Thursday, April 25, 2013

CHADEMA walalamika kutopewa ratiba ya uchaguzi


WAKATI vyama vya siasa nchini vikiwa vinajiandaa na uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani katika kata 26 utakaofanyika Juni 16, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeeleza kusikitishwa na kitendo cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutowapelekea  ratiba ya uchaguzi huo kiofisi.
Akizungumza na Tanzania Daima juzi, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa alisema taarifa za kuwepo kwa ratiba ya uchaguzi ya NEC, aliisikia na kuisoma kupitia vyombo vya habari na kuipata barua hiyo kutoka katika chama kimojawapo cha siasa nchini.
“Ofisi yangu haijapata barua rasmi kutoka tume kuhusu ratiba ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Chambani na kata 26 zilizo wazi, habari za kuwepo jambo hilo kwanza nilizipata kupitia vyombo vya habari Jumatatu,” alisema Dk. Slaa.
Kutokana na hali hiyo, alieleza kutopendezwa na tabia ya NEC ya kutokiarifu chama chake katika masuala ya msingi kama hayo.
Aidha, alisema katika uchaguzi wa serikali za mtaa uliomalizika mwanzoni mwa mwaka huu pia hawakupewa taarifa mapema ila vyama vingine vilipata.
“Vitendo kama hivi ambavyo vinafanywa na tume ndivyo vinavyopelekea mara kwa mara tuseme kuwa hatuna imani nayo… huo ni ubabaishaji ambao hatuukubali na hata wananchi ambao ndio wapiga kura wanawajua,” alisema Dk. Slaa.
Akijibu tuhuma hizo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Julius Malaba, alikana madai hayo na kueleza kuwa hawawezi kutoa taarifa katika vyombo vya habari kabla ya kuviarifu vyama vya siasa ambavyo ndiyo wahusika wakubwa.
Akizungumzia taarifa ya kutotangazwa kwa uchaguzi mdogo wa Kata ya Sombetini ambayo ipo wazi katika Halmashauri ya Jiji la Arusha, Malaba alisema kuwa hawajapewa taarifa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) kwamba ipo wazi na inatakiwa kurejea kwa uchaguzi.
Malaba alifafanua kwamba NEC inatoa ratiba ya kufanyika uchaguzi mdogo wa kata ambayo ipo wazi baada ya kupata taarifa rasmi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI ambao nao wanakuwa wameandikiwa na mkurugenzi wa halmashauri husika.

No comments:

Post a Comment