Saturday, April 6, 2013

Kiongozi mwingine CHADEMA akamatwa


KAMATA kamata ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) inayofanywa na Jeshi la Polisi imeendelea, ambapo sasa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (BAVICHA) mjini Bukoba amekamatwa akidaiwa kukabiliwa na makosa ya jinai.
Hatua hiyo inakuja zikiwa ni wiki takribani tatu tangu kukamatwa kwa Mkugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama hicho, Wilfred Lwakatare ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mkoa wa Kagera.
Lwakatare alikamatwa pamoja na kijana Joseph Ludovic kisha kuhojiwa na kufunguliwa mashtaka manne ya jinai ukiwemo ugaidi.
Uchunguzi wa gazeti hili ulibanini kuwa kiongozi huyo, Evodi Justinian (30) alishikiliwa kwa siku mbili mfululizo kabla ya kumsafirisha jana kwenda wilayani Igunga, Tabora ambako anadawa kutenda makosa ya jinai.
Justinian alikamatwa Jumanne, siku moja baada ya mapumziko ya Sikukuu ya Pasaka alipojisalimisha mwenyewe katika kituo cha polisi mijini hapa kufuatia taarifa za awali kuwa alikuwa akitafutwa na polisi.
Kukamatwa kwa kiongozi huyo kunakuja baada ya wiki kadhaa tangu kukamatwa Lwakatare ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, akihusishwa na makosa ya jinai.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Philip Kalangi hakutaka kulizungumzia kwa undani suala hilo lakini aligusia kuwa alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya kushambulia na kujeruhi mtu huko wilayani Igunga.
Kalangi alisema kuwa mtuhumiwa anadaiwa kutenda kosa hilo mwaka 2011 na kwamba polisi wenzao mkoani Tabora waliwatumia ujumbe ambao ulifuatia kukamatwa kwake baada ya kufika katika Kituo Kikuu cha Polisi mjini Bukoba siku ya Jumanne.




Hata hivyo taarifa ambazo gazeti hili lilizipata kabla ya Justinian ambaye pia ni Mweka Hazina wa Baraza la Vijana wa Wilaya ya Bukoba kusafirishwa kwa siri juzi asubuhi, polisi walifuatana naye maeneo ya Rwamishenye na kufanya upekuzi nyumbani kwake.
Kwa mujibu wa maelezo ambayo yako kwenye nakala aliyoachiwa mke wa kiongozi huyo baada ya upekuzi, vitu vilivyochukuliwa na polisi nyumbani mwake ni pamoja na CD tatu za CHADEMA za kusherehekea ushindi wa mbunge 2012 zilizoandaliwa na Victor Video.
Vitu vingine vilivyochukuliwa katika upekuzi huo uliofanywa na H. S. Mwaibambe ni CD nyingine mbili, moja iliyoandikwa The Sick sin na nyingie Obama Jaluo.
Tangu taarifa za kukamatwa kwa kiongozi huyo zifahamike, viongozi wa CHADEMA akiwemo Mwenyekiti wa Wilaya ya Bukoba mjini, Victor Sherejeh pamoja na jamaa walionekana katika kituo kikuu cha polisi katika kutaka kumpatia dhamana.
Sherejeh alisema kuwa polisi waliwaambia kuwa kiongozi huyo angesafirishwa kwenda mkoani Tabora ambako suala lake litashughulikiwa.
Hata hivyo, taarifa zilizopatikana saa 12.00 za jioni jana zilieleza kuwa kada huyo alikuwa katika Kituo cha Polisi mkoani Mwanza ambako polisi walikuwa wakiendelea kumhoji badala ya kupelekwa Igunga kama ilivyoelezwa na polisi hapo awali.
Kutokana na taarifa za kukamatwa kwa kiongozi huyo kuhusishwa na tukio la Igunga, tayari kumekuwa na minong’ono kuwa huenda linahusiana kwa karibu na matukio yaliyojitokeza wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge mwaka 2011.
Katika uchaguzi huo uliokuwa na mikiki mikiki ya hapa na pale, mgombea wa CCM, Dalali Kafumu alimshinda mpinzani wake wa CHADEMA, Joseph Kashindye.
Hata hiyo mahakama ilitengua ushindi wake kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa kupinga matokeo hayo kutokana na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi.
Wakati wa kampeni za uchaguzi huo, kijana wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) alimwagiwa tindikali usoni na mtu asiyefahamika, ingawa tangu wakati huo Jeshi la Polisi halikuweza kumkamata mtuhumiwa.

No comments:

Post a Comment