KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimechanganyikiwa ndiyo maana kinafanya hujuma kutaka kuisambaratisha CHADEMA.
Dk. Slaa alisema CCM inafanya hivyo kwani inajua fika mwisho wao wa kutawala kwa kuwadanganya Watanzania umewadia.
Alitoa kauli hiyo jana katika Ukumbi wa Vijana mjini hapa wakati wa mkutano wa uzinduzi wa Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) Kanda ya Kati inayojumuisha mikoa ya Singida, Morogoro na Dodoma.
Akizungumza na wajumbe wa mikoa hiyo, Dk. Slaa alisema hujuma za kutaka kuisambaratisha CHADEMA zimekuwa zikifanywa na serikali, Bunge na CCM yenyewe.
Alisema serikali kupitia vyombo vyake na kwa kushirikiana na CCM, inatapatapa kuokoteza ushahidi wa uongo kuwabambikizia kesi baadhi ya viongozi na wanachama wa CHADEMA, huku Bunge kupitia spika na naibu wake likitumia udikteta kukisambaratisha chama hicho.
“Nyie wajumbe ni mashahidi wa hili, mmesikia jinsi serikali na CCM walivyotengeneza ushahidi wa video ya kutunga kumbambikia kesi ya ugaidi Mkurugenzi wetu wa Ulinzi na Usalama, Wilfred Lwakatare.
“Serikali inahaha, Bunge linahaha na CCM inahaha usiku na mchana kujaribu kuisambaratisha CHADEMA, lakini nawaambia hawawezi na mwisho wa utawala wao umekwisha,” alisema Dk. Slaa na kuibua shangwe kutoka kwa wajumbe hao.
Dk. Slaa alimshambulia Spika wa Bunge Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai kwamba wanaongoza Bunge kwa maelekezo ya serikali yao ya CCM ili isianguke.
“Bunge linaonesha kila dalili ya upendeleo, spika anafanya kazi kwa maelekezo, si kwa utashi wake, sio kwa kanuni, sio kwa busara zake bali kwa maelekezo ya chama na serikali yake. Hili ni jambo baya sana,” alisema.
Alisema dalili za chama chochote tawala kupoteza madaraka ni pale kinapoanza kutumia dola na Bunge kutaka kubaki madarakani na kutolea mfano wa CCM kwamba mwisho wake ni 2015.
Bonyeza Read More Kuendelea
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alitumia nafasi hiyo kuwafahamisha wajumbe jinsi Spika Makinda alivyokosea kuhalalisha adhabu iliyotolewa na Naibu wake, Ndugai dhidi ya wabunge sita wa CHADEMA.
Mbali ya hilo, Mbowe alielezea sababu na umuhimu wa mpango huo wa kanda na kuwataka wajumbe wa mkutano huo kutambua kwamba wana kazi kubwa ya kufanya kuleta mabadiliko katika mikoa hiyo.
Mbowe alisema katika kipindi cha miaka 22 tangu CHADEMA ilipoanzishwa, ina mbunge mmoja wa kuchaguliwa na wanne wa viti maalumu katika kanda hiyo inayojumuisha mikoa mitatu.
“Miaka 22 imepita na katika kipindi hicho tumefanya kazi kubwa. Wapo watu waliojitolea hadi kupoteza maisha, wengine wamefilisika kwa kujitolea, lakini katika muda huo tuna mbunge mmoja katika majimbo 28 na wabunge wa viti maalumu watatu,” alisema Mbowe.
Alimtaja mbunge wa kuchaguliwa kuwa ni Tundu Lissu wa Singida Mashariki na wabunge wa viti maalumu ni Suzan Kiwanga, Christowaja Mtinda na Christina Lissu.
Alisema hali hiyo ilitokana na chama kutofika ngazi ya chini, lakini mpango huo unalenga kupoka madaraka ya chama kutoka makao makuu ya Dar es Salaam, kuyafikisha ngazi ya kanda, wilaya, kata vijiji hadi chini.
Dk. Slaa aliongeza kuwa mpango huo utabadilisha mkakati wa mapambano kwani badala ya harakati hizo kuanzia makao makuu ya chama, zitaanzia ngazi ya kanda kushuka chini.
Akizungumzia kuhusu mabadiliko ya katiba, Mbowe alisema msimamo walioutoa bungeni upo pale pale kwamba kama hakutafanyika mabadiliko kuhakikisha wajumbe wa mabaraza ya katiba wasiwe wajumbe wa CCM kama walivyofanya sasa, CHADEMA itajitoa katika mchakato huo ifikapo mwisho wa mwezi.
Wakati huo huo, wabunge sita wa CHADEMA waliosimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa siku tano, leo wanatarajiwa kuwasha moto kwenye mkutano wa hadhara utakaofanyika jijini Mwanza.
Wabunge hao watafanya mkutano huo katika viwanja vya Mbugani unaotazamiwa kuhudhuriwa na maelfu ya watu kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Mwanza.
Wabunge hao ni Tundu Lissu (Singida Mashariki), Highnes Kiwia (Ilemela), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Ezekia Wenje (Nyamagana), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa) na Godbles Lema (Arusha Mjini).
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili kuhusu mkutano huo, Wenje alisema kuwa wameamua kuionesha dunia dhuluma na ukandamizwaji wa demokrasia unaofanywa na Serikali ya CCM.
Alisema kwa muda wa siku tano nje ya Bunge watafikisha na kuonesha jinsi Serikali ya CCM ilivyojipanga kuzima hoja za maendeleo.
“Timu ya wabunge wote tuliotolewa nje tumeamua kuwasha moto wa ukombozi kwa Watanzania. Tunakwenda kuishughulikia kikamilifu Serikali ya CCM.
“Tunakwenda kuionesha nchi na dunia jinsi demokrasia, haki na usawa vinavyodhulumiwa na serikali. Moto tunaokwenda kuuwasha ni wa kueleza uozo wa kiti cha spika na wabunge wa CCM,” alisema Wenje.
Aidha alisema operesheni yao hiyo wataifanya kwa kila jimbo la mbunge aliyesimamishwa bungeni.
Kwa mujibu wa Wenje, timu hiyo pia itahutubia mikutano mikubwa kwenye Jimbo la Kongwa la Ndugai na wakiwa huko watafichua uovu wa kiongozi huyo.
Mbunge wa Ilemela, Kiwia alisema uongozi wa kibabe unaofanywa na kiti cha spika kamwe hauna nia njema ya kuwasaidia Watanzania masikini.
No comments:
Post a Comment