1.0 UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
katika hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika bajeti
ya wizara hii mwaka 2012/13, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na
CHADEMA ilibaini mapungufu mengi ya kiutendaji na kiuwajibikaji katika wizara
hii, na hivyo kuitaka Serikali kufanya
mambo yafuatayo ili kuboresha utendaji na ufanisi:
1. Kuziwezesha
balozi zetu nje kwa kuzitengea fedha za kutosha
ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi
2. Kutoa
idadi ya majengo ya balozi zetu nje (nyumba za mabalozi, nyumba za maafisa wa balozi
na ofisi za balozi) kwa mchanganuo wa idadi ya nyumba katika nchi na kama
nyumba hizo zina hati miliki au la.
3. Kutoa
taarifa ya namna kila ubalozi ulivyotekeleza sera ya Diplomasia ya uchumi kwa
kuzingatia kwamba balozi nyingi ziko hoi kifedha kiasi cha kwamba waambata wa
kiuchumi wanakosa fedha za kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa ajili
ya upelelezi wa masuala ya kiuchumi.
4. Kulikarabati
jengo la ubalozi wa Tanzania huko Msumbiji lililokuwa limechakaa kwa
kutofanyiwa ukarabati tangu 1975 ingawa jengo hilo tulipewa bure na Serikali ya
Msumbiji chini ya FRELIMO.
5. Kujenga
kitega uchumi katika kiwanja cha
Tanzania kilichopo Dubai na kukiendeleza kiwanja namba 19 tulichopewa bure na Serikali ya Uingereza
kilichopo Uingereza (Central London) ambavyo vimekuwa maficho ya wezi kwa
kutoendelezwa kwa muda mrefu na kusababisha Serikali za nchi hizo kutaka
kutaifisha viwanja hivyo.
6. Kufanya
uchunguzi kuhusu tuhuma za balozi zetu nchini China, na Uingereza kutoa hati za
kusafiria kwa mataifa mengine hasa ya Afrika Magharibi ili kubaini ukweli na
kuliondolea taifa aibu kutokana na tuhuma hizi.
7. Kukarabati
jengo la ubalozi wetu nchini China ambalo lilikuwa na nyufa na kuvuja nyakati
za mvua, na kununua samani na vifaa vya
ofisi kama mashine za nukushi na za kurudufu ambazo zilikuwa hazipo,
8. Kununua
magari mapya ya ofisi ya ubalozi wetu nchini China kwa kuwa magari matatu yaliyokuwepoyalikuwa
yameshapitiliza muda wa miaka 10 ambao kwa mujibu wa sheria za China hayapaswi
kutumika tena,
9. Kupeleka
mwambata wa kiuchumi (economic attaché)
nchini China ili kufuatilia fursa mbalimbali za kiuchumi katika
kutekeleza diplomasia ya uchumi kutokana na mahusiano makubwa ya
kibiashara kati ya nchi yetu na China
10. Kuwawekea
zuio wahusika wa kashfa ya rada kuwa viongozi wa shughuli za kiserekali ili
walau kuonesha uwajibikaji wa kimaadili (moral accountability) baada ya
kushindwa kuwawajibisha kisheria, ili kuondoa dhana iliyojengeka miongoni mwa
jamii kwamba dola imetekwa na mafisadi.
11. Kuchunguza
na kuwachukulia hatua watanzania (wafanyabiashara na wanasiasa) waliotorosha
kiasi kikubwa cha fedha za nchi yetu (zaidi ya shilingi bilioni 315) na
kuzificha katika mabenki ya uswisi
12. Kutoa
mchanganuo wa jinsi fedha za rushwa ya rada (chenji ya rada) zilivyotumika
13. Kueleza
bayana faida za kiuchumi tunazopata kama taifa kwa kushirikiana na jumuiya
mbalimbali za kimataifa ili kuthibitisha kwamba mashirikiano hayo hayatumiki
kupora rasilimali za nchi yetu kwa hila ya “uwekezaji”
Mheshimiwa Spika,
kabla sijajielekeza kwenye mambo mahsusi kwa kipindi hiki cha bajeti ya
2013/2014, napenda kuchukua nafasi hii kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inayoongozwa na CHADEMA, kuitaka Serikali kutoa majibu mbele ya Bunge
hili tukufu, kwamba imetekeleza kwa kiwango gani masuala yaliyoorodheshwa hapo
juu, tuliyoitaka iyatekeleze (moja baada ya jingine) kwa mwaka wa fedha
unaomalizika wa 2012/2013?
Bonyeza Read More Kuendelea
1.1
Upotevu wa Fedha za Safari za Rais,
Shilingi bilioni 3.5
Mheshimiwa
Spika, katika hotuba yangu ya mwaka 2012/2013 nilihoji
kuhusu serikali Kuchunguza na kuchukua hatua kwa waliohusika na upotevu wa
shilingi bilioni 3.5 kwa ajili ya safari “hewa” za Rais nje ya nchi, ili waweze
kubainika na kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria zetu.
