Wednesday, March 27, 2013

RC aikejeli CHADEMA, Lema amuonya


MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), amemuonya mkuu wa mkoa huo, Magesa Mulongo, kuacha kutumia nguvu kubwa kudhibiti harakati za chama, vinginevyo atashindwa kufanya kazi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Lema alimtaka mkuu huyo kuacha kuingilia majukumu ambayo si yake na kwamba endapo ataendelea wataitisha mikutano na kuwasihi wananchi kutompa ushirikiano.
Kauli ya CHADEMA ilikuja baada ya mkuu wa mkoa kusikika katika vituo vya radio vya mjini Arusha jana asubuhi akiwataka vijana kutoshiriki maandamano ya chama hicho akidai viongozi wao wasingelidhurika na matokeo ya maandamano hayo.
CHADEMA jana iliahirisha maandamano yake yaliyokuwa yafanyike katika majiji manne likiwemo la Arusha ili kumshinikiza waziri wa elimu na naibu wake kuachia ngazi kutokana na matokeo mabaya ya kidato cha nne 2012.
Mulongo katika kujaribu kufifisha nguvu ya CHADEMA, alitumia vituo hivyo vya redio akisema, “Vijana mnahamasishwa kuandamana, wakati mnafanya hivyo viongozi wa chama watakuwa baa wakinywa bia nyie mnakabiliana na vyombo vya dola, hivyo nawaonya kutojiunga katika maandamano hayo.’’
Kufuatia kauli hiyo, Lema alisema ameshangazwa na mkuu huyo wa mkoa kwani suala la maandamano lilikwishatolewa tamko na viongozi wa makao makuu wa chama hicho baada ya kushauriana na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Saidi Mwema.
“Sasa hivi hakuna mawasiliano ndani ya serikali kwani suala la maandamano lilishamalizwa na viongozi wa kitaifa yeye bado analiendeleza na kukashifu chama, tutamfanya akose ushirikiano katika kazi zake akiendelea na tabia hii,’’ alisema Lema.
Naye Mwenyekiti wa Vijana wa Mkoa wa chama hicho, Ephata Nanyaro, amempa siku tatu Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD), Gilles Bilabaye, akimtaka kukiomba radhi chama hicho na wananchi wa Arusha kuwa wanataka kuandamana kwa sababu ni walevi.
“Huyu OCD anatuambia sisi ni walevi wa viroba pamoja na wananchi ndio maana tunaandamana! Tunaomba ndani ya siku tatu atuombe radhi kabla hatujaamua kutumia nguvu ya umma kushughulika naye!’’ alisema Nanyaro ambaye ni Diwani wa Kata ya Levolosi.
Juzi OCD huyo alinukuriwa katika maeneo mbalimbali ya mjini Arusha alikokuwa akizunguka na kipaza sauti akiwa ndani ya gari namba PT 1844, akiwazuia wananchi kutojitokeza katika maandamano hayo.
Alipotafutwa na gazeti hili kufafanua madai ya kutumia nguvu kubwa katika kukidhibiti chama hicho, Mulongo alijibu kwa kifupi kuwa anawatakia kila la kheri kwa wanachotaka kukifanya.
“We ni mwanahabari nadhani unatambua mimi ni nani katika mkoa huu, basi kama ni hivyo nawatakia kila la kheri,’’alisema Mulongo.
OCD yeye alikataa kuzungumzia shinikizo hilo la CHADEMA akisema aulizwe Kamanda wa Polisi Mkoa, Loberatus Sabas, lakini naye alidai kutosikia kauli za OCD wake.

No comments:

Post a Comment