YALAANI PIA DANADANA SAKATA LA KIBANDA
KAMATI Kuu (CC) ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imeazimia masuala nane likiwemo la kubariki hatua ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuendelea na hatua ya kukiwajibisha kiti cha Spika kutokana na kushindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo.
Kamati hiyo iliyokutana kwa siku tatu jijini Dar es Salaam ilijiridhisha kuwa katika vikao vya Bunge vya Februari mwaka huu, Spika wa Bunge Anne Makinda, Naibu wake, Job Ndugai na wenyeviti wa Bunge walikuwa wakivunja kanuni na kuondoa hoja binafsi za wabunge wa upinzani kwa lengo la kuilinda Serikali ya CCM isifedheheke.
Akisoma maazimio hayo kwa waandishi wa habari jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika alisema kuwa CC imeafiki kuwa hatua za kibunge zichukuliwe dhidi ya Makinda na Ndugai.
Hatua hiyo ni mwendelezo wa kusudio lililotolewa na chama hicho Februari mwaka huu, kuwa kitawasilisha hoja bungeni kutaka viongozi hao wang’olewe kutokana na kuliongoza Bunge kibabe na kukiuka kanuni rasmi.
“Mliona mambo yaliyojiri bungeni Februari, Spika alikuwa anavunja kanuni, kuondoa hoja binafsi za wabunge wa upinzani. Kimsingi kiti kilikiuka kanuni za Bunge. Kamati Kuu imeazimia kuwa hatua za kibunge zichukuliwe dhidi ya Spika na naibu wake,” alisema.
Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Ubungo, aliongeza kuwa hatua za awali ambazo CHADEMA walianza nazo wakiwa bungeni ni kuwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na Spika na naibu wake wakiwatuhumu kutumika kupindisha kanuni za Bunge kwa minajili ya kutimiza matakwa ya serikali.
Alisema hali hiyo inaonesha kuwa viongozi hao wako pale kwa manufaa ya serikali kinyume na kanuni ya nane ya Bunge.
Sakata la Kibanda
Kuhusu sakala la kuvamiwa na kuumizwa vibaya kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Absalom Kibanda mwanzoni mwa mwezi uliopita, Kamati Kuu ililaani kitendo hicho na kutaka hatua za haraka zichukuliwe kuwabaini wahusika.
“CHADEMA inalaani kitendo hicho cha kusikitisha, lakini kwa kuwa tukio hilo linafanana na lile la Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk. Stephen Ulimboka, tunaomba serikali ichukue hatua iache kusuasua,” alisema.
Mnyika alisema kuwa jambo hilo linafanywa kimya kimya bila kushughulikiwa kama lilivyofanywa la Dk. Ulimboka ambapo Ofisa wa Usalama wa Ikulu Ramadhani Ighondu amekuwa akitajwa kuhusika, lakini serikali haijawahi kuchukua hatua.
“Kama ambavyo serikali haijachukua hatua zozote kwa mauaji ya Mwangosi, ingawa awali baada ya kifo hicho Ikulu ilitoa kauli ikisema inasubiri ripoti ya tume, tume zote zilitoa majibu yake, lakini hadi sasa Ikulu ipo kimya,” alisema Mnyika.
Kuhusu suala la waliokuwa madiwani wa CHADEMA jijini Arusha na kutimuliwa kisha wakashindwa kutekeleza amri ya mahakama ya kulipa fidia ya chama, Mnyika alisema kuwa CC imeridhia wakamatwe popote walipo ili sheria ichukue mkondo wake.
“Na kuhusu meya aliyejipachika wadhifa huo kinyume cha kanuni katika uchaguzi wa Manispaa ya Ilemela, CC imebariki kuwa aandliwe hati ya madai ya sh milioni 29 kutokana na kufuta kesi aliyokuwa amekifungulia chama,” alisema.
Kamati Kuu hiyo pia ilipokea nakala ya barua iliyoandikwa kwa Waziri Mkuu kumtaka ashughulikie mgogoro huo wa uchaguzi batili wa meya wa Ilemela, ambayo hadi sasa haijajibiwa na hivyo kuwataka wabunge wa CHADEMA wamhoji bungeni ni kwanini anasimamia uvunjaji wa sheria namna hiyo.
Pia, CC ilijadili suala la udini nchini na kulaani viashiria vyote vinavyochochea hali hiyo inayoanza kuligubika taifa kwa sasa.
Mnyika alisema kuwa Kamati Kuu imeonya kuwa propaganda hizo zimepandikizwa na viongozi wa serikali na CCM.
Mambo mengine yaliyojadiliwa na kutolewa maazimio katika kikao hicho ni Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Elezer Feleshi kukalia jalada la vitendo vya kijinai na fujo vilivyofanywa na viongozi wa CCM wakiongozwa na Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Rage.
Alisema kuwa Rage na wenzake waliwashambulia na kuwajeruhi viongozi na wanachama wa CHADEMA huko Dodoma, Februari mwaka huu. Kwamba CC imeazimia kuendelea kushauriana na wanasheria wake ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Kuhusu ziara ya Rais wa China nchini hivi karibuni, CHADEMA imeitaka serikali kuweka wazi mikataba iliyoingiwa baina ya Tanzania na China.
“Watanzania hawajui kuhusu mikataba iliyosainiwa na iwapo serikali itazidi kukaa kimya, tutatumia kanuni za kibunge kudai uwazi katika mikataba hiyo bungeni, kwani nchi yetu imekuwa ikiingia katika mikataba mibovu kwa kuwa ina maslahi ya CCM,” alisema.
No comments:
Post a Comment