Mheshimiwa
Spika, fedha hizi ni nyingi sana na hasa ikikukumbukwa kuwa mwaka jana 2012 wapo
mawaziri ambao walichukuliwa hatua na Bunge hili kutokana na upotevu ama
madhaifu yaliyofanyika kwenye wizara zao, wapo ambao walihukumiwa kutokana na
kupotea kwa Twiga kwenye wizara zao, wapo waliohukumiwa kutokana na udhaifu
katika kusimamia wizara zao na taasisi zilizoko chini yao. Kambi rasmi ya upinzani, inahoji iweje leo waziri aliyeshindwa
kusimamia wizara yake na kusababisha upotevu wa fedha hizi mpaka leo bado yupo,
wakati wapo mawaziri wengine walioshughulikiwa kutokana na udhaifu walioonyesha
kwenye kusimamia wizara zao, au ndio kusema kuwa Serikali hii ya CCM inafanya
upendeleo na kuonea baadhi ya mawaziri na kuwaacha wengine? “This
clearly indicates the “double standard” nature of this Government in the
performance of its functions”
1.2.
Kuanzishwa kwa Ubalozi Mdogo Guangzhou -China
Mheshimiwa
Spika, mwaka jana Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilipendekeza kuwa serikali ianzishe
ubalozi mdogo katika Jiji la Guangzhou kwa ajili ya kurahisisha biashara kati
ya wafanyabiashara wa Tanzania na wale wa China. Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inatambua kuwa serikali
imelifanyia kazi wazo hili na imeamua kuanzisha ubalozi mdogo katika mji huo
,ila tunataka kujua ni lini ubalozi huu utazinduliwa rasmi, kupata watendaji na
vitendea kazi ili uweze kuanza kufanya kazi .
2.0 DIPLOMASIA YA UCHUMI
Mheshimiwa Spika, moja
ya matarajio ya ushirikiano wa kimataifa ni kuweza kutafuta, na kunufaika na
fursa mbalimbali za kiuchumi zinazoweza kupatikana katika mashirikiano hayo ili
kama Taifa, tuweze kujikwamua kiuchumi na kujitegemea.
Mheshimiwa Spika,
kinyume na matarajio hayo mazuri, sasa nchi yetu imegeuzwa kuwa kitega uchumi
cha nchi zilizoendelea kwa kisingizio cha “ushirikiano wa kimataifa” chini ya
mwavuli wa “uwekezaji”. Matokeo ya
ushirikiano huu wa kinyonyaji (exploitative relationship) ni kwamba kiwango cha
umasikini katika nchi yetu kimeongezeka na hivyo kuifanya nchi yetu kuwa
tegemezi zaidi kuliko ilivyokuwa hapo kabla.
Mheshimiwa Spika, Hayati
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikerwa na unyonyaji na unyanyasaji uliokuwa
ukifanywa na wakoloni, hali iliyompelekea kusema maneno yafuatayo:
“Tumeonewa kiasi cha kutosha,
tumenyonywa kiasi cha kutosha, tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu ndiyo
uliotufanya tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa. Sasa tunataka kufanya mapinduzi”
Mheshimiwa Spika, baada
uhuru, Mwalimu akaanzisha siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Ujamaa ulilenga kujenga
umoja wa kitaifa na umoja wa bara la
Afrika dhidi ya unyonyaji wa kibeberu, wakati kujitegemea kulimaanisha kujenga uchumi endelevu ili kulijengea taifa
heshima na nguvu ya maamuzi mbele ya mataifa mengine, na kuliepusha taifa na
fedheha ya kuombaomba.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani imesikitishwa sana na
kitendo cha Serikali kulidanganya taifa, kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2010
kwamba: “Katika kipindi cha miaka mitano 2010 -2015, Serikali ya Chama cha
Mapinduzi itatekeleza Sera ya Diplomasia ya Uchumi” wakati Ibara ya 98 (i) ya Ilani
hiyohiyo ya CCM inasema kwamba Serikali ya CCM itaendelea kushinikiza nchi
tajiri kutekeleza ahadi yao ya kutenga asilimia 0.7 ya pato la taifa la nchi
zao kwa ajili ya misaada kwa nchi masikini”.
Mheshimiwa Spika,
ikumbukwe kwamba ahadi hii ya asilimia 0.7 ya pato la taifa la nchi tajiri
ambayo Serikali ya CCM inakodolea macho ni fedha za walipa kodi wa nchi hizo
kama ambavyo wananchi wetu wanavyolipa kodi. Aidha ni aibu kwa Serikali hii ya
CCM kuchukua ahadi za wahisani na kuziweka kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM kama
ahadi kwa wananchi ili kubembelezea kura.
