Thursday, April 4, 2013

Chadema wamrushia Mwakyembe kombora


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimemjia juu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kikimtuhumu kukiuka masharti ya zabuni kwa kuipa kampuni inayomilikiwa na CCM zabuni ya ujenzi wa mradi wa maegesho ya magari makubwa na makontena, utakaogharimu Sh. bilioni 10, ambao kimesema ni ufisadi kwa kuwa ni kinyume cha Sheria ya Manunuzi ya Umma.
 
Kampuni hiyo imetajwa kuwa ni “Jitegemee Trading Company Limited”.
 
Chadema imedai mbali na kuipa zabuni kampuni ya CCM, Mwakyembe pia ameupeleka mradi huo kujengwa kwenye eneo la Shirika la Uchumi na Kilimo Tanzania (Sukita), ambalo linalomilikiwa pia na CCM, Barabara ya Mandela, katika Bonde la Mto Msimbazi, eneo la Tabata, jijini Dar es Salaam. 
 
Mkurugenzi wa Organaizesheni na Mafunzo wa Chadema, Singo Kigaila, alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.
 
Alisema mradi huo ni kitu kizuri, lakini cha msingi, ambacho kinapaswa kuhojiwa, unajengwa wapi, na nani na kiasi gani taratibu zimefuatwa.
 
Kigaila alisema Halmashauri ya Temeke awali, ilitaka kuingia ubia na Bandari kujenga mradi huo kwenye eneo la Kurasini, karibu na Bandari, lakini Mwakyembe ameliacha eneo hilo na kuupeleka kwenye eneo la Sukita.
 
“Ukipeleka kujenga mradi kama huo Sukita, ambako CCM ilikuwa inafuga nguruwe pale na ng’ombe, wakachukuliwa na maji kwenye mafuriko, unakwenda kujenga mradi wa kupaki magari ya watu pale ya wateja wanayotoa bandarini, maana yake unataka yakichukuliwa, Bandari ilipe fidia kwa hao watu. Unapeleka pale kwa sababu ni eneo la CCM ili iendelee kupata pesa. Kwa hiyo, unaitafutia ulaji CCM,” alisema Kigaila.
 
Alisema Mwakyembe pia ameipa kampuni hiyo zabuni bila kuifanyia upembuzi yakinifu kujua kama ina uwezo wa kiuchumi wa kufanya hiyo kazi.
 
Kigaila alisema kwenye bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014, kampuni hiyo imeshatengewa Sh. bilioni 10 kwa ajili ya kazi hiyo.
 
Hata hivyo, alisema wakati serikali ikipiga kelele kuwataka waliojenga mabondeni wahame ili kuepuka nyumba zao kubomolewa na mafuriko, inachukua mabilioni ya shilingi na kuipa kienyeji kampuni ya CCM kwenda kujenga kwenye bonde hilo.
 
Alisema hata kama eneo hilo litainuliwa juu sana, bado litaleta madhara, kwani maji yatamwagika kwa walalahoi na hivyo, kuwapelekea mafuriko.
 
Kutoka na hali hiyo, alihoji sababu za mradi huo kupelekwa kwenye bonde la maji, huku wanaoishi mabondeni wakitakiwa kuhama, sababu za kampuni hiyo kupewa zabuni bila kutangazwa, sheria ya manunuzi ya umma kutofuatwa na kama huo siyo ufisadi.
 
Waziri Mwakyembe alipoulizwa jana, alisema yeye anafanya kazi kuhakikisha Watanzania wanapata maendeleo na kwamba, kazi ya Chadema ni kupiga porojo, hivyo akawataka waendelee kupiga porojo.
 
Katibu wa Halmashauri Kuu (Nec) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alipoulizwa na NIPASHE jana kama kweli kampuni hiyo inamilikiwa na CCM na imepewa zabuni hiyo na Waziri Mwakyembe, alisema ataijibu Chadema katika mkutano wake na waandishi wa habari leo.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment