MBOWE ASEMA HUO NI MTIRIRIKO WA MABAVU YA DOLA
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana ilimfutia kesi ya makosa ya ugaidi Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare na Ludovick Joseph, kisha kuwakamata tena na kuwafungulia kesi mpya yenye mashitaka yaleyale.
Awali ilielezwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka ( DPP), Dk. Eliezer Feleshi, aliwasilisha hati ya kuwafutia kesi washitakiwa kwa sababu hana haja ya kuendelea nayo.
Hata hivyo baada ya kuachiwa, Lwakatare na mwenzake walikamatwa tena na kufikishwa mahakamani hapo kisha kufunguliwa kesi mpya namba 6/2013 ambayo imepangiwa kwa Hakimu mpya, Aloyce Katemana.
Katika kesi ya awali namba 37/2013 iliyofunguliwa na Jamhuri dhidi ya Lwakatare na wenzake Machi 18, mwaka huu, jana ilikuwa imekuja kwa ajili ya Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru, kuitolea uamuzi wa ama kuwapatia dhamana washitakiwa hao au la.
Lakini Hakimu Mchauru alijikuta akishindwa kutoa uamuzi wake kwa sababu mawakili viongozi wa serikali, Ponsian Lukosi, Prudence Rweyongeza na Peter Mahugo, waliwasilisha hati hiyo ya DPP chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002.
“Kwa kuwa kesi hii Na. 37/2013 ilifunguliwa na upande wa Jamhuri Machi 18, mwaka huu, na leo kesi hii ilikuja kwa ajili ya mahakama kutolea uamuzi wa maombi ya washitakiwa kupatiwa dhamana au la, pamoja na maombi mengine…mahakama hii inasema haitaweza kutoa uamuzi wake kwa sababu DPP amewasilisha hati ya kutotaka kuendelea kuwashitaki, hivyo mahakama hii inawafutia kesi washitakiwa wote,” alisema Hakimu Mchauru.
Baada ya Hakimu Mchauru kuwafutia kesi, askari kanzu waliwakamata tena washitakiwa hao na kuwaweka chini ya ulinzi na ilipofika saa 4:20 asubuhi, waliingizwa tena katika ukumbi namba mbili wa mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi mwingine, Aloyce Katemana.
Mawakili wakuu wa serikali, Lukosi, Rweyongeza na Peter Mahugo walidai kuwa kesi hiyo ni mpya na imepewa Na. 6 ya mwaka huu, ambapo washitakiwa ni Lwakatare na Ludovick wanaotetewa na mawakili wa kujitegemea Prof. Abdallah Safari na Peter Kibatara.
Walisema kuwa hati hiyo ina mashitaka manne, ambapo shitaka la kwanza linaangukia kwenye Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002 na makosa matatu yote yanaangukia kwenye Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya mwaka 2002.
Wakili Rweyongeza alilitaja kosa la kwanza ambalo linawakabili washitakiwa wote kuwa ni kula njama kutenda kosa la jinai kinyume cha kifungu cha 284 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.
Alidai kuwa mnamo Desemba 28, mwaka jana, huko Kimara King’ong’o Stopover, wote kwa pamoja walitenda kosa hilo kwa kutaka kutumia sumu kwa lengo la kumdhuru Dennis Msacky, ambaye ni Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi.
Alilitaja kosa la pili kuwa ni la kula njama ambalo pia ni kwa ajili ya washitakiwa wote, ikiwa ni kinyume cha kifungu cha 24(2) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi Na. 21 ya mwaka 2002, kwamba washitakiwa hao walitenda kosa la ugaidi la kutaka kumteka Msacky.
Shitaka la tatu ambalo pia linawakabili wote wawili ni kupanga kufanya makosa ya ugaidi kinyume cha kifungu cha 59(a) cha Sheria ya Kuzuia ugaidi, kwamba Desemba 28, mwaka jana, walishiriki katika mkutano wa kupanga kufanya vitendo vya kumteka nyara Msacky.
Rweyongeza alidai kuwa shitaka la nne linamkabili Lwakatare peke yake, ambalo ni kuwezesha kutendeka kwa kosa la ugaidi kinyume cha kifungu cha 23(a) cha sheria ya kuzuia ugaidi.