Mheshimiwa Spika,
kutokana na uvivu wa kufikiri na kubuni mbinu za kuikwamua nchi hii na
umasikini, Serikali hii ya CCM sasa hivi imeachana kabisa na sera ya
kujitegemea, ambayo Mwalimu kupitia
Azimio la Arusha alisema kwamba “ … Hakika ni ujinga na upumbavu zaidi kwetu
sisi, kufikiri kwamba tutaondokana na
umasikini wetu kwa misaada ya fedha kutoka nje kuliko rasilimali zetu wenyewe”
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza bunge hili, kama
inatekeleza Diplomasia ya Uchumi kwa kutegemea ahadi ya misaada ya fedha kutoka
kwa wahisani na kama hilo ndio suluhisho la matatizo yanayokumba uchumi wetu
kama taifa kwamba tutaweza kuendelea kwa kutegemea hisani na fadhila za
wafadhili huku tukishindwa kuzitumia rasilimali zetu kwa ajili ya kujikomboa
kiuchumi.
Aidha,
Kambi Rasmi ya Upinzani imejiridhisha kwamba kauli mbiu ya ‘Diplomasia ya Uchumi’ imeendelea kubakia kama ilivyo kauli
mbiu ya ‘Kilimo Kwanza’ ambayo
imebakia kutamkwa na viongozi bila kuwa na mkakati wa utekelezaji wala vigezo
vya kupima kiwango cha utekelezaji wake.
3.0. VYAMA VYA SIASA NA MISAADA KUTOKA NJE YA
NCHI.
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa ‘United Nations University’(UNU-WIDER) ya mwezi Aprili 2012
iliyoandaliwa na Aili Mari Tripp
ilionyesha kuwa misaada ya wahisani kutoka nje katika mabadiliko ya kisiasa
Tanzania ‘Donor Assistance and Political Reform in Tanzania’, inaonyesha kuwa Tanzania imepokea misaada
kutoka nje yenye thamani ya dola za
kimarekani bilioni 26.85 toka mwaka
1990-2010.
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa ripoti hiyo ni kuwa Tanzania ni nchi inayoongoza kusini mwa
jangwa la Sahara kwa kupokea misaada mingi kutoka nje ya nchi na hasa kutoka
mataifa ya Ulaya na taasisi za nchi za Uingereza, Marekani, Ujerumani, Uholanzi,
Norway, Canada, Sweden, na taasisi kama Benki ya Dunia, IMF ,UNDP ,UNICEF na
mengineyo. Pamoja na misaada yote hiyo, bado tumeendelea kuwa nchi maskini sana
duniani pamoja na kuwa na rasilimali lukuki ambazo tumepewa na Mungu ila
tunashindwa kuzitumia kwa manufaa ya watanzania na badala yake tumeendelea
kudanganywa na vimisaada vidogo vidogo na kubadilishana na rasilimali zetu kama madini, misitu ,wanyama nk kwa ajili ya
misaada hiyo.
Mheshimiwa Spika,
pamoja na misaada hiyo kwa serikali hii ya CCM bado vyama vya siasa vimekuwa na mahusiano na
baadhi ya vyama vingine vya siasa katika mataifa ya magharibi na vimekuwa
vikipokea misaada ya aina mbalimbali kama fedha , nyenzo na mengineyo kadiri ya
makubaliano na mirengo ya kiitikadi ya vyama husika.Pamoja na ukweli huo bado
vipo vyama vya siasa vinavyopotosha umma kuhusiana na misaada vinayopokea
kutoka nje ya nchi na vyama hivi vimekuwa mstari wa mbele kueneza propaganda za
uongo kuwa vyenyewe havipokei misaada kutoka nchi za magharibi.
Mheshimiwa Spika,
CCM wao ‘wanajiita’ kuwa wapo mrengo wa kijamaa/kikomunisti na wamekuwa
wakipokea misaada mingi sana ya fedha na nyenzo kutoka Umoja wa Vyama vya Kikomunisti
Ulimwenguni ‘Socialist International’ kutoka katika nchi kama za
Ujerumani kupitia SDP ,Uingereza kupitia chama cha Labour,China kupitia chama
cha Kikomunist ,Marekani kupitia chama cha Democrats. Pamoja na misaada ya
kifedha na kiufundi ambayo CCM imekuwa ikipata kutoka nje wamekuwa hawatangazi
hadharani hata mara moja kuhusiana na kiasi ambacho wamekuwa wakipokea na hivyo
kila kitu kwao imekuwa ni siri kuu ya viongozi wao.
Mheshimiwa Spika,
kwa upande wa chama cha CUF, kutokana na itikadi zake za mrengo wa Kiliberali
ambazo miongoni mwa misingi yake mikuu ni pamoja na “kupigania haki za ndoa ya jinsia
moja, usagaji na ushoga”. Hii ni kwa mujibu wa tangazo lao kwenye
mtandao wao wa umoja wa maliberali ulimwenguni, likiungwa mkono na Waziri wa
Haki na Usawa wa Uingereza, Lynn Featherstone kutoka chama cha
Liberal Democrats wakati chama hicho(www.liberal-international.org) kilipokuwa kinapitisha azimio la kuruhusu
ndoa za jinsia moja kama haki ya mtu mmoja mmoja, wanashirikiana na vyama kama vile LPC ya
Canada, Det Radikale Venstre cha Norway, FDP cha Ujerumani, Israel Liberal
Group cha Israel,PDS cha Senegal na Liberal Democrats cha Uingereza.
