Saturday, March 23, 2013

Lwakatare atinga Mahakama Kuu


MAWAKILI wanaomtetea Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare jana wamewasilisha Mahakama Kuu ombi la kuitishwa kwa majalada ya kesi za ugaidi zilizofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kuzifanyia marejeo.
Maombi hayo ambayo yamepewa namba 14 ya mwaka huu, yaliwasilishwa jana kwa kiapo cha mmoja wa mawakili wa mshitakiwa huyo, Peter Kibatara.
Mawakili wa Lwakatare wanaomba Mahakama Kuu ipitie uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Dk. Eliezer Feleshi wa kuifuta hati ya awali ya mashitaka na kisha kuwafungulia kesi upya mteja wao na mwenzake Joseph Ludovick Rwezaura wakati kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya uamuzi wa dhamana, lakini ikashindwa kwa sababu DPP aliwasilisha hati ya kuifuta.
Maombi ya mawakili wa utetezi yaliomba washitakiwa wapewe dhamana wakati mawakili wakuu wa serikali, Ponsian Lukosi, Prudence Rweyongeza na Peter Mahugo waliomba mahakama isitoe dhamana kwa sababu makosa yanayoangukia katika sheria za ugaidi ya mwaka 2002 hayana dhamana.
Siku hiyo Hakimu Emilius Mchauru aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 20 kwa ajili ya kutolea uamuzi wa maombi hayo pamoja na mengine, lakini alijikuta akishindwa kufanya hivyo kwa sababu DPP alifuta kesi chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 kwa sababu hana haja ya kuendelea kuwashitaki.
Lakini dakika chache baada ya hakimu Mchauru kuwafutia kesi hiyo, wanausalama waliwakamata tena washitakiwa hao na kisha kuwapandisha mahakamani mbele ya hakimu mwingine, Alocye Katemana na wakili wa serikali Rweyongeza alianza kuwasomea mashitaka manne mapya katika kesi mpya iliyopewa Na. 6/2013 ambayo mashitaka ni yale yale yaliyokuwa kwenye hati ya mashitaka ya awali iliyofutwa na DPP.
Katemana aliwataka washitakiwa wasijibu chochote na akaamuru waende gerezani hadi Aprili 3, mwaka huu.
Habari za kuaminika toka ndani ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam zimesema kuwa tayari uongozi wa mahakama umeshatoa amri ya kuyaitisha majalada hayo mawili ya kesi yanayomkabili Lwakatare na mwenzake kwa ajili ya kuyafanyia marejeo.

No comments:

Post a Comment