Kwamba, Desemba 28, mwaka jana, Lwakatale akiwa ni mmiliki wa nyumba hiyo iliyopo Kimara King’ong’o kwa makusudi aliruhusu kufanyika kwa kikao hicho baina yake na Ludovick cha kutenda kosa la ugaidi la kutaka kumteka nyara Msacky.
Washitakiwa wote walikanusha mashitaka hayo na Hakimu Katemana alisema hawatakiwi kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, hivyo akaiahirisha kesi hiyo hadi Aprili 3, mwaka huu, itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.
Wakili wa utetezi Kibatara, aliomba mahakama isikilize ombi lake alilokuwa akitaka kuliwasilisha, lakini Hakimu Katemana alisema yeye ndiye kiongozi na mawakili wa utetezi na Jamhuri wapo chini yake na kwamba ana majukumu mengine hivyo hayupo tayari kusikiliza ombi hilo wala lile la upande wa Jamhuri.
Jamhuri iliomba mahakama imruhusu Ludovick aende kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya hatua zaidi za kipelelezi lakini hakimu huyo akaamuru washitakiwa wapelekwe gerezani.
Baada ya kesi hiyo kuahirishwa, wafuasi wa CHADEMA ambao baadhi yao walikuwa wamevalia sare walipaza sauti na kusema: “People’s Power. Hakuna kulala hadi kwanza walale wao.”
Mbowe anena
Akizungumza nje ya viwanja vya mahakama baada ya kesi kuahirishwa, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema kwanza asingependa kuingilia mtiririko wa mahakama.
Hata hivyo alizungumza kwa kifupi akisema kuwa wao wanafanya kazi za mageuzi kwa ajili ya kuwatetea raia wanyonge na maskini na kwamba kilichompata Lwakatare si kigeni, bali ni mtiririko wa mabavu ya dola dhidi ya wanamageuzi.
Lissu ang’aka
Akizungumza kwa simu, Wakili maarufu, Tundu Lissu, ambaye alikuwa miongoni mwa wanajopo wa utetezi wa Lwakatare katika kesi ya kwanza, alisema kitendo cha kumfutia kesi mshitakiwa kabla hajajibu mashitaka na kumfungulia mashitaka yaleyale, kinaonesha ni matumizi mabaya ya taratibu za kimahakama.
Alisema ni kitendo cha kutumia vibaya mahakama ili hakimu asitoe majibu kwa mambo ambayo yalikuwa yanatarajiwa kutolewa uamuzi jana.
“Leo tulitarajia kuwa tunakuja kujadili kama Lwakatare anapata dhamana au hapana, na pia kuja kuzungumzia kama mashitaka ambayo yaliletwa mahakamani yalikuwa na hati ya ridhaa ya DPP. Tulijiandaa kwa hayo, wala si mengine, sasa wamefika mahakamani wakamfutia mashitaka na kumfungulia mengine,” alisema.
Lissu aliongeza kuwa, mashitaka ya Lwakatare pamoja na kutajwa kuwa ni ya kigaidi, yapo katika kanuni za adhabu kama makosa ya kawaida kwa mujibu wa sheria kifungu cha 384, hivyo ni makosa yanayodhaminika.
Tanzania Daima
CHADEMA WATANZANIA WANAKIPENDA SANA HICHO CHAMA NA WANAHAMINI KUWA NDICHO CHAMA CHA UKOMBOZI KUTOKA KWA MAFISADI WALIO IKALIA HII NCHI KWA MUDA MREFU BILA MAENDELEO YEYOTE, ZAIDI NI KUJINUFAISHA WAO NA FAMILIA ZAO,MSIKATE TAMAA HAYO MAPITO TU, MABADILIKO YANAITAJI UVUMILIVU WA KHALI YA JUU,NAHAMINI MTAKUTANA NA MISUKOSUKO MINGI SANA LAKINI SIKU YA SIKU MTASHINDWA NA MTAONGOZA DPLA HII AMBAYO LEO HII INAWASUMBUA SANA,HATA MIMI HILO NALIONA WAZI HALINA KIFICHO KABISA, TUPO PAMOJA WANACHADEMA WEZANGU, HIYO KESI TUNASHINDA, HAKUNA UGAIDI WA KITOTO KAMA HUO DUNIANI WAMETENGENEZA VICHEKESHO KABISA.
ReplyDelete