Kutokana
na umoja huo, CUF wamekuwa wakipata msaada wa kifedha na nyenzo nyingine
mbalimbali kutoka kwa vyama hivyo vya mrengo wa Kiliberali na msaada wa mwisho
ni hivi majuzi mwezi Machi 2013 waliposaini makubaliano na chama cha Kiliberali
kutoka Norway.
Mheshimiwa Spika,
kwa upande wa CHADEMA, wapo kwenye Umoja wa Vyama vya Kidemokrasia
Ulimwenguni (International Democratic Union - IDU). Huu ni umoja wa
vyama ambavyo vipo kwenye mrengo wa kati na ambavyo msingi wake mkuu ni pamoja na kuwa na familia, kama taasisi
muhimu katika jamii, ikimaanisha kwamba: “tunapinga
vitendo vyote vya ushoga na usagaji”. Tunatetea demokrasia, haki za binadamu na kupambana na
ufisadi katika serikali. Vyama wanachama wa umoja huu ni pamoja na Conservative
Party cha UK, CPP cha Norway, Republican cha Marekani na vingine
vinavyofuata mrengo huo.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya
upinzani Bungeni, inavitaka vyama vyote ambavyo vimekuwa
na mahusiano na vyama vya nje viweke wazi mikataba yao na malengo ya mahusiano
hayo ikiwa ni pamoja na misaada ambayo vimekuwa vikipokea kutoka kwenye nchi
hizo .
4.0 MPANGO WA KUJITATHIMINI
KIUTAWALA BORA (APRM)
Mheshimiwa Spika,
itakumbukwa kuwa mnamo mwezi Januari, 2013 ulifanyika mkutano wa 20 wa wakuu wa
Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa ,Ethiopia na ni katika
mkutano huo Mhe. Rais Kikwete aliwasilisha taarifa ya nchi yetu kuhusu
kujitathimini katika utawala bora kwenye mpango wa nchi zinazojitathimini
katika utawala bora (APRM).
Mheshimiwa Spika,
baada ya taarifa hiyo (randama uk.15) nchi yetu ilitakiwa kutafutia ufumbuzi
changamoto zifuatazo;
i.
Migogoro baina ya wakulima na wafugaji
ii.
Imani za kishirikiana (uchawi)
iii.
Kuhakikisha kuwa manufaa ya kukua kwa
uchumi yanawafikia wananchi
iv.
Kutoa elimu kwa umma kuhusu mipango na
sera za serikali
Mheshimiwa Spika,
changamoto hizi ambazo nyingine zinatia aibu taifa letu mbele ya mataifa
mengine kama vile sisi kuonekana ni wachawi na hivyo kutakiwa kuchukua hatua
dhidi ya uchawi !ni fedheha na aibu kubwa kwa taifa letu .
Aidha
, Kambi rasmi ya upinzani Bungeni inataka kujua serikali na wizara imechukua
hatua gani mpaka sasa katika kukabiliana na changamoto hizi na hasa tatizo la
wakulima na wafugaji na kuhakikisha kuwa manufaa ya kukua kwa uchumi wetu
yanawanufaisha wananchi na sio kuwanufaisha baadhi ya viongozi na mafisadi
wachache.
5.0 MLIPUKO WA BOMU ARUSHA NA
BARAZA LA USALAMA LA UMOJA WA MATAIFA.
Mheshimiwa Spika,
mwaka huu tarehe 05 Mei, Kanisa
Katoliki Parokia ya Olasiti huko Arusha
lililipuliwa kwa bomu. Tukio hili lilitokea wakati akiwepo balozi wa
Vatican Nchini na ambaye ndio alikuwa mgeni wa heshima kwenye tukio la kuzindua
Parokia hiyo.
Mheshimiwa Spika,
mara baada ya tukio hilo, Balozi wa Vatican nchini aliwasilisha taarifa hiyo
kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuonyesha kuwa Tanzania sio
nchi salama sana kutembelewa na wageni na kama wakitembelea basi wanapaswa
kuchukua tahadhari kubwa kwa kipindi chote watakapokuwa hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, inataka kujua nini kauli ya serikali
kuhusiana na tukio hili na hasa kuhusiana na taarifa za hali ya usalama wa nchi
yetu na wageni zilizowasilishwa kwenye Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa .
6.0 SAFARI ZA VIONGOZI NJE NA
MISAFARA MIKUBWA
Mheshimiwa Spika,
tangu mwaka 2011/2012 Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikihoji suala la
misafara ya Viongozi wa kitaifa kuwa mikubwa kutokana na kuambatana na watu
wengi ambao wengine wanakuwa hawana hata majukumu ya msingi ya kufanya wakati wa ziara hizo huku
wakiliongezea taifa gharama kubwa ya kuwasafirisha na na kulipia malazi yao na
starehe zao.
Aidha
, tumekuwa tukipendekeza na kushauri kuwa sasa ni wakati muafaka kwa Rais wa
nchi kuamua kutuma wasaidizi wake kwenye baadhi ya ziara za nje kama wanavyofanya
viongozi wengine wa nchi jirani kama Rais Kagame wa Rwanda na hata Mwai Kibaki, Rais mstaafu wa Kenya alivyokuwa anafanya
akiwa Rais, kwani kwa kufanya hivyo
atapunguza msururu wa maafisa na viongozi mbalimbali wa kuambatana naye.
