa anatoa kati ya lita 7-30ltrs kwa siku kutegemea na matunzo na elimu ya
ufugaji aliyonayo mfugaji. Hivyo basi ili
mfugaji wa ng’ombe za asili aweze kupata lita 30 za maziwa kwa siku atahitaji
kuwa na ng’ombe 15. Mbali na mambo hayo yote ambayo yataenda na uwiano huo
lakini jambo la muhimu kwa mfugaji wa asili ni kwamba madawa yanayohitajika
kwa chanzo, kuosha na kutibu magonjwa ni
zile zile kwa ng’ombe wote wa asili na wa kisasa.
- HUDUMA ZA UGANI
Mheshimiwa Spika, ili
sekta hii ya mifugo iweze kuleta tija inayokusudiwa huduma ya ugani ni muhimu
sana, lakini kwa mtindo wa utendaji kazi kwa watoa huduma hiyo ulivyo ni
dhahiri tija inayotegemewa ni vigumu kupatikana.
Mheshimiwa Spika,
kutokana na watoa huduma kutokuwa na idadi maalum ya wafugaji wanaowahudumia,
eneo maalum na hivyo kuweza kuwajibika kwa matokea yatakayopatikana katika eneo
husika ni tatizo kubwa sana.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaona itakuwa ni vyema kama kila afisa ugani atakuwa
na orodha kamili ya wafugaji anaofanya nao kazi katika eneo maalum, kwani
utaratibu huo utarahisisha upatikanaji wa kumbukumbu sahihi na pia kuweza
kupima utendaji wa afisa huyo.
Kwa
mfano kwa maafisa ugani wanaofanyakazi mkoa wa Kagera ambao ni watumishi wa Serikali (Ndg. Patrick,
Kashankoro, Kanyambo na Mutabazi), hawa wote wanamiliki vitalu vya Ranchi. Hoja
ni je utaratibu wa watendaji wa Serikali kujimilikisha mali za wananchi
unaendelea hata kwenye ngazi ya chini? Na mgongano wa maslahi katika suala hili
unashughulikiwa vipi?
- SEKTA
YA NGOZI
Mheshimiwa Spika, wakati waziri kivuli wa fedha akiwasilisha maoni ya
Kambi ya Upinzani kwenye muswada wa fedha, tarehe 16.08.2012 alisema yafuatayo “Mheshimiwa Spika, katika kifungu cha 12 cha muswada, serikali inatoa pendekezo la kufanyia
marekebisho sheria ya kodi ya mauzo ya nje ya nchi sura 196 kwa kuweka jedwali
jipya ambalo linaongeza viwango vya tozo kwenye ngozi ghafi inayosafirishwa
kwenda nje ya nchi. Kama serikali ina mpango madhubuti wa kuendeleza sekta ya
viwanda nchini na kuleta tija kiuchumi ni dhahiri kuwa inatakiwa kusitisha
uamuzi huu.
Mheshimiwa
Spika, kwenye
hotuba yetu ya bajeti tulipendekeza kuwa serikali izuie kabisa ngozi ghafi
kusafirishwa nje ya nchi na badala yake ijikite kutafuta uwezekano wa kuitumia
ngozi hiyo hapa nchini na kuanzisha viwanda vya kutengeneza bidhaa zitokanazo
na ngozi hiyo. Hata Kamati ya fedha na uchumi ilikuwa na mapendekezo hayahaya.
Hii ni kutokana na manufaa makubwa ya kiuchumi wanayopata wenzetu hasa nchi ya
Ethiopia.
Mheshimiwa
Spika,
hata katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki wenzetu wa Uganda na Rwanda nao
wamezuia ngozi ghafi kuuzwa nje ya nchi. Mapendekezo haya ya serikali yakibaki
kama yalivyo hayataifanya serikali kupata mapato yanayostahili kwa sababu
wafanyabiashara wengi wanatoa takwimu zisizo sahihi kuhusu mauzo halisi
watakayokuwa wanauza nje ya nchi (under invoicing).
Mapato ambayo serikali inahofia kuyapoteza kwa
kupiga marufuku uuzaji wa ngozi ghafi nje ya nchi yatapatikana tena kwa kiasi
kikubwa kutokana na ajira zitakazopatikana katika viwanda vya kusindika ngozi,
kodi ya mapato kama vile PAYE n.k. Ni wakati muafaka sasa tuchukue hatua hii
kwani hata nchi ya Pakistani ambao ndio wanunuzi wa ngozi yetu wamepiga
marufuku kabisa uuzaji wa ngozi ghafi nje ya nchi yao”.
- SEKTA
YA MAZIWA
Mheshimiwa Spika,
Taarifa ya uwezo wa viwanda na hali halisi ilivyo sasa hivi Inayonyesha kuwa
hadi sasa hivi kuna viwanda 35 vyenye uwezo wa kusindika zaidi ya lita 1000 kwa
siku kwa kila kimoja. Kati ya hivyo ni viwanda 28 tu ambavyo vinazalisha hadi
sasa na vingine 7 ama vimefungwa au kusimamisha uzalishaji. Kuna baadhi ya
viwanda vinatumia hadi zaidi ya 80% ya uwezo wake na vingine chini ya 16%. Kwa
vile kuna viwanda visivyozalisha kabisa, wastani wa matumizi ya uwezo wa
kusindika ni 12% tu.
Mheshimiwa Spika,
Uwezo wa jumla wa viwanda vyote ni kusindika, lita 428,500 kwa siku lakini hali
halisi ni kusindika lita 52,330 kwa siku. Hali hii inaonyesha kuwa juhudi kubwa
zinahitajika ili kuwezesha sekta ya viwanda vya maziwa kuwa na uwezo wa
ushindani na kutoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa taifa.
- MATATIZO YANAYOATHIRI USINDIKAJI WA
MAZIWA
Mheshimiwa Spika,
Matatizo yanayovikabili viwanda vya maziwa ni mengi na yanahitaji uchunguzi wa
kina katika kila kiwanda ili kutoa ushauri kwa kila kiwanda husika, lakini
matatizo yaliyotajwa na viwanda vyote ni kama yafuatayo:
- Ukosefu wa
maziwa ya kutosha.
Mheshimiwa Spika,
Ingawa Tanzania inakadiriwa kuzalisha lita 1,400 milioni za maziwa kila mwaka
kiasi cha maziwa yanayopatikana kwa ajili ya kusindika ni kidogo sana. Hali hii
inatokana na maziwa mengi kuzalishwa na wafugaji wa jadi ambayo kiasi kikubwa
kinatumika na wafugaji wenyewe, uzalishaji ni wa msimu na ukusanyaji ni mgumu.
Wafugaji hawa ndio huzalisha 70% ya maziwa yote nchini.
Upungufu
wa maziwa ya kusindika ambao huwa zaidi wakati wa kiangazi unachangiwa na
sababu nyingi ambazo ni:
- Gharama kubwa
na ugumu wa kukusanya maziwa ya wafugaji
waliosambaa maeneo ya mbali
- Ushindani na
wachuuzi wadogo wadogo.
- Faida ndogo
kutokana na matumizi kidogo ya uwezo wa viwanda.
- Uzalishaji wa
msimu ambapo maziwa mengi hupatikana msimu wa mvua na kidogo sana wakati
wa kiangazi na hivyo kushindwa kutosheleza[4]
Mheshimiwa Spika,
katika kuhakikisha kuwa viwanda vya maziwa vilivyopo vinapata maziwa ya
kutosha, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuhakikisha kwamba maziwa yanayozalishwa na wafugaji wadogo au
wa asili yanauzwa kwenye vituo maalum vya kukusanyia maziwa, na pia maziwa
yasiuzwe kwa wanunuzi bila ya kuyasindika. Kufanya hivyo kutaondoa kwanza
matatizo ambayo yanayoweza kutokana na magonjwa ya kuambukizwa kati ya mifugo
na binadamu (zoonotic deseases).
Mheshimiwa Spika,
pia liwe ni jukumu la Halmashauri kulinda soko la maziwa yaliyosindikwa, na kwa
njia hiyo wafugaji wadogo na wale wa asili maziwa yao yatakuwa na uhakika wa
soko badala ya sasa ambapo wakati wa msimu wa mvua maziwa yanakosa soko na
hivyo kumwagwa.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa maziwa kuuzwa moja kwa moja na
wafugaji wadogo na wakubwa ni upotevu wa mapato, hivyo basi Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kuwa, liwe ni jukumu la Halmashauri kutunga kanuni ndogo za kuhakikisha viwanda
vya maziwa vinalindwa kwa kupata maziwa muda wote ili kiwanda kiweze kulipa
kodi kwa halmashauri.
