Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeilalamikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), kwamba ina mikakati ya kuvuruga uchaguzi mdogo wa madiwani na ubunge unaotarajiwa kufanyika Juni 16, mwaka huu. Uchaguzi huo utahusisha kata 26.
Mkurugenzi wa Kampeni na Uchaguzi wa chama hicho, Msafiri Mtemelwa, aliwaambia waandishi wa habari jana ofisini kwake kwamba Wakurugenzi wa baadhi ya Halmashauri ambao ndiyo wasimamizi wa uchaguzi kwa niaba ya NEC, hawajatoa ratiba ya uchaguzi huo kiofisi.
Alisema fomu za kuomba kuwania nafasi hizo zimefichwa na katika maeneo mengine zinatolewa kwa siri katika baadhi ya Halmashauri hususani ya Babati na Singida, jambo linaloashiria mchezo mbaya unaofanywa na NEC.
Alitoa mfano kwamba, Singida fomu zimeanza kutolewa mwishoni mwa wiki siku ambayo siyo ya kazi kiserikali hivyo kuathiri utaratibu mwingine ambao mgombea anapaswa kuufuata ikiwamo kuapa mahakamani.
"Hali si nzuri katika uchaguzi, kuna kiwingu cha kutaka kuuvuruga, kuna rafu na hila, tumewasilisha malalamiko haya NEC hivyo tunaiomba iyafanyie kazi ili kuondoa hii hali," alisema.
Akijibu tuhuma hizo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Julius Malaba, alieleza kutofahamu taarifa hizo kwa kuwa alikuwa kwenye kikao na kumtaka mwandishi wa gazeti hili kufika ofisini kwake leo kwa ufafanuzi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Babati, Dominick Kweka, alikataa kuzungumzia malalamiko hayo kwa madai kwamba hawezi kuzungumza na mwandishi wa habari asiyemfahamu kwenye simu, wakati Mkurugenzi wa Halmashauri ya Singida, E. Mwenda, simu yake haikuwa inapatikana.
Wakati huo huo, Mtemelwa amesema Chadema inajipanga kwa ajili ya kunyakua jimbo la Sumbawanga Mjini mwaka 2015, baada ya Mahakama ya Rufani kumtangaza mbunge wa jimbo hilo (CCM), Hilaly Aeshi, kuwa mbunge halali.
No comments:
Post a Comment