Tunashauri tena kuwa rais awe anatuma wasaidizi wake kwenye ziara za kawaida na
yeye awe na jukumu la kushiriki kwenye ziara rasmi za kiserikali ‘State
Visits’ na mikutano maalum ya Kimataifa kama UN na AU.
Hivyo
basi Kambi rasmi ya Upinzani inashauri mambo yafuatayo yafanyike ili kupunguza
gharama hizi kubwa za kuwasafirisha viongozi na misafara isiyokuwa na tija kama
ifuatavyo;
i.
Serikali itengeneze kanuni za kuthibiti
idadi ya maafisa na watu ambao watakuwa wakiambatana na Rais kwenye ziara za
nje (idadi ya wajumbe kwenye misafara iwe wazi na ijulikane)
ii.
Pawepo na kanuni za kuainisha kuwa ni
nani watapaswa kupanda ndege daraja la kwanza na wale wenye haki ya kulala
kwenye hoteli za daraja la kwanza wajulikane.
6.1. Idara ya Protocol na Mabilioni ya Fedha za
Safari za Nje.
Mheshimiwa Spika, katika
mwaka wa fedha 2011/2012 fungu 221100 ‘travel out of country’zilitumika
shilingi 36,121,942,870.00 kwa ajili
ya safari za nje ya nchi kwa viongozi wakuu. Katika mwaka wa fedha uliopita wa
2012/2013 kifungu 1010 ambacho ni kwa ajili ya protocol walitengewa shilingi 8,372,581,824 na fedha ambazo zilikuwa
zimepokelewa na wizara mpaka mwezi Februari 2013 zilikuwa jumla ya shilingi 26,081,860,727.16! (randama uk.4)jedwali
la 2 na zilitumika kwa ajili ya kugharamia safari za viongozi nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika,
katika mwaka wa fedha 2012/2013 Bunge lilikuwa limetenga na kuidhinisha kiasi
cha shilingi 8,372,581,824 kwa ajili
ya kifungu hiki cha Protocol ‘travel out of Country’kwa mujibu wa kitabu cha
matumizi ya kawaida juzuu ya pili (volume II). Jambo la kushangaza ni kwamba, wizara iliieleza kamati na Bunge hili kuwa
walishatumia zaidi ya bilioni 26.081 kutokana na fedha walizokuwa wamejitengea
wenyewe wizara ambazo hazikuidhinishwa na Bunge kiasi cha bilioni 29.404
Mheshimiwa Spika, Kambi
rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA, inataka maelezo ya kina kuhusiana na mamlaka ya wizara hii kwenda
kutenga na kutumia fedha nyingi kuliko zilizokuwa zimeidhinishwa na Bunge hili
na zilikuwa fedha kwa ajili ya safari za kwenda nje ya nchi, ni nani aliipa
wizara mamlaka hiyo na kiburi hicho kiasi cha kupuuza maamuzi ya Bunge hili
tukufu.
Mheshimiwa Spika,
katika mwaka huu wa fedha 2013/2014 kitengo hiki cha Protocol kimetengewa jumla
ya shilingi 15,155,377,400.00 kwa
ajili ya matumizi mengineyo ,ambazo
katika mchanganuo wake kwenye kifungu 1010 kifungu kidogo cha 221100 ‘travel
out of Country’ zimetengwa shilingi 9,381,328,850.00
kwa ajili ya kugharamia safari za kikazi za viongozi wa Kitaifa nje ya nchi.
Aidha,
katika kifungu kidogo cha 220700 ‘rental expenses’ zimeombwa jumla ya shilingi 2,925,445,000.00 kwa ajili ya kukodisha
ndege ,magari na kumbi za mikutano kwa ajili ya viongozi wa kitaifa.
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni, haikubaliani
na kamwe haitakubaliana na ufujaji huu wa fedha za walipakodi maskini wa
Tanzania . Tunamtaka waziri atoe maelezo ya kina kwa watanzania ni kwanini nchi
maskini kama yetu tutumie fedha nyingi kiasi hicho kwa ajili ya safari za viongozi
nje ya nchi? Aidha , hatukubaliani na kitendo cha kutenga fedha kwa ajili ya
kukodi ndege wakati Rais ana ndege yake ambayo ilinunuliwa na
mabilioni ya fedha za watanzania. Ikumbukwe kwamba ndege hii ya Rais
ilinunuliwa kwa mbwembwe nyingi kiasi kwamba Waziri wa Fedha wa wakati huo
Ndugu Bazili Mramba alisema watanzania wafunge mkanda, hata kama watakula
majani, lazima ndege ya Rais inunuliwe. Watanzania hawa wamekula majani sasa
kiasi cha kutosha, bado tena Serikali inaendelea kuwanyonya ili ipate pesa za
kukodisha ndege wakati Rais ana ndege? Hivi Serikali sasa inataka watanzania
wale mawe ndio ijue kwamba watu wamefunga mkanda kiasi cha kutosha?
