Thursday, April 25, 2013

Wabunge Chadema wembe uleule

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilbroad Slaa amewataka wabunge wa chama hicho kuendelea na msimamo wao wa kutetea haki za wananchi. Alisema viongozi wa chama hicho wakiwamo wabunge wako tayari kuumia na kupoteza maisha kwa kutetea maslahi ya watanzania. Amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya Spika wa Bunge Anna Makinda kukosa dira au muelekeo.

Dk. Slaa alisema uamuzi anaoufanya Spika ni ishara ya anguko la serikali iliyopo madarakani.

Alitoa kauli hiyo jana kwenye mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na maelfu ya wakazi wa Jiji la Mbeya katika viwanja vya mikutano vya Ruanda Nzovwe. “Nimeunga mkono msimamo wa wabunge wangu juu ya uamuzi mbovu wa spika kwa sababu wabunge niliwatuma kuwatetea wananchi si kukaa kimya ikizingatiwa sera ya chama ni kutetea maslahi ya wanyonge.

“Kazi tuliyowatuma ni kutetea haki zenu na ndizo zilizowafanya wabunge wetu wafukuzwe.

“Hivyo wananchi tunahitaji michango kwa ajili ya mafuta ambayo yatawafikisha kwenye jimbo la Njombe Kusini kwa Spika, Iramba Magharibi kwa Mwigulu Nchemba na jimbo la Kongwa kwa Job Ndugai,” alisema.

Dk. Slaa alisema ameshangazwa na kitendo cha Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe kutenga Sh bilioni 30 kwa ajili ya maji katika jimbo la Mwanga wakati majimbo mengine yametengewa Sh bilioni nne tu.

Pia alionyesha kushangazwa na kile alichokiita unafiki wa Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.

Alisema wakati wa kampeni za uchaguzi wananchi wa Kyela walionekana kumuunga mkono.

Dk. Slaa alisema alikiomba Chadema kisimchafue katika siasa lakini alimtahadharisha kuwa atakapoingia bungeni asiende kuwageuka wapinzani hasa katika masuala yanayohusu maslahi ya taifa.

Katibu Mkuu huyo wa Chadema alidai kuundwa idara mpya ya kusimamia miradi (Presidential Delivery Unit) kilichotengewa zaidi ya Sh bilioni 29 kwa ajili ya kitengo cha mipango na wataalamu, ni aina nyingine ya ufisadi.

Alisema fedha hizo zingeweza kujenga madarasa 4,142 ya shule za msingi, madarasa 2,071ya shule za sekondari, zahanati 580 na vituo vya afya 290

Hii ni mbinu za kuendeleza ufisadi mpya ndani ya serikali ya Chama cha Mapinduzi, alidai Dk. Slaa.

Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Jimbo la Iringa, alisema wabunge wa Chadema wapo tayari kupoteza viti vyao vya ubunge ili watoto waje kuishi maisha mazuri katika bunge la 2015.

“Jumatatu narudi bungeni tena naenda kuwasilisha bajeti kivuli ya maliasili na utalii, cheche nitakazoonyesha hapo Mungu ndiye anayejua kwa vile lengo ni kusimamia haki za wapiga kura wetu ambao ndiyo waliotufikisha hapo bungeni,’’alisema.

Msigwa alidai kiti cha Spika kimekuwa hakiwatendei haki kwa sababu wabunge waliotoa kauli za matusi ni wa Chama cha Mapinduzi.

Alisema anashangazwa Wabunge wa Chadema kuadhibiwa.

Naye Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia alisema ili maendeleo yaweze kufikiwa ni lazima watu waumie.

Alisema kwa sababu hiyo kuondolewa kwao bungeni ni ishara ya mafanikio ya chama kushika nchi mwaka 2015.

“Mtu ukianza safari ya ukombozi ni lazima uwe na utayari wa kuumia hivyo hatushangazwi na hatua ya kuondolewa bungeni … hii ni ishara ya kupatikana kwa maendeleo,”alisema.

Mbunge wa jimbo la Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi alisema ni vigumu kukaa kimya huku kiongozi wa kambi ya upinzani akitolewa nje bila ya sababu ya msingi.

Alimtaka Naibu Spika, Jobu Ndugai kutambua kuwa yeye ameenda bungeni kufanya kazi na si kukaa kama boya.

Akizungumzia shughuli za maendeleo, Sugu aliwataka wananchi kutokubali kupokea au kukabidhiwa barabara viraka zinazojengwa hivi sasa kupitia mradi wa Benki ya dunia.

Sugu pia alitoa miezi mitatu kwa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Rashidi Juma kuhakikisha ujenzi wa soko la Mwanjelwa unakamilika na kukabidhiwa.
Mtanzania

No comments:

Post a Comment