POLISI WAZINGIRA NYUMBA YAKE USIKU, WAMKAMATA
SIKU tatu baada ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, kuliamru Jeshi la Polisi mkoani hapa kumkamata Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, hatimaye amri hiyo ilitekelezwa juzi usiku saa 5:30.
Lema alikamatwa baada ya maofisa wa polisi wa kitengo cha upelelezi na wale wa doria kuizingira nyumba yake kuanzia saa 4:00 hadi saa 5:30 usiku alipoamua kujisalimisha.
Mbunge huyo anatuhumiwa na mkuu wa mkoa kuwa alichochea vurugu za wanafunzi katika Chuo cha Uhasibu Arusha na kusababisha kiongozi huyo kuzomewa na gari lake kurushiwa mawe.
Hata hivyo madai ya Mulongo kuwa Lema aliwachochea wanafunzi hao si ya kweli, kwani ushahidi wa video unaonesha kuwa mbunge huyo alitumia kila aina ya ushawishi kuwasihi wasiandamane baada ya mwenzao, Elly Kago (22), kuuawa na watu wasiojulikana jirani na chuo hicho.
Katika hali ya kuonesha kuwa Mulongo anatumia madaraka yake vibaya, Lema juzi aliwaeleza waandishi wa habari kuwa alipokea ujumbe wa maandishi kutoka kwa mkuu huyo ukimtisha.
“Umeruka kihunzi cha kwanza, nitakuonyesha kuwa mimi ni serikali, ulikojificha nitakupata na nitakupa kesi ninayotaka mimi,’’ ulisomeka ujumbe huo uliotumwa kupitia simu namba 0752 960276, ambayo Lema alidai ni ya Mulungo.
Akithibitisha kukamatwa kwa Lema, Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, alisema alijisalimisha kwa maofisa hao baada ya mashauriano makubwa baina yake na viongozi wa chama.
Golugwa alisema baada ya maelezo hayo waliamua kumpigia simu Lema ambaye alikuwa nyumbani kwake na familia yake ili awasikilize maofisa hao. Kwamba alipotoka nje walimweleza kuwa wanamhitaji kituoni kwa tuhuma za uchochezi.
“Sisi kama viongozi baada ya kupata taarifa ya askari kuizingira nyumba ya Lema tulifika haraka nyumbani kwake Njiro na baadhi ya wanachama wengi wa CHADEMA, hali iliyomtia moyo na kuamua kujisalimisha kwa amani,’’ alisema.
Alisema kuwa tayari wamewasiliana na viongozi wa chama makao makuu akiwamo Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa na mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lisu, ambao waliwataka viongozi hao kutochukua hatua zozote kichama hadi watakapopata maelekezo kutoka makao makuu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabasi, alithibitisha kuhusu tukio hilo akisema kuwa bado wanaendelea kumhoji na atabaki mahabusu hadi Jumatatu atakapofikishwa mahakamani.
Kukamatwa kwa Lema kulizua tafrani kwa baadhi ya wafuasi wake ambao walijitokeza kwa wingi kituo kikuu cha polisi lakini baadaye waliondolewa na askari.
Bonyeza Read More Kuendelea
Mbowe ahadharisha
Kufuatia tukio hilo, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, ameitahadharisha serikali kuwa makini na vurugu za Arusha, vinginevyo watajikuta wakisababisha vurugu zaidi.
Alisema Mkuu wa Mkoa wa Arusha alipaswa kutumia busara alipofika kuzungumza na wanachuo ambao tayari walikwisha kuwa na hasira baada ya mwenzao mmoja kuuawa.
“Ukiangalia mkanda wa video uliochukuliwa kwenye tukio hilo na sasa upo kwenye mtandao wa You tube, hakuna sehemu Lema ameonekana akichochea vurugu.
”Utaona kuwa Lema alitumia nguvu na busara sana kuwazuia wanachuo wasiandamane. Lakini mkuu wa mkoa ndiye aliyelikoroga,” alisema.
Katika hatua nyingine, wabunge wanne miongoni mwa sita wa CHADEMA waliokuwa wamesimamishwa kuhudhuria vikao vitano vya Bunge, jana walifanya mkutano mkubwa katika Jimbo la Kongwa linaloongozwa na Naibu Spika, Job Ndugai.
Wabunge hao, Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Peter Msigwa (Iringa Mjini), Ezekiel Wenje (Nyamagana) na Highness Kiwia (Ilemela), waliapa kuendeleza msimamo wao bungeni kutetea hoja zenye masilahi ya wananchi.
Wakiwa na wabunge wengine wa chama hicho pamoja na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, walifanya mikutano katika kata za Kibaigwa, Kongwa, Ngomai, Chamkoroma, Hembahemba, Pandambili na Mlali wakiwataka wananchi wasifanye makosa mwaka 2015 kuichagua CCM.
No comments:
Post a Comment