6.2 Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje
Mheshimiwa Spika,
mwaka 2012 Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje Ulinzi na Usalama,
ilifanya ziara kwenye balozi takribani zote na iliona matatizo yanayozikumba
balozi zetu huko na ilikuwa matumaini yetu kuwa baada, ya ziara ile ya kamati ingehakikisha kuwa fedha zinaongezwa kwenye
wizara hii na hasa kwenye fungu la maendeleo ili tuweze kuboresha mazingira ya
balozi zetu. Kinyume na matumaini hayo, ni kwamba hakuna jitihada zilizofanyika
kuongoeza bajeti ya wizara hasa katika fedha za maeendeleo.
Mheshimimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, inaitaka kamati ya Bunge ya Ulinzi na usalama,
kuishinikiza Serikali ili kuhakikisha
kuwa katika mwaka huu wa fedha wizara hii inaongezewa fedha kwa ajili ya
kuboresha mazingira ya balozi zetu , na hiyo ndio njia pekee ya kuonyesha kuwa
kamati haikuenda kufanya utalii bali ilienda kuona matatizo ya balozi zetu na
kuchukua hatua.
7.0 UFISADI KATIKA UNUNUZI WA JENGO
LA OFISI NA MAKAZI KATIKA UBALOZI WA TANZANIA JIJINI PARIS – UFARANSA.
Mheshimiwa Spika,
katika mwaka huu wa fedha kwa mujibu wa randama ya wizara ni kuwa mwaka huu wa
fedha kiasi cha shilingi bilioni 28
(28,000,000,000.00) zimepangwa kwa
ajili ya matumizi ya maendeleo na kati ya hizo kiasi cha shilingi bilioni 24 na milioni 188 (24,188,000,000.00) ni kwa ajili ya
ununuzi wa jengo la ofisi na makazi ya balozi jijini Paris ,Ufaransa (randama
uk 25) na kiasi cha shilingi bilioni 3
na milioni 812 (3,812,000,000.00) ni kwa ajili ya gharama za ukarabati wa
majengo ya ofisi na makazi yaliyopo Ubalozi wa Tanzania Maputo,Msumbiji.
Mheshimiwa Spika,
ukisoma randama ya wizara (uk.120) katika kasma 6391 ,kifungu kidogo 411100
kiasi cha fedha kilichoombwa ni shilingi
bilioni 23 na milioni 900 (23,900,000,000)
kwa ajili ya ununuzi wa jengo la ofisi na makazi ya Balozi jijini Paris, Ufaransa
na shilingi bilioni 3 namilioni 700 (3,700,000,000.00)
kinaombwa kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya ofisi na makazi yaliyopo
ubalozi wa Tanzania Maputo,Msumbiji.
Hata
hivyo, katika mwaka huu wa fedha 2013/2014 kwenye kasma 6391 katika fungu la
Maendeleo (randama uk.120) wizara inaomba kutengewa kiasi cha shilingi milioni 400 (400,000,000.00) (kifungu
221100 ) fedha ambazo hazipo kwenye kitabu cha matumizi ya kawaida juzuu ya
pili (volume II) kwa ajili ya posho ya kujikimu na gharama za usafiri kwa ajili
ya kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Wizara, miradi yenyewe ni
miwili mmoja wa kununua nyumba Ufaransa na kukarabati jengo Msumbiji.
Mheshimiwa Spika,
mkanganyiko huu wa kimahesabu unatia mashaka makubwa sana kuhusiana na dhamira
ya serikali na wizara hii hasa fedha zinapotengwa bila kufuata utaratibu wa
kibajeti na bila kuingizwa kwenye vitabu vya fedha na mafungu husika.
Kambi rasmi ya Upinzani,
inajiuliza tunapitisha mafungu yapi? Kwani kwenye randama fedha zinatofautiana
kwenye fungu moja la maendeleo baina ya (ukurasa 25 na 120) , vilevile kwenye
kitabu cha matumizi ya kawaida hali ni tofauti kwenye fungu la travel out of the Country kwani sasa
wizara imejiongezea shilingi milioni mia nne kwa ajili ya kufuatilia miradi
miwili ambayo ni kununua jengo Paris na kukarabati Jengo la ubalozi - Maputo,Msumbiji.
