Tukio hilo linaelezewa kusababishwa wafuasi hao wakijumuika na wakazi wengine wa mji mdogo wa Ruaha wilaya ya Kilosa, wakipinga ushindi kwa mgombea wa uenyekiti wa kijiji cha Ruaha kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Wakitumia magogo na kuchoma moto matairi barabarani, walidai kutoridhika na kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi huo juzi.
Hatua hiyo ya kufunga barabara ilipelekea abiria wanatumia barabara hiyo kushindwa kupita kutokana na vurugu kubwa zilizofanywa katika mji huo, huku baadhi ya mali zikiharibiwa.
Polisi mkoani Morogoro ililazimika kutumia kikosi cha kutuliza ghasia, kikiwa na askari waliotumia magari zaidi ya matano.
Chanzo cha vurugu hizo kinadaiwa kuwa kutangazwa kwa Rashid Kisauni, aliyekuwa mgombea kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa mwenyekiti wa kijiji hicho aliyepita bila kupingwa.
Kabla ya ushindi huo, Kisauni alishinda rufaa aliyoikata katika ngazi ya wilaya, dhidi ya aliyekuwa mgombea kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Isaac Maliwa, aliyeenguliwa kutowania nafasi hiyo.
Katika uchaguzi mdogo wa kijiji hicho uliofanyika wiki iliyopita, Maliwa alishinda lakini Kisauni alikata rufaa kwa madai kuwa mgombea huyo alishindwa kuwasilisha fomu za ugombea kwa mujibu wa sheria.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, John Laswai, alisema vurugu hizo zinadaiwa kufanywa na wafuasi wa Chadema.
Bonyeza Read More Kuendelea
Alisema kuwa katika vurugu hizo, watu hao wanadhaniwa kuwa ni wafuasi wa Chadema, walivamia nyumba anamoishi Kisauni na kuvunja milango, kisha kupora vitu mbalimbali ikiwamo runiga na deki.
Naye Kisauni, alisema kujitambua kuwa mwenyekiti halali wa kijiji hicho, baada ya kushinda kihalali rufaa ya pingamizi dhidi ya mgombea wa Chadema.
Mwenyekiti wa CCM wilayani Kilosa, Nassoro Udulele, amelishutumu jeshi la polisi kwa kushindwa kuwalinda viongozi wake katika vurugu za kisiasa zinazojitokeza mara kwa mara katika kijiji hicho.
Alisema matukio kama hayo yalijitokeza pia mwaka jana wakati wa uchaguzi uliofutwa wa mwenyekiti wa kijiji cha Ruaha na mwenyekiti wa kitongoji cha Ruaha B.
Alisema diwani wa kata ya Ruaha, Raheli Nyangasi na kiongozi wa CCM, Abdallah Dube, waliharibiwa malizao za mamilioni ya fedha.
Kwa upande wake Kaimu Katibu wa Chadema mkoa Morogoro , Boniface Ngonyani, alikanuasha wafuasi ya Chadema kushiriki vurugu hizo na kudai kuwa walioshiriki ni wananchi wa Ruaha.
Alisema wananchi hao hawakuridhika na utaratibu uliotumika kumpata mwenyekiti wa kijiji hicho, huku mgombea wa Chadema akienguliwa.
Naye Mkuu wa kitengo cha ulinzi na usalama wa Chadema mkoa wa Morogoro Zinga Muro, alidai kuwa polisi imetumia nguvu kubwa kuwapiga wafuasi wa Chadema, ikiwamo kupiga jumla ya mabomu ya machozi 56 na risasi za moto 18.
Alisema wamekusanya ushahidi wa maganda yake ikiwa kama vielelezo vya tukio hilo.
Mkoani Iringa, imeripotiwa kuwa wakazi wa manispaa ya Iringa wamelazimika kutembea kwa miguu umbali wa zaidi ya kilomita 15, kutokana na mgomo wa watoa huduma ya usafiri wa daladala.
Mgomo huo ulidumu kwa takribani saa 11, wakidai kunyanyaswa na Ofisa wa Mamlaka ya Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) mkoa wa Iringa, Rahim Kondo.
Usafiri uliopatikana jana, ukiwahusisha watu wachache wenye uwezo wa kati kiuchumi, ulikuwa wa kutumia pikipiki maarufu kama bodaboda, pikipiki za matairi matatu zenye tela za mizigo na magari aina ya Toyota Pick Up.
Abiria hao walitozwa kati ya Shilingi 1,000 hadi 2,000 kwa safari ambayo nauli ya daladala ni Shilingi 400.
Hali ilikuwa mbaya zaidi kwa watumishi wa umma, wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu vya Tumaini, Ruaha na Mkwawa kutokana na huduma hiyo kukwama tangu saa 12:00 asubuhi hadi saa 9:20 alasiri.
Wakizungumza na NIPASHE Jumamosi, wasafirishaji waliogoma, walisema kuwa pamoja na kadhia wanazozipata, Sumatra imewazuia kutumia vituo vya daladala Miyomboni, Posta na National.
Katibu wa wasafirishaji hao, Seleman Mzibilwa, alisema mgomo haukuwa wa kisiasa, isipokuwa kutaka haki itendeke.
“Kuna watu wemetozwa faini ya Shilingi 200,000 hadi 250,000 kwa madai ya kukatisha ruti,” alisema.
Alisema, wasafirishaji hao walimkataa ofisa huyo wa Sumatra kuitaka serikali kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, kuzungumza nao.
Walisema, hawapaswi kuzuiwa kutumia vituo vya Miyomboni, Posta na National kwa kuwa, Sumatra haijawaelekeza kituo kipya.
Hata hivyo, Kondo, alisema tuhuma dhidi yake ikiwamo kuwanyang’anya madereva na makondakta kibali cha usafirishaji hazina ukweli.
Badala yake alisema, amekuwa akiwaonya na kuwataka waache kukatisha ruti kwa kuwa wanawanyima haki abiria wanaolipa nauli halali kwa mujibu wa sheria.
“Kiwango kilichowekwa na serikali kwa kosa kubwa ni Shilingi 250,000 na kwa kiwango cha chini 100,000. Sijaona kosa langu hapa kwa sababu jambo hili lipo kisheria,” alisema.
Hata hivyo, usafiri huo ulirejea majira ya alasiri na kuifanya hali kuwa ya kawaida.
Habari hii imeandikwa na Ashton Baraigwa, Morogoro na Godfrey Mushi na George Tarimo, Iringa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment