Sunday, April 28, 2013

Mbowe: Hakuna wa kutuziba midomo


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema hakitakubali kuzibwa midomo bungeni kwa ajili ya kupigania haki za Watanzania.

Hivi karibuni wabunge watano wa Chadema walifukuzwa bungeni na kupewa adhabu ya kutohudhuria vikao vitano vya Bunge la Bajeti kutokana na madai ya kufanya vurugu.

Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, aliyaeleza hayo jana wakati akizungumza na maelfu ya wananchi wa kata ya Ruaha wilayani Kilosa mkoani hapa kwa kusema hawatishwi na hali hiyo kwakuwa tayari Watanzania wamewaelewa wabunge wa chama hicho ndiyo watetezi wa maslahi yao.

“ Kuna upendeleo wa wazi unafanyika pale bungeni lakini nyinyi Watanzania mnajua wabunge wa Chadema ndiyo wanatetea maslahi yenu hivyo wanatafuta sababu ya kutupunguza nguvu lakini tunawaambia hawataweza kutuziba midomo tutaendelea kuwatetea tu,” alisema Mbowe na kushangiliwa na umati mkubwa watu.

Alisema namna Chadema inavyojitahidi kutetea haki za Watanzania kupitia kwa wabunge wake ni pamoja na kuhakikisha hotuba za mawaziri vivuli wa chama hicho zinazowasilishwa bungeni wanaidurufu na kusambaza kwa wananchi wa ngazi za chini hasa kuanzia ngazi za vijiji ili waone viongozi wao wanachokifanya.

Alisema kuwa Chadema itahakikisha inapigania rasilimali za nchi ili zitumike kwa manufaa ya wananchi wote na sio watu wachache ambao hawana uchungu na nchi.

“Sisi Chadema hatupo bungeni kwa ajili ya kuwafurahisha wachache bali ni kutetea haki za wanyonge hivyo nawaomba Watanzania mtuunge mkono katika juhudi za Chadema ili kuleta ukombozi,” alisema Mbowe.

Mbowe pia aliwaombea kura wagombea wa nafasi za mwenyekiti wa kitongoji kata ya Ruaha huku akiwataka viongozi wa Chadema kufanya kazi kwa uadilifu na kuwatendea haki wananchi wote bila ya kujali itikadi zao za kisiasa.

Katika mkutano huo wananchi walieleza kero zao mbalimbali ikiwamo suala la mwenyekiti wa kijiji cha Ruaha, Isaack Maliwa, kupitia Chadema kuwekwa rumande zaidi ya miezi sita na kukosa dhamana na hivyo walimuomba Mbowe kupeleka hoja hiyo bungeni ili Watanzania wengine wajue namna sheria za nchi zinavyokiukwa. 
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment