MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), amesema kutokana na kuliongoza jimbo hilo kwa vipindi viwili mfululizo, sasa ametangaza rasmi kutowania nafasi hiyo tena katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Alisema kazi kubwa aliyoifanya kwa wananchi wa jimbo lake, imefika wakati sasa wa yeye kupumzika kuweza kupisha watu wengine waweze kuliongoza jimbo hilo, huku akiahidi kuendelea kufanya shughuli za maendeleo pasi ya kuwa mbunge.
Kutokana na kauli hiyo aliiyoitoa mbele ya wananchi katika mikutano yake ya hadhara iliyofanyika katika Kata za Bitale na Mahembe iliyofanyika juzi na jana, iliwafanya baadhi ya wananchi kuangua vilio huku wakipinga hatua yake ya kutaka kutogombea tena nafasi hiyo.
Zitto ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Taifa, alisema ni muhimu kwa wanasiasa hasa wanaojitambua kutumia nafasi zao kupima uwezo wa namna ya kuwaongoza wananchi kwa kusukuma maendeleo yao, kuliko kutumia muda mwingi kung’ang’ania madaraka.
“Ninachokifanya ndugu zangu ninaomba mjiandae kisaikolojia katika hili, ninatamka wazi kuwa mwaka 2015 sitagombea ubunge tena katika jimbo letu hili la Kigoma Kaskazini na lengo la kufanya hivi ni kutoa fursa kwa watu wengine kutoka ndani ya Chadema nao waonyeshe uwezo wao wa kuwahudumia wananchi.
“Pia ni vema muone naweza kufanya kazi ya kusukuma shughuli za maendeleo hata kama sitagombea tena nafasi hii ya ubunge. Leo tulipofikia unaweza kukutana na wanasiasa na hata kuwaona hufanya kitu fulani kwa sababu tu wanataka kitu fulani.
“Mimi nafanya kwa sababu ya kuipenda Kigoma yetu, ni wazi kwa muda mrefu mkoa wetu ulikuwa hauna hadhi na hata wananchi wake kukosa heshima mbele ya jamii. Lakini leo hii ninaacha ubunge ni wazi hata mwananchi wa Kigoma akifika eneo hili na kusema yeye ni mwenyeji wa mkoa wetu uheshimika mbele ya jamii.
“Hata kama Mungu atanichukua leo nitakufa kwa furaha kwa kuona Mkoa wa Kigoma umekuwa na heshima mbele ya jamii pamoja na watu wake, barabara zetu zinafunguka na hata tunaona namna maliasili zetu namna zinavyojitangaza zenyewe bila hata kutumia nguvu.
“Bado kuna jambo moja ambalo kwangu linaniumiza kila kukicha, ni kuona namna nchi yetu ilivyokuwa na rasilimali lakini zimegeuka kuwa ni balaa huku mamlaka zinazohusika hazichukui hatua mapema na badala yake hushituka baada ya kuona kuna machafuko,” alisema Zitto.
Alisema pamoja na hatua ya machafuko yaliyotokea mkoani Mtwara ni vema Serikali ikaanza sasa kufanyika kazi hata suala la gesi iliyogundulika katika mwambao wa Ziwa Tanganyika, huku akimtaka Rais Jakaya Kikwete kutoa kauli kabla ya mambo hayajachafuka.
“Katika suala la gesi katika Mkoa wetu wa Kigoma ni wazi ipo Ziwa Tanganyika, ilikuja kampuni ya Total toka nchini Ufaransa ambapo katika utafiti wao waligundua gesi nyingi, lakini taarifa yao walikwenda kuitoa Jamhuri ya Demokrasia na Kongo badala ya kuja huku kwetu Tanzania.
“Ninapenda kuweka wazi ni vema Rais Kikwete atoe kauli ya kina kuhusu suala hili, kwani hata ziara yake aliyoifanya Ufaransa hivi karibuni alifanya mazungumzo nao, sasa ni haki yetu wana Kigoma kujua nini alichozungumza nao hii kampuni ya Total,” alisema Zitto.
Mtanzania
Hongera sana Wabunge wa CHADEMA kwa kupigania maslahi ya umma,kweli hiki ndicho cha Watanzania.
ReplyDelete