Wednesday, March 27, 2013

Dk. Slaa ampiga kombora Nape Nnauye


KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema watu wanaosema chama hicho kinapata misaada kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuihujumu serikali, wanapaswa kupuuzwa na kudharauliwa.
Dk. Slaa alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, kabla ya kusaini mkataba wa ushirikiano wenye thamani ya zaidi ya sh mil. 400, baina ya chama hicho na kile cha Conservative cha watu wa Denmark (CPD).
Ingawa Dk. Slaa hakumtaja mtu, lakini ni dhahiri kwamba alikuwa akimjibu, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) taifa, Nape Nnauye, ambaye mwaka jana aliwahi kuishambulia CHADEMA kuwa inafanya usanii wa kuitisha harambee kwa ajili ya kuhalalisha mabilioni ya fedha inayopata kutoka kwa wafadhili wao.
Katika maelezo yake wakati huo, Nape alisema siri kubwa inayofichwa kuhusu mikataba na mabilioni wanayopewa CHADEMA ni kwa sababu wanaotoa fedha hizo wana ajenda ya kunyemelea rasilimali za nchi.
Akielezea mkataba huo jana, Dk. Slaa alisema umelenga kuwajengea uwezo wa kazi wanawake na vijana wa chama hicho zaidi ya 30,000 watakaokuwa na uwezo mzuri wa kueneza sera za CHADEMA baada ya mafunzo.
“Tulikuwa tunaambiwa CHADEMA inasaidiwa na mataifa ya nje kwa ajili ya kuihujumu serikali, sisi mikataba yetu iko hadharani mwenye kutaka kuijua anaweza akaisoma; hatuna siri kama wengine waliosaini mikataba 19 juzi na bado wanafanya siri wananchi wasijue kilichosainiwa,” alisema Slaa.
Aliongeza kuwa ni wakati wa serikali kujifunza kutoka kwao namna mikataba inayowahusu wananchi inavyopaswa kuwa wazi kwani rasilimali zote ni mali ya wananchi na siyo ya viongozi.
Alisema hivi karibuni serikali imesaini mikataba ipatayo 19 pasipo hata wabunge kujua na kwamba alipowauliza wabunge wa CHADEMA kama wanajua kilichosainiwa katika mikataba hiyo, hakuna aliyejua.
“Tunaposhirikiana na vyama vingine nje ya nchi, serikali ya CCM na idara ya usalama wa taifa wanatengeneza propaganda kuwa tuna dhamira ya kuihujumu nchi, hawa watu wa usalama waisaidie serikali kuonyesha matatizo ya Watanzania siyo kushinda na kutufuatilia,” alisema Slaa.
Aliongeza kuwa CHADEMA inafanya mambo kwa uwazi ili kuepuka propaganda zinazofanywa na serikali kupitia usalama wa taifa pamoja na CCM, kupotosha ukweli juu ya ushirikiano wake na vyama rafiki duniani.
Kwa upande wake mwakilishi wa CPD, Rolf Aagaard-Svendsen, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje katika chama hicho, alisema awali walifika Tanzania kuangalia namna ya kuwajengea uwezo vijana na wanawake wa CHADEMA na sasa wametekeleza dhamira hiyo.

No comments:

Post a Comment