- Matatizo ya
kimfumo na sera
Mheshimiwa Spika,
mbali ya matatizo hayo pia kuna matatizo ya kimfumo na sera. Katika
kundi hili kuna matatizo kama urasimu katika vyombo vya kudhibiti ubora kama
TBS, kuwa na vyombo vingi vya uthibiti, wadau kutoshirikishwa katika maandalizi
ya sera, migogoro kati ya wafugaji na wasindikaji na vyama vya wadau visivyo
imara.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwepo uwajibikaji kwenye vyombo vya udhibiti
na vyombo hivi madhumni yake, yawe ni kuwezesha na siyo kukwamisha.
Inapendekezwa kuwa shughuli zote za udhibiti wa sekta ya maziwa zifanywe na
Bodi ya Maziwa tofauti na sasa ambapo vyombo vingi hufanya hivyo. Aidha, Bodi
ya Maziwa iliyoanzishwa kisheria iwezeshwe kufunya shughuli zake kwa kupewa
rasilimali zinazotakiwa tofauti na sasa ambapo Bodi ipo kwa jina tu.
Mheshimiwa Spika, aidha, wadau washirikishwe katika
utayarishaji wa sera zinazohusu sekta ya maziwa, kwani sasa wanaohusishwa ni
wale wenye viwanda vya maziwa, je wafugaji wa asili wanahusishwa vipi?
- Matatizo mengineyo:
Mheshimiwa Spika,
Haya ni kama kipato kidogo cha wananchi, wawekezaji kuwa na miradi mingi kwa
pamoja, sekta ya maziwa kutokuwa na mvuto kwa wawekezaji, ukosefu wa vyombo vya
mikopo ya muda mrefu na riba ndogo na kutokuwa na maeneo maalum yenye
miundombinu ya kutosha ya kujenga viwanda.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi Upinzani inaitaka pia Serkali itafute njia ya kuimarisha vyama vya
kitaifa vya wadau (TAMPA, TAMPRODA) ili viwe kweli vya kitaifa na vyenye uwezo
wa kushirkiana na Serikali kundeleza sekta.
Mheshimiwa Spika,
nguzo ya 7 aya ya 7.2.3 ya kilimo kwanza
inayosema kwamba “Kuainisha na kuimarisha uwezo unaohitajika
kwa kuendeleza sekta ya mifugo- Kwa
mwaka 2010 serikali pamoja na TPSF
ilitakiwa Kukarabati viwanda vyote vya maziwa vilivyopo nchini na kuanzisha
vituo vya kukusanyia maziwa”. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
kulieleza Bunge na wadau kwenye sekta hii ya maziwa utekelezaji wa nguzo hii ya
Kilimo kwanza imetimizwa kwa kiasi gani?
Mheshimiwa Spika, kwa
mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano inaonyesha ili sekta ya Mifugo
iweze kuleta tija tarajiwa ilitakiwa kwa mwaka wa fedha 2013/14 ipewe shilingi
bilioni 275.98 kama fedha za maendeleo. Lakini kwa masikitiko makubwa mwaka huu
wa fedha Wizara imetengewa jumla ya shilingi bilioni 8.97. Kambi Rasmi
ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge ni kwanini imeshindwa kutekeleza
matakwa ya mpango wa maendeleo ambao ulipitishwa na Bunge?
- SEKTA
YA UVUVI
Mheshimiwa Spika,
Tanzania inamiliki maeneo makubwa ya maji ambamo rasilimali za uvuvi hupatikana
kwa wingi. Maeneo hayo ni pamoja na Ziwa Vctoria, Ziwa Tanganyika Ziwa Nyasa,
Mabwawa
(Nyumba
ya Mungu, Mtera na mengine mengi ya asili), mito (Rufiji, Ruvu, Kilombero
n.k.), malambo na maeneo oevu ambayo yana fursa kubwa ya uvuvi hapa nchini.
Aidha, kuna Bahari ya Hindi ambayo ina maeneo mawili ya Bahari ya Taifa
(Territorial Sea) na Ukanda wa Uchumi wa Bahari (Exclusive Economic Zone -
EEZ).