Mheshimiwa Spika,
utata wa fedha unaendelea kuonekana kwenye randama ya wizara katika
kiambatanisho Na.1 ‘utekelezaji wa ushauri na mapendekezo ya kamati ya kudumu
ya Bunge ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa’ katika
ushauri/mapendekezo Na.5 kamati iliitaka ‘Wizara itoe mchanganuo wa matumizi ya
fedha za bajeti ya maendeleo zilizopokelewa kutoka hazina katika mwaka wa fedha
2012/13’
Maelezo
ya wizara yalikuwa kama ifuatavyo; nanukuu randama ya wizara “katika mwaka wa fedha 2012/2013 ,hadi
kufikia mwezi Machi ,2013 wizara imepokea kutoka Hazina kiasi cha shilingi 13,261,281,600.00 ambapo kati ya fedha
hizo kiasi cha shilingi 9,660,000,000.00
zimetumika kwa ajili ya kulipia malipo ya awali ya ununuzi wa Jengo la Ofisi na
Makazi ya Balozi Paris,Ufaransa;shilingi 995,930,000.00
zimetumika kwa ajili ya ukarabati wa jengo la serikali lililopo Maputo,Msumbiji
;shilingi 626,899,155.00 zimetumika
kwa ajili ya ukomboaji wa vifaa vya ujenzi bandarini vilivyotumika katika ujenzi
wa kituo cha mikutano cha kimataifa cha Julius Nyerere na safari ya kikazi ya
wataalam katika balozi za Maputo,Pretoria na Lusaka kwa ajili ya kazi ya
upembuzi yakinifu wa miradi ya maendeleo iliyopo katika Balozi hizo; na
shilingi 1,978,452,485.20 bado
hazijatumika na zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya kulipia gharama za ukarabati
wa jengo la Serikali lililopo Maputo’
Mheshimiwa Spika, baada
ya kufuatilia na kufanya tathimini ya kina kuhusiana na majibu hayo ya wizara
kuhusu fedha za maendeleo kwa ajili ya ukarabati wa Jengo la Maputo na kununua
Jengo la Ofisi na Makazi ya Balozi Ufaransa na kukuta kuwa ni fedha nyingi sana
kuliko uhalisia wenyewe , kwa mfano waziri anataka Bunge na taifa tuamini kuwa
kufanya ukarabati wa jengo moja la ofisi Maputo Msumbiji tunahitaji kutumia
kiasi cha shilingi 4,695,930,000.00 kwa
kutumia fedha inayoombwa mwaka huu wa fedha na zile ambazo tayari zilishalipwa
katika mwaka wa fedha wa 2012/2013. Aidha wakati wizara inawasilisha majibu
yake kwenye kamati ya kudumu ya Bunge walisema kuwa (swali 12 uk.5) ‘kiasi
cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya Serikali yaliyopo
Maputo ni shilingi 3,812,000,000.00……kiasi hicho cha fedha kinatosheleza
kukamilisha kazi ya ukarabati wa majengo hayo ya Serikali yaliyopo Maputo, Msumbiji’
Aidha,
kununua jengo moja la ofisi na makazi katika Jiji la Paris Ufaransa tunahitaji
kutumia kiasi cha shilingi bilioni 33 na
milioni 560 33,560,000,000.00.
Mheshimiwa Spika, kwa
majibu haya ya wizara ni kuwa tayari wizara imeshafanya malipo ya shilingi bilioni 9.66 kama malipo ya awali kwa
ajili ya ununuzi wa jengo la ofisi na makazi huko Paris Ufaransa , na kuwa
tayari tumeshafanya malipo ya awali kiasi cha shilingi milioni 995.930 kwa ajili ya ukarabati wa jengo la ubalozi huko
Maputo,Msumbiji.
Mheshimiwa Spika,
hakika kiasi hiki ni kikubwa kupitiliza na hata utafiti na tathimini ambayo
ilifanywa na Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni ilionyesha kuwa kununua jengo la
ofisi katika jiji la Paris kwenye mji wa bei ghali kama Co’te d’Azur (most expensive area in Paris) huwezi kutumia fedha
nyingi kiasi hicho kwa ajili ya manunuzi ya jengo la ofisi na makazi.
Aidha,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tunakumbuka sakata la ununuzi wa jengo la
ubalozi lililomkumba balozi Prof.Mahalu huko Roma - Italia na yaliyofuatia
mpaka kesi na fedha zetu tulizoambiwa kuwa zimepotea hazikuweza kurejeshwa
baada ya Prof.Mahalu kushinda kesi hiyo mahakamani.
Hivyo
basi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kupata majibu kuhusiana na mambo
yafuatayo;
i.
Ni eneo gani ambalo tumepata jengo la
kununua kwa ajili ya ubalozi na makazi ya balozi huko Paris, Ufaransa, na ni
nyumba ya aina gani .
ii.
Je, Serikali inaweza kuonyesha mkataba
wa manunuzi wa nyumba hizo (Paris) kwa Bunge na tutalipa kiasi gani kununua
jengo hilo?
iii.
Ni nani au wakala gani wa serikali
aliyefanya tathimini ya hayo majengo na kuamua kuwa tulipe kiasi hicho cha
fedha?
iv.
Ni kampuni gani iliyohusika katika
kufanya makubaliano ya mauziano ya nyumba hizo na tunawalipa kamisheni ya
shilingi ngapi?
v.
Nani, aliidhinisha kutumika kwa kiasi
kikubwa hivyo kwa ajili ya kununua jengo la Ubalozi na makazi huko Paris, je
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, ilishirikishwa katika manunuzi haya?
vi.
Ukarabati unaofanywa kwenye jengo la Maputo
Msumbiji ni wa aina gani, au tunajenga upya nyumba hizo?
vii.
