Saturday, May 18, 2013

CCM wahofia anguko 2015


AHADI nyingi zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete wakati wa uchaguzi mkuu 2010 zimeanza kuwatia hofu ya kushindwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 wabunge wa CCM.
Wabunge hao wa CCM walisema endapo ahadi hizo hazitatekelezeka chama hicho kitarajie kuanguka katika uchaguzi mkuu ujao.
Wakichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka 2013/2014 bungeni mjini hapa, wabunge wengi wa CCM walimtaka Dk. Harrison Mwakyembe wakimtaka ahakikishe ujenzi wa reli, viwanja vya ndege, meli na bandari vinakamilika kabla ya 2015.
Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangala Mwakyembe kwa kushirikiana na waziri mwenzake wa ujenzi, Dk. John Magufuli kuhakikisha wanaufungua Mkoa wa Tabora kwa usafiri wa reli, anga na barabara.
“Tabora imechagua wabunge wote wa CCM 2010, lakini leo haifikiki kwa usafiri wowote iwe reli, ndege wala barabara. Na hatua hiyo imewafanya wapinzani hasa CHADEMA na CUF kutuchonganisha kwa wananchi kuwa umasikini wao umetokana na kuichagua CCM.
“Sasa Mwakyembe kwa kushirikiana na Magufuli hakikisheni mnaifungua Tabora kwa kutekeleza ahadi za rais, vinginevyo uchaguzi ujao 2015 CCM itakuwa janga,” alisema.
Alisema kuwa Serikali ya CCM inapaswa kulifufua Shirika la Ndege (ATC) kwa kukopa ndege kama wanavyofanya mataifa mengine akiitolea mfano Rwanda iliyonunua ndege mpya kwa utaratibu huo.
“Waziri Mwakyembe naamini una akili timamu, una uwezo wa kufanya hayo. Na sisi ukiyafanya hayo hata mwaka 2015 tunaweza kukufikiria kwenye ile nafasi (akimaanisha urais),” alisema.

Bonyeza Read More Kuendelea




Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani alimtaka Mwakyembe alieleze Bunge ni kwanini miradi yote wizara hiyo aliyoahidi Rais Kikwete haitengewi fedha.
Alisema kuwa wananchi wanahoji kiwanja cha ndege Tanga mjini, upanuzi wa bandari ya Tanga na ujenzi wa bandari mpya ya Korogwe, huku akioneshwa kusikitishwa na uamuzi wa ujenzi wa bandari ya Bagamoyo wakati ile ya Tanga ikiwa haijatekelezwa.
“Waziri aniambie kiwanja cha ndege Tanga kiko wapi kwenye bajeti yake, tuliahidiwa reli kufufuliwa na kwenda hadi Musoma. Viwanja vya ndege Same, Arusha na Moshi tulivyoambiwa vimetengewa fedha mwaka jana vipi,” alisema.
Ngonyani, maarufu kama Majimarefu aliongeza kuwa waliokuwa wafanyakazi wa reli Tanga waliahidiwa kulipwa madai yao lakini hadi sasa bado, na hivyo kuonya kuwa bila mambo hayo kufanyika hali itakuwa ngumu kwa CCM 2015 licha ya majimbo yote kukaliwa na chama hicho.
Hata hivyo, wakati CCM wakihofia kuangushwa 2015, wabunge wa upinzani wamekuwa wakishangilia hatua ya serikali ya chama hicho kushindwa kutekeleza ahadi zake wakisema kimechoka kutawala.
Akichangia hotuba hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga, Amina Mwidau (CUF), alisema kuwa serikali ya CCM ilichowafanyia wananchi wa mkoa huo kwa kutowajengea bandari waliyoahidiwa na badala yake bandari hiyo kuhamishiwa Mbegani Bagamoyo ni sawa na kujipa talaka.
“Hii ndiyo talaka yenu CCM, majibu yake mtayaona 2015 kwenye uchaguzi mkuu. Wenzetu Kenya wamekopa wakajenga bandari ya kisasa Lamu, wanayo Mombasa na sasa wana mpango wa kujenga nyingine Shimoni, sisi Tanga tutakuwa wapi kama ahadi yetu imepelekwa Bayamoyo?” alihoji.

No comments:

Post a Comment