Sekta
ya uvuvi inatoa mchango mkubwa katika kuwapatia wanachi ajira, lishe, kipato,
na kuingizia nchi fedha za kigeni. Uvuvi nchini huendeshwa na wavuvi wadogo
takriban 200,000 ambao huvua asilimia zaidi ya 90 ya samaki wote wanaovuliwa
nchini. Zaidi ya wananchi 4,000,000 hujishughulisha na kujikimu kutokana na
shughuli zinazoendana na uvuvi hapa nchini.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na uharibifu uliopo katika uvuvi umesababisha kuwepo kwa upungufu
mkubwa wa rasilimali ya uvuvi, hususan katika Ziwa Victoria ambalo huongoza kwa
upatikanaji wa samaki aina ya Sangara ambao wamepungua kutoka tani 676,000
mwaka 2006 hadi tani 331,000 mwaka 2009. Hali hii imetokana na sababu
zifuatazo:-
- Ongezeko la
kasi ya matumizi ya zana haramu pamoja na ongezeko la idadi ya wavuvi
kutoka 92,529 mwaka 2000 hadi 105,016 mwaka 2008;
- Ongezeko la
vyombo vya kuvulia samaki kutoka vyombo 30,171 (2000) hadi vyombo 52,174
(2008); na
- Ongezeko kubwa
la mahitaji ya samaki na mazao yake katika soko la samaki ndani na nje ya
nchi na hivyo kuwa kichocheo kikubwa cha samaki wachanga kuvuliwa. Kwa
upande wa Bahari ya Hindi, mathalani rasilimali ya kambamiti imepungua
kiasi cha kusababisha uvuvi wake kwa meli kubwa kufungwa hadi sasa. Aidha,
rasilimali ya Kambamiti (Prawns) imepungua kutoka tani 1,320 kwa mwaka
2003 hadi kufikia tani 205 mwaka 2007[5].
Mheshimiwa Spika, pamoja
na uwepo wa ongezeko la mahitaji ya samaki na mazao yake katika soko, wavuvi
wamekuwa wakiilalamikia Serikali kuwa inakwamisha au kuwahujumu kwa uchomaji wa nyavu za wavuvi ambao hata
hawaelewi ni kwanini wanauziwa nyavu zisizostahili kwa mujibu wa Watendaji.
Lakini ukweli ni kuwa nyavu zote kustahili au kutostahili inategemea unavua
samaki wa aina gani na nyavu hizo zinatumika namna gani, hivyo basi kitendo cha
kuchoma nyavu (Zana za uvuvi) za wavuvi bila ya kuhakiki matumizi yake na bila
ya kutoa nyavu (zana mbadala) ni hujuma kwa sekta hii ya uvuvi na wavuvi
wenyewe. Kumekuwepo na tabia ya kufunga ziwa au kusitisha shughuli za uvuvi
kiholela, bila taarifa au sababu za kisayansi zinazotolewa kwa wavuvi.
Mheshimiwa Spika, Mfano
wa tabia hii yenye kujenga hisia ya chuki za wananchi kwa Serikali yao ni Ziwa
Basotu. Hili ziwa limeingizwa kwenye mitego, chambo na chuki/ulipazaji visasi
vya kisiasa tu kumewekupo na shinikizo la ulipazaji kisasi ya kisiasa kwa
kufungiwa ziwa mara kwa mara ili wataabike, wasipate kitoweo na kipato na
kuvuruga mfumo wao wa maisha ya kila siku lakini sio ukweli wa hali halisi kuwa
kuna uvuvi usiofaa. Je, haya ndo mandeleo ya sekta ya uvuvi? Hivi jambo la
kisayansi linaendeshwaje kisiasa? Nadhani haya si maendeleo tuliyotarajia kwa
mujibu wa ilani za CCM za mwaka 2005-10 na 2010-15 bali ni hujuma na upandikizwaji wa mbegu mbaya za
chuki ya kisiasa tu.
Kambi
Rasmi ya Upinzani inamtaka Waziri awaeleze wananchi wa BASOTU kwanza ni nani
mwenye mamlaka ya kusitisha uvuvi katika ziwa na hatua zipi ambazo pia
zinashirikisha wadau zinapaswa kufuatwa?
a. UFUGAJI WA SAMAKI
Mheshimiwa Spika, shughuli za ufugaji wa samaki unafanywa na
wafugaji wadogo. Hata hivyo, ufugaji wa samaki lazima ishindane na shughuli
zingine za vijijini kwa eneo la ardhi, maji, nguvu kazi na vyakula. Hali hii
hupelekea umuhimu wa kutathmini gharama na faida ya ufugaji samaki na mchango
wake kwa maisha ya wakazi wa vijijini kulingana na shughuli zao zingine.
Mheshimiwa Spika, zaidi ya hayo, ufugaji wa samaki hukabiliwa na
matatizo na changamoto zingine kama ukosefu wa sera thabiti ya ufugaji samaki;
mabadiliko katika sera za uchumi; ukosefu wa teknolojia bora; upungufu wa
vifaranga bora; miundombinu duni ya usafiri; utafiti usiokidhi mahitaji;
ukosefu wa takwimu za uzalishaji; upungufu wa taarifa sahihi za utunzaji wa
bwawa la samaki.