Ni kampuni gani ya ujenzi inayofanya
ukarabati wa jengo letu huko Msumbiji na mkataba wa ukarabati huo uko wapi,
tungetaka uwekwe hadharani.
Aidha , kambi rasmi ya Upinzani
Bungeni , inatoa hoja ya kumtaka Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kufanya uchunguzi maalum (Special Audit)
kuhusiana na ununuzi wa majengo haya na ukarabati unaofanyika kwenye jengo letu
huko Maputo, Msumbiji, na kuona kama thamani halisi ya fedha imezingatiwa , na
kama sheria ya manunuzi ya umma imefuatwa kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, Vile
vile, tungetaka sehemu ya fedha hizi zitumike kwa ajili ya kukarabati jengo
letu la zamani la ubalozi lililopo Washngton ambalo kwa sasa halitumiki baada
ya kutekelezwa kwani likikarabatiwa litaweza kuliongezea taifa mapato kutokana
na matumizi ya kibiashara ya jengo hilo.
8.0 MPANGO WA WIZARA WA KUTOA VISA
KWENYE BALOZI TU
Mheshimiwa Spika,
mpango wa Wizara kutoa visa kwenye balozi tu haukubaliki. Kwa Mujibu wa majibu ya wizara kwenye kamati ya kudumu ya Bunge ya
Mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa ilionyesha kuwa ili wizara iweze
kukusanya fedha za kutosha kwenye balozi zetu ni kwa kurudisha utaratibu wa
utoaji wa viza kufanywa na Balozi zetu tofauti na utaratibu unaotumika hivi
sasa ambapo wageni huweza kupatiwa viza pindi wanapowasili katika vituo vya kuingilia nchini (viza on
arrival).
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni,
haikubaliani na wazo hili la wizara kwani badala ya kuongeza wageni kuja nchini
litapunguza sana hasa ikizingatiwa kuwa ni nchi chache sana ambako tuna ofisi
za Balozi na pia kuna nchi nyingine kama Marekani ambapo, kama mgeni yupo
Carlifonia na anataka kusafiri kuja Tanzania atalazimika kwanza kusafiri kwenda
Washington ambako ndiko kwenye ubalozi atafute visa na ndipo aweze kuja nchini.
Utaratibu huu utaongeza gharama kubwa za
usafiri kwa wageni na watalii na hivyo kulipotezea taifa mapato yataokanayo na
utalii kwani wageni watapungua.
Aidha,
tunaikumbusha wizara kuhusiana na Itifaki ya kuwa na“Single Tourist Destination Protocol” na uwepo wa hati ya kusafiria
na visa moja ya utalii “Single Tourist Visas”
kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo kama sisi tukifanya huo uamuzi basi
wenzetu Kenya wataendelea kupata wageni wengi zaidi kutokana na visa ya pamoja
na wageni wataingia Tanzania kutokana na visa za Kenya chini ya Itifaki hiyo.
8.1 Mkutano wa Mabalozi wa Mwaka
2013/2014
Mheshimiwa Spika,
wizara inahitaji kiasi cha shilingi bilioni
1 kwa ajili ya kufanikisha mkutano wa mabalozi kwa mwaka wa fedha 2013/2014
, na wizara iliwasilisha maombi ya fedha hizo Hazina kama sehemu ya kipaumbele
lakini hazikuweza kupatikana .
Kambi rasmi ya upinzani Bungeni,
inaitaka serikali kuiondoa aibu hii na kutenga hizo fedha kwa ajili ya
kufanikisha mkutano huo na tunapendekeza kuwa katika fungu la protocol safari
za nje ndipo fedha hizo zipunguzwe na kutumika kwa ajili ya mkutano wa mabalozi
wetu ili waweze kupeana ushauri na uzoefu,ili kuboresha ufanisi wa majukumu
yao.
8.2 Utaratibu wa Kupeleka Fedha
kwenye Balozi
Mheshimiwa Spika,
kutokana na utaratibu wa kupeleka fedha kwenye balozi zetu kuwa na mlolongo
mrefu wa kwanza kutoka Hazina na kupelekwa Wizarani, ndipo wizara isambaze
fedha hizo kwenye balozi zetu mbalimbali umesababisha fedha kuchelewa
kufikishwa kwa wakati kwenye balozi zetu na hivyo kusababisha usumbufu mkubwa
na ucheleweshaji wa kazi kwenye balozi zetu.
Kambi rasmi ya Upinzani Bungeni,
inaitaka serikali kubadilisha utaratibu huu na hazina iwe inapeleka fedha hizo
moja kwa moja kwenye balozi husika badala ya kuzipitisha wizarani kama
ilivyofanya kwenye fedha za Halimashauri mbalimbali nchini ili kupunguza
usumbufu huo.
Mheshimiwa Spika,
baada ya kusema hayo kwa niaba ya kambi rasmi ya Upinzani naomba kuwasilisha.
________________________________
Ezekiah Dibogo Wenje
MSEMAJI
MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
NA
WAZIRI
KIVULI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
Imesomwa
leo, tarehe 30 Mei, 2013.
thank u wenje
ReplyDeleteok
ReplyDelete