Mheshimiwa Spika, ili kuwa na uwezo wa kufanya shughuli kwa
mafanikio, ni muhimu kuwa na takwimu ya utendaji na shughuli husika. Vivyo
hivyo, ili kuendesha shughuli za ufugaji samaki kibiashara, mfugaji analazimika
kuchukua na kutunza takwimu kwa hatua zote au shughuli yoyote anayoifanya
ikiwemo ya kutunza matumizi na mapato ya fedha.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka
mitano, sekta ya Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2013/2014 ilitakiwa itengewe jumla ya
shilingi bilioni 60.896 ili sekta nzima
ya uvuvi iweze kuleta tija stahili pamoja na faida zingine ni kwamba kama uwekezaji
kwa mujibu wa mpango hadi 2015. Makusanyo ya Serikali kwa mwaka katika sekta
hii yalitakiwa kukua kutoka shilingi bilioni 6.58 hadi shilingi bilioni 12.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka
Serikali iwaeleze watanzania ni kwanini Serikali imekinzana na mpango wa Maendeleo
ambao ulipitishwa na Bunge?
- MAPITIO
YA BAJETI YA UTEKELEZAJI KWA WIZARA
Mheshimiwa Spika, Ukiangalia mwenendo wa bajeti ya wizara kwa miaka
minne inaonyesha kuwa bajeti ambayo imekuwa ikitolewa kwa wizara hii imekuwa
ikishuka, mwaka wa fedha 2010/2011 zilitengwa shilingi bilioni 58.8, mwaka
2011/2012 zilitengwa shilingi bilioni 57.2, mwaka wa fedha 2012/2013 zilitengwa
shilingi bilioni 54.6 na kwa mwaka huu wa fedha 2013/2014 zimetengwa shilingi
bilioni 47.18
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa tafsiri ya
kupungua huko kwamba ni fundisho kwa watendaji wizara kuangalia fursa za mapato
ambazo zipo katika wizara hiyo zifanyiwe kazi na ziweze kuwekezwa kwa maendeleo
ya sekta hizi mbili-(Mifugo na Uvuvi), na kwamba kutokana na ukweli ulipo wa fursa
hizo wizara imelala na hata kusimamia sheria na kanuni zilizopo za kuhakikisha
mirabaha ya uvuvi inalipwa imeshindwa na wajanja wanavuna raslimali yetu bila
nguvu yoyote ya ziada.
- HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na
CHADEMA inasema kwamba, wizara hii kwa kipindi kirefu imekuwa kama nyumba
isiyokuwa na msimamizi kiasi kwamba raslimali za nchi hii zimekuwa zikigawiwa,
zikivunwa na kutumiwa bila kufuatwa kwa sheria na kanuni, mfano mmojawapo ni
ugawaji wa mashamba ya Ranchi za Taifa na kilichofuata ni nchi kuingia kwenye
migogoro mikubwa kati ya wafugaji na wakulima.
Mheshimiwa Spika, katika kuonyesha kuwa Serikali imeshindwa
kuthamini sekta ya mifugo kwa ujumla, mwaka 1981, Morogoro Muasisi wa nchi hii
Mwalimu J.K Nyerere alisema “tumetenga, kwa mfano, maeneo maalum kwa ajili ya
mazao kama pamba, kahawa, tumbaku na katani lakini hatujatenga maeneo kama hayo
kwa ajili ya mifugo.Tumetenga maeneo maalum kwa ajili ya pundamilia (hifadhi za
taifa) lakini wafugaji wananing’inia hewani tu”.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaona kama kungekuwa
na umakini katika serikali hii ya CCM ni dhahiri kuwa makosa ambayo yalikuwa
yametendeka huko nyuma ulikuwa ni muda mwafaka wa kurekebisha makosa katika
sekta hii ya mifugo na hivyo yanayopelekea wafugaji kuwa wahamiaji au watu
wasiohitajika katika nchi yao kama ilivyo sasa.
Mheshimiwa Spika, mwisho lakini kwa umuhimu mkubwa ni shukrani kwa
wanachama na wapenzi wote wa Wilaya ya Maswa kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa
katika kujenga na kuimarisha chama chetu.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.
………………………………………..
Slyvester Mhoja Kasulumbayi (Mb)
Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani-
Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
31.05.2013
No comments